Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wameulalamikia uongozi wa idara ya afya wilayani humo, kwa kushindwa kudhibiti vitendo vya wizi wa madawa ya kutibu wagonjwa, ambao umekuwa ukifanyika katika hospitali ya wilaya hiyo.

Sambamba na hilo imeelezwa katika kikao hicho kwamba licha ya tatizo hilo kuwepo, pia kumekuwa na upungufu mkubwa wa madawa hayo katika zahanati na vituo vya afya.

Malalamiko hayo yalitolewa hivi karibuni katika kikao cha baraza la madiwani kilichoketi kwenye ukumbi wa jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.

Walisema dawa zinazosafirishwa na kupelekwa katika vituo vya afya au zahanati huko vijijini, wakati mwingine zimekuwa hazifikishwi kwenye maeneo husika, jambo ambalo limekuwa likisababisha wagonjwa kukosa matibabu.
Diwani wa viti maalum kata ya Mbinga mjini Bi. Grace Millinga, alisema utafiti unaonesha kwamba tatizo hili limekuwa sugu katika wilaya ya Mbinga, hivyo hatua za makusudi inabidi zichukuliwe ili kuwabaini watu wanaohusika na kuhujumu madawa hayo.
“Hizi dawa wakati mwingine hazipelekwi kwenye vituo vyetu vya afya huko vijijini, dawa nyingi zinaishia njiani, tunaomba halmashauri yetu iunde tume maalumu ya kuchunguza tatizo hili na kikao kijacho cha baraza tupate majibu”, alisema Bi. Millinga.

Naye diwani wa kata ya Mbangamao Bw. Christantus Mbunda alisema mbele ya baraza hilo kuwa, hata ukihitaji matibabu katika hospitali ya wilaya ya Mbinga, wakati mwingine mgonjwa anapohitaji kupewa hata dawa aina ya panado imekuwa ni tatizo hivyo viongozi husika wanapaswa kuchukua hatua madhubuti ili kuweza kumaliza tatizo hilo.

Alipotakiwa kujibu hoja hizo katika kikao hicho cha baraza la madiwani Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Mbinga Bw. Damas Kayera, alikiri kuwepo kwa matatizo hayo na kusema hatua zimekwisha anza kuchukuliwa ili kudhibiti hali hiyo.