Wednesday, October 31, 2012

WANAFUNZI HATARINI KUANGUKIWA NA JENGO WANALOSOMEA


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
HUENDA maafa makubwa yatajitokeza katika shule ya Msingi Myangayanga, iliyopo kijiji cha Myangayanga Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma , kutokana na jengo moja linalotumika kusomea wanafunzi kuwa katika hali mbaya.
 
Mwandishi wa habari hizi ambaye alitembelea shule hiyo ameshuhudia jengo hilo lilivyokuwa, ambapo ni chakavu na limekuwa na nyufa kubwa huku watoto na walimu wa shule hiyo wakiendelea kulitumia wakati wa vipindi vya masomo.
 
Jengo hilo ambalo lina vyumba vinne limekuwa likitumika kusomea wanafunzi wa darasa la awali, darasa la tatu na la nne na kwamba lina ofisi tatu za walimu hivyo huenda likabomoka wakati wowote.
 
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bw. Maxensius Kiyao ameliambia gazeti hili kwamba jumla ya wanafunzi 140 na walimu sita wakati wa masomo kwa siku hulitumia jengo hilo kutokana na upungufu wa vyumba vya kusomea, jambo ambalo ni hatari kwao.
 
Alisema jitihada za kulikarabati zimegonga mwamba kutokana na kukosa fedha, hivyo uongozi husika wa halmashauri ya kijiji cha Myangayanga na wa wilaya ya Mbinga, unapaswa kuchukua hatua za makusudi katika kunusuru hali hiyo ili lisiweze kuleta madhara makubwa baadaye.
 
Bw. Kiyao alisema tatizo hili ni la muda mrefu lina zaidi ya miaka miwili sasa iliyopita na taarifa katika ngazi za juu halmashauri ya wilaya hiyo zimekwisha pelekwa lakini utekelezaji hakuna.
 
“Jengo hili kama unavyoliona limechakaa na lina nyufa kubwa jambo ambalo ni hatari na linatishia amani kwa watoto wetu, linahitaji nguvu kubwa katika kulikarabati”, alisema.
 
Alifafanua kwamba uongozi husika wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga baada ya kupewa taarifa juu ya hali mbaya ya jengo hilo , ulituma wataalamu kutoka idara ya ujenzi ambao walikwenda kufanya upembuzi yakinifu juu ya tatizo hilo .
 
Alisema tokea wataalamu hao wamekwenda kufanya kazi hiyo ni miaka miwili sasa imepita hakuna jitihada zilizozaa matunda na jengo linaendelea kuwa katika hali mbaya.
 
Kadhalika aliongeza kuwa shule hiyo inakabiliwa na tatizo la nyumba za walimu wengi wao hupanga uswahilini ambapo zilizopo ni tatu tu.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa kijiji hicho walisema hata Mbunge wao wa Mbinga Mashariki Bw. Gaudence Kayombo wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita mwaka 2010, walimweleza juu ya tatizo hilo na kuwaahidi kwamba atachangia nguvu zake kwa kuwanunulia vifaa vya viwandani wakati ukarabati utakapoanza.
 
Walisema tokea Mbunge huyo atoe ahadi hiyo ya kuwachangia hawajawahi kumuona tena kijijini hapo na hakuna taarifa zozote zinazoonesha jitihada za kumaliza kero hiyo na wananchi wapo tayari kuchangia nguvu zao kama vile tofari, mchanga na mbao.
 
“Huyu Mbunge tumemuona hapa wakati wa kampeni tu, tokea amepata madaraka hajawahi hata kututembelea hapa kijijini, alisema Alfrida Komba.
 
Mbunge Kayombo alipoulizwa juu ya suala hilo alisema yeye hajawahi kutoa ahadi yoyote kwa wananchi hao ya kuchangia ukarabati wa jengo hilo .
 
“Hapana sijawahi kutoa ahadi ya mchango wowote katika kulikarabati jengo hilo , ila nakumbuka mtaalamu wa ujenzi tulimtaka aende kule ili aliangalie na kutuletea majibu kama jengo linafaa kukarabatiwa au kulibomoa lote na kujenga upya”, alisema.
 
Kwa ujumla shule ya msingi Myangayanga ina jumla ya wanafunzi 391 kutoka darasa la awali mpaka darasa la saba hivyo jitihada za kuboresha mazingira ya shule hiyo zinahitajika kutekelezwa mapema kabla ya kujitokeza matatizo makubwa baadaye.
 
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya hali hiyo ofisa elimu shule za Msingi Wilaya ya Mbinga Bw. Mathias Mkali alisema taarifa juu ya ubovu wa jengo hilo ofisi yake haina taarifa, ambapo alisema atafanya utaratibu wa kufuatilia tatizo hili.
 
Bw. Mathias alisema hivi sasa utaratibu wa kujenga miundombinu ya shule ikiwemo majengo ya shule na nyumba za walimu ni jukumu la halmashauri ya kijiji husika kwa kushirikisha wananchi kuchangia nguvu zao na serikali kuwasaidia vifaa vya viwandani.
 
Akizungumzia suala la upungufu wa nyumba za walimu alisema wilaya hiyo imekuwa na matatizo makubwa ya upungufu wa nyumba za walimu na kwamba zilizopo sasa nyingi ni chakavu.
 

No comments: