Wednesday, October 31, 2012

JITIHADA ZA KUPAMBANA NA MALARIA ZINAHITAJIKA ZAIDI










Mratibu wa Malaria mkoani Ruvuma Bi. Kibua Kakolwa.  (Picha na Kassian Nyandindi)



Na Kassian Nyandindi, 
Songea.

 

UGONJWA ambao ni tishio kwa maisha ya wananchi wengi ni malaria, na hususani kwa wale walio maskini duniani ndio huteseka nao kwa kiasi kikubwa , hivyo jitihada za kuendelea kupambana nao katika kuutokomeza zinahitajika zaidi ili jamii iweze kusonga mbele kimaendeleo.

 
Ni ugonjwa unaoenezwa na mbu jike aina ya Anofelesi mwenye vimelea vya ugonjwa huo, kwa kuuma na kufyonza damu ya mtu asiye na vimelea hivyo kisha kumuambukiza.
 
Hapa kwetu Tanzania ugonjwa wa malaria umekuwa tishio kwa maisha ya wananchi wengi, hususani akina mama wajawazito na watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano, ambao kutokana na mdudu huyo anayeambukiza kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.
 
Watu zaidi ya milioni 20 inakadiriwa wanaokwenda hospitali kupatiwa matibabu kila mwaka hapa nchini, hugundulika kuwa na vijidudu vya ugonjwa huu ambapo kati ya hao 60,000 hufariki dunia wengi wao wakiwa watoto walio chini ya umri huo.
 
Katika nchi za Afrika Mashariki inakadiriwa kuwa na wagonjwa milioni 60 na watu milioni moja huripotiwa kufa duniani kila mwaka.
 
Watu 291 huripotiwa kufa kila siku kutokana na ugonjwa huo wengi wao wakiwa watoto wadogo, ambapo takwimu hizo zinafafanua kuwa kila baada ya saa moja watu wanaokufa kwa ugonjwa huu ni zaidi ya kumi.
 
Idadi hii ni kubwa hasa kwa kuzingatia kwamba tiba na kinga ya ugonjwa huo ipo lakini bado idadi ya vifo inaongezeka kila kukicha na kutishia uhai wa wananchi wengi.
 
Akizungumza na Waandishi wa makala haya Mratibu wa Malaria mkoani Ruvuma Bi. Kibua Kakolwa anasema, elimu juu ya kupambana na kutokomeza ugonjwa wa malaria hapa nchini imekuwa ikiendelea kutolewa na serikali kwa kushirikiana na taasisi binafsi, ikiwa ni lengo la kuhakikisha kwamba jamii inaepukana na ugonjwa huo kwa namna moja au nyingine.

“Elimu ya namna ya kupambana na ugonjwa huu  inapaswa kutiliwa mkazo wakati wote, kutokana na kwamba malaria ni ugonjwa hatari ambao unagharimu maisha ya watu wengi”, anasema Bi. Kakolwa.

Anasema vifo vingi vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara hivyo anasisitiza wataalamu wa afya hawana budi kuendelea kuelimisha wananchi kupitia mikutano au makongamano mbalimbali ambayo yatalenga, kusaidia jamii kuweka mazingira yao katika hali iliyosalama ambayo haitaweza kutengeneza mazalia ya mbu ambao ndio chanzo kikuu cha kueneza ugonjwa huu.

Mratibu huyo anasema wanachohitaji ni kuona serikali na wadau mbalimbali wa afya, wanaongeza nguvu katika kujenga ushirikiano wa kupambana na ugonjwa huo ili nguvu kazi ya taifa hili iweze kusonga mbele.

Akifafanua juu ya hali ya ugonjwa wa malaria na utekelezaji kazi mkoani Ruvuma, katika kipindi cha mwaka 2011 hadi sasa Bi. Kakolwa anasema mkoa ulilaza wagonjwa wenye umri chini ya miaka mitano wapatao 21,940 na walio zaidi ya umri huo walikuwa 21,819.

Hali kadhalika katika kipindi hicho, vifo vilivyosababishwa na ugonjwa huo kwa watoto chini ya miaka mitano vilikuwa 334 na kwa wagonjwa waliozaidi ya umri huo vilikuwa 318.

Anasema katika kipindi cha mwaka 2008, 2009, 2010 na 2011 watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa huu walikuwa 3,451.

Mkoa wa Ruvuma una jumla ya wilaya tano ambazo ni Mbinga, Namtumbo, Tunduru, Songea na Manispaa ya Songea ambapo katika wilaya hizo malaria bado inaendelea kushika namba moja kati ya magonjwa mengine yaliyopo, hivyo kuendelea kuwa tishio kwa afya na ustawi wa wananchi wanaokadiriwa mkoani humo kufikia milioni 1.41.

Anafafanua kuwa takwimu za mwaka jana zinaonesha mkoa ulipokea idadi ya wagonjwa wa nje wa malaria wenye umri chini ya miaka mitano 216,311 ambao ni sawa na asilimia 45 ya wagonjwa waliopokelewa.

Anaongeza kwamba wagonjwa wenye umri zaidi ya miaka mitano walikuwa 207,664 ya wagonjwa wa nje waliopokelewa ikiwa ni sawa na asilimia 40 ya wagonjwa wote.

Bi. Kakolwa akielezea mafanikio katika miaka mitatu mfululizo takwimu zinaonesha wagonjwa wa malaria wamepungua kwa wastani wa asilimia 6.5 na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vimeweza kupungua kwa wastani wa asilimia 15.4.

Kadhalika jumla ya vyandarua 706,219 vimegawiwa kwa wananchi katika kila sehemu ya malazi mkoani humo, na kufanikiwa kwa asilimia 112 ambapo taasisi binafsi 33,814 zimegawiwa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu.

Vilevile matumizi ya chandarua chenye dawa kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano yamefanikiwa kwa asilimia 75 na kuwahi matibabu yamefanikiwa kwa asilimia 71.

Pamoja na mafanikio hayo Mratibu huyo amezitaja changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kuwa ni taarifa sahihi za malaria kutoka katika wilaya za mkoa huo zimekuwa zikipatikana kwa kuchelewa, jambo ambalo linakwamisha usambazaji wa dawa kutofanyika kwa wakati katika vituo vya kutolea huduma.

Anasema hali ya upatikanaji wa dawa za kutosha kwa ajili ya kutibu malaria katika vituo hivyo, imekuwa ni tatizo kubwa ambapo uwepo wa uhaba wa SP katika vituo hivyo kunaathiri akina mama wajawazito, kwani dawa hizo huzuia maambukizi ya malaria kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Changamoto nyingine anasema ni ushiriki duni wa jamii katika kuboresha mazingira ya makazi yao ili kuondoa vyanzo vya mazalia ya mbu na kwamba baadhi ya wananchi bado hawajaweza kuchukua hatua za haraka za kupata matibabu kwenye vituo vya kutolea huduma mara waonapo dalili za ugonjwa huo.

Vilevile kumekuwa na matumizi yasiyo sahihi ya vyandarua ambapo baadhi ya wananchi wanatumia chandarua kufungia bustani ili kuzuia kuku wasiharibu kile ambacho kimeoteshwa katika bustani hizo.

Akizungumzia mikakati ambayo imepangwa katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria anaeleza kuwa, wamekuwa wakiendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu ukubwa wa tatizo la malaria na jinsi ya kujilinda na ugonjwa huo huku jamii ikihamasishwa kuwa na tabia ya kuwahi matibabu ya malaria haraka, mara waonapo dalili zake na pia kutumia dawa sahihi za kutibu malaria.

Mkakati mwingine ni kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vinatoa matibabu sahihi ya malaria kwa kuhakikisha mgonjwa anayehisiwa ana ugonjwa huo, anapimwa kabla ya matibabu na watoa huduma kuheshimu majibu ya vipimo vya mgonjwa husika.

Bi. Kakolwa anaeleza kwamba katika jitihada za kupambana na ugonjwa huo wamekuwa wakihamasisha matumizi sahihi ya vyandarua vyenye dawa ya kudumu, na kutoa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu kwa watoto wachanga na akina mama wajawazito kupitia mpango wa hati punguzo.

Pia anasema wamekuwa wakizuia maambukizi ya malaria kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kwa kutumia dawa aina ya SP katika kliniki za afya ya mama na mtoto na kwamba hutoa elimu kwa jamii kuhusu usafi wa mazingira ili kupunguza mazalia ya mbu waenezao ugonjwa huo.

Kuhusu utekelezaji wa mikakati hiyo Bi. Kakolwa anafafanua kuwa elimu imetolewa katika kila wilaya, kulingana na mipango iliyowekwa kwa kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali ambazo ni PSI, COMMIT na CSSC ambapo elimu hiyo imetolewa kwa njia mbalimbali kama mawasiliano ya moja kwa moja, mikutano ya hadhara, matangazo na kwa kutumia michezo na ngoma.

Kwa mwaka 2011 takwimu zinaonesha kuwa utoaji wa dawa aina ya SP ya kwanza kwa akina mama wajawazito imetekelezwa kwa asilimia 46.5 wakati kiwango cha mwaka 2010 kilikuwa asilimia 59.9 ambapo SP ya pili ilifikia asilimia 35.1.

Jumla ya hati punguzo za wajawazito 36,588 zimetolewa katika mwaka 2011 kati ya hizo hati punguzo 19,721 sawa na asilimia 54 zilinunuliwa vyandarua na kwamba hati punguzo za watoto zipatazo 28,595 zimetolewa na asilimia 55.4 ambayo ni sawa na hati punguzo 15,781 zilinunuliwa vyandarua.

Binafsi tunasema malaria husababisha upotevu wa nguvu kazi ya Taifa letu ukizingatia kwamba huwakumba hasa watoto wadogo na katika kuhamasisha juhudi hizo kila Mtanzania analojukumu la kujilinda mwenyewe pamoja na familia yake katika kudhibiti ugonjwa huo hapa nchini.
 
Tanzania ni moja kati ya nchi zinazopambana dhidi ya ugonjwa wa malaria duniani ni vyema tuhamasishe sekta zote za jamii katika kupambana nao ikiwemo kujikinga kwa kulala ndani ya chandarua kilichowekwa dawa, kutambua na kuutibu mapema pamoja na kuangalia afya ya mama mjamzito mara kwa mara.
 





No comments: