Wednesday, October 31, 2012

WALIOJERUHIWA KATIKA VURUGU ZA UCHAGUZI WA UDIWANI SONGEA WAENDELEA VIZURI



Na Amon Mtega,
Songea.
  
WAFUASI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na CHADEMA ambao walijeruhiana katika mkutano wa mwisho wa kampeni za uchaguzi, kuwania nafasi ya udiwani kata ya Mletele iliyopo manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, na kulazwa katika Hospitali ya Songea [HOMSO] sasa wanaendelea vizuri baada ya afya zao kuanza kurejea katika hali ya kawaida.

Mganga mkuu mfawidhi wa hospital hiyo Dkt.  Benedick Ngaiza alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Dkt. Ngaiza alisema katika watu waliojeruhiwa wanne walitibiwa na kuondoka na waliokuwa wamelazwa walikuwa watatu ambao mpaka sasa bado wanaendelea na matibabu ambapo mmoja ni Mashaka Mbawala [45] aliumizwa mikononi na kichwani.

“Kwa mgonjwa aliyekuwa na jeraha la kusababishwa na kitu chenye ncha kali inatakiwa uwangalizi wa karibu  hata kama hali yake inaendelea vizuri”

“Hivyo hata wakipata bahati ya kuruhusiwa bado wataendelea kuangaliwa ili kubaini kama kunatatizo jingine linalo jitokeza”, alisema Dkt. Ngaiza.

Majeruhi hao walijeruhiana Oktoba 27 mwaka huu majira ya saa tisa mchana wakati wafuasi hao wakiwa kwenye mkutano wa mwisho wa kufungia  kampeni  za uchaguzi mdogo kuwania nafasi ya udiwani katika kata ya Mletele iliyopo manispaa ya Songea.

Pamoja na patashika hilo CCM iliibuka mshindi kwenye kinyang’anyiro hicho kwa mgombea Maurus Lungu kushinda katika nafasi hiyo.

No comments: