Wednesday, October 31, 2012

SHULE YA MSINGI NGADINDA SONGEA VIJIJINI WAJISAIDIA VICHAKANI












Wanafunzi wa darasa la awali shule ya msingi Masumuni iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakiwa wamepanga foleni kwenda kupokea uji kwa ajili ya kifungua kinywa majira ya asubuhi kama walivyokutwa na mpiga picha wetu. Serikali hapa nchini imekuwa ikisisitiza shule nyingi kutoa huduma ya chakula kwa wanafunzi mashuleni ili waweze kuondokana na njaa na hatimaye wafanye masomo yao vizuri. (Picha na Kassian Nyandindi)

Na Dustan Ndunguru,
Songea.


WANAFUNZI na walimu wa shule ya msingi Sokoine kijiji cha Ngadinda Songea vijijini mkoani Ruvuma, wanalazimika kujisaidia vichakani kutokana na uhaba wa vyoo uliopo shuleni hapo.

Shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na uchanga wake, hivyo jitihada za kuinusuru ili iweze kuondokana na matatizo hayo zinahitajika kwa uharaka zaidi ili wanafunzi na walimu wasipatwe na magonjwa ya mlipuko.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mwalimu mkuu wa shule hiyo  Bw. Theoderi Moyo alisema, mahitaji halisi ya matundu ya vyoo ni 16  na sasa shule ina matundu manne tu ambayo hayatoshelezi.

Kutokana na hilo walimu wamekuwa wakijisaidia katika vyoo vya nyumba za watu wanaoishi jirani na shule hiyo.


Alisema licha ya kufanya vikao mbalimbali ambavyo vilijumuisha wazazi na walimu bado suala hilo limekuwa gumu katika utekelezaji hivyo jitihada zinahitajika zaidi katika kutatua suala hilo.

Alieleza kwamba uongozi husika wa Halmashauri ya wilaya ya Songea umekwisha pelekewa taarifa, lakini hadi sasa hakuna utekelezaji au hatua zilizochukuliwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Ngadinda Bw. John Komba alisema, tatizo kubwa lililopo katika kijiji chao ni ubishi wa baadhi ya wananchi kutoshiriki katika shughuli za maendeleo hususani kwa kazi za kujitolea.  

Bw. Komba alifafanua kuwa Kutokana na hali hiyo wanakusudia kutumia sheria ndogo ndogo zilizowekwa na serikali ya kijiji hicho, ili kuwabanaa wale wote wasiokuwa tayari kushiriki katika maendeleo.






























































No comments: