Wednesday, October 31, 2012

VIJANA WASHAURIWA KUJIUNGA NA VYUO VYA UFUNDI STADI












  


Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi Dkt. Shukuru Kawambwa. (Picha na mtandao)


Na Mwandishi wetu,
Songea.

VIJANA mkoani Ruvuma wametakiwa kubadilika kimawazo na kuacha tabia ya kusubiri ajira za serikali na taasisi za umma, badala yake wajiunge katika vyuo vya ufundi stadi (VETA) ili waweze kupata ujuzi utakaowafanya wajiajiri wenyewe na kumudu kuendesha maisha yao.

Wito huo umetolewa na mkuu wa chuo cha Veta Songea Bw. Gideon Ole Ruimbe wakati akizungumzia mpango wa chuo hicho kupanua wigo wa mafunzo ili kuwawezesha vijana wengi kupata ujuzi utakaowafanya waweze kujitegemea na kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Bw. Ole Ruimbe alisema wakati umefika kwa vijana hapa nchini, kupanua fikra zao zaidi na kuangalia mustakabali wa maisha yao, kutokana na tatizo kubwa la ajira lililopo sasa.


“Wasipofanya hivyo watajikuta wakiwa mzigo mkubwa katika familia zao  hivyo njia pekee ya kujinasua na tatizo hilo ni wao wenyewe kubadilika, na kujiunga na vyuo vya ufundi ili kupata ujuzi wa mambo mbalimbali”, alisema.

Aliongeza kuwa tatizo kubwa lililopo kwa vijana  wanaomaliza masomo ya sekondari na vyuo ni kupata ajira kutokana na kutawaliwa na tamaa jambo linalowachelewesha kusonga mbele kimaendeleo katika Nyanja mbalimbali.  

Vilevile alisikitishwa na idadi ndogo ya vijana wanaojiunga na chuo hicho kutoka mkoa wa Ruvuma, kwani hailete picha nzuri licha ya kuwa chuo hicho kina sura ya kitaifa.

Wito umetolewa kwa wazazi na walezi na hata vijana wenyewe kuchangamkia nafasi hizo za kujiunga na vyuo vya ufundi stadi.

No comments: