Friday, December 30, 2016

NHIF YAVUNA WANACHAMA MAHANJE SACCOS

Na Julius Konala,      
Songea.

MFUKO wa Taifa Bima ya Afya (NHIF) mkoani Ruvuma, umevuna wanachama zaidi ya 100 wa chama cha ushirika wa akiba na mikopo Mahanje SACCOS waliopo katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani humo baada ya kujiunga na mfuko huo.

Wanachama hao wamejiunga na NHIF baada ya kuhamasika na maelezo yaliyotolewa na Ofisa wanachama wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya mkoa wa Ruvuma, Anthony Mgina alipopewa nafasi ya kuelezea faida za mfuko huo katika mkutano mkuu wa 19 wa chama hicho uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Tumaini Madaba uliopo mjini hapa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu, wanachama hao walisema kuwa wameamua kujiunga na mfuko huo kwa lengo la kupata huduma mbalimbali za matibabu kwa urahisi pamoja na kupunguza pia gharama za matibabu hayo.

Wanachama hao walidai kuwa wananchi wengi wamekuwa wakikabiliwa na tatizo kubwa la kushindwa kumudu gharama za matibabu, kwa kushindwa kujiunga na mfuko huo.

WANACHAMA MAHANJE SACCOS WALALAMIKIA WAKAGUZI WA COASCO SONGEA

Na Julius Konala,       
Songea.

WANACHAMA wa chama cha akiba na mikopo Mahanje SACCOS katika Halmashauri ya Madaba wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wameilalamikia Ofisi ya ukaguzi wa vyama hivyo COASCO mkoani hapa kwa madai kuwa wameshindwa kutoa taarifa ya ukaguzi wa chama hicho tangu mwaka 2014.

Malalamiko hayo yalitolewa jana na wanachama hao kwenye mkutano mkuu wa 19 wa chama hicho, uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Tumaini uliopo mjini hapa, ambapo walidai kuwa hali hiyo inasababisha chama chao kushindwa kupata mikopo na kufanya shughuli zao mbalimbali za kimaendeleo.

Akichangia hoja katika mkutano huo mshauri wa chama hicho, Nathan Malangalila alisema kuwa vyama vingi vya ushirika wa akiba na mikopo vimekufa kwa sababu ya kukosa usimamizi wenye uongozi makini pamoja na kushindwa kutoa ripoti mbalimbali za ukaguzi.

HALMASHAURI MANISPAA SONGEA YAFANIKIWA KUKUSANYA MAPATO ZAIDI YA BILIONI MOJA

Ofisi kuu za Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imefanikiwa kukusanya mapato kutoka katika vyanzo vyake vya ndani kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 1.1 katika kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Disemba mwaka huu.

Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kwamba katika kipindi cha mwaka huu wa fedha Manispaa hiyo inatarajia kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 3.3.

Midelo alifafanua kuwa makusanyo hayo ni sawa na asilimia 33.27 na kwamba lengo la kufikia asilimia 100 ya makusanyo linatarajiwa kufikia kabla ya mwishoni mwa mwaka wa fedha Juni 30, 2017.

AFARIKI DUNIA BAADA YA NYOKA WAKE KUPIGWA MAWE NA KUUAWA

Na Mwandishi wetu,     
Songea.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mkazi mmoja ambaye anaishi wa mtaa wa Mateka kata ya Mateka Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Denis Komba (26) amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa Songea mkoa hapa, baada ya watu wenye hasira kumuua kwa mawe na fimbo nyoka aliyekuwa amembeba kwenye mfuko wa jaketi.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Komba kabla ya kufariki dunia alikuwa amekodi pikipi ya Kassian Haulle (24) mkazi wa Mpitimbi yenye namba za usajili MC 724 AKB aina ya Sunlg, ili apelekwe nyumbani kwake anakoishi Mateka.

Zubery Mwombeji.
Aidha walipofika eneo ilipokuwa zamani Benki ya Posta mjini hapa barabara kuu ya Sokoine, dereva wa pikipiki alianza kuhisi kwamba kuna kitu kinamtekenya na kumgonga gonga sehemu ya mgongoni na kwamba alipogeuka nyuma ili aweze kujua nini, ndipo alimuona nyoka mkubwa amesimamisha kichwa huku akiwa amebebwa na mteja huyo aliyekodi pikipiki yake.

Kwa upande wake Haulle alisema kuwa, mara baada ya kumuona nyoka huyo alilazimika kuruka kutoka kwenye pikipiki hiyo ambapo baada ya kuanguka nyoka huyo alikimbilia kwenye Kalavati la maji machafu lililopo kando kando ya barabara na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada ndipo kundi la vijana wenzake ambao ni waendesha pikipiki walijitokeza na kuwasili katika eneo la tukio hilo kwa lengo la kumsaidia mwenzao.

Kabla ya vijana hao hawafanya jambo lolote marehemu Komba ambaye alikuwa amembeba nyoka huyo, aliwaomba vijana hao na watu wengine waliofika katika eneo hilo la tukio wasimpige nyoka wake, kwani iwapo watampiga na kufa yeye pia atapoteza maisha.

Tuesday, December 27, 2016

WAFANIKIWA KUSAMBAZA VYANDARUA KWA WATOTO MASHULENI

Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

KATIKA kuhakikisha kwamba ugonjwa hatari wa malaria unaendelea kudhibitiwa, Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma katika kipindi cha mwezi Oktoba mwaka jana hadi Septemba mwaka huu, imesambaza vyandarua 42,174 kwa watoto wa shule za msingi na sekondari zilizopo wilayani humo. 

Aidha hali ya maambukizi ya ugonjwa huo katika wilaya hiyo imepungua kwa asilimia 24 kutokana na wataalamu wa afya kuendelea kuhimiza wananchi kuweka mazingira yao wanayoishi katika hali ya usafi wakati wote ili kuepukana na mazalia ya mbu wanaobeba vimelea vya ugonjwa huo.

Kaimu mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Mbinga, Sarah Komba alisema hayo wakati alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya halmashauri yake ilivyojiwekea mikakati ya kupambana na ugonjwa huo kwa lengo la kupunguza maambukizi na vifo visivyokuwa vya lazima vitokanavyo na malaria.

MBINGA WAVUKA LENGO UTOAJI CHANJO KWA WATOTO WADOGO

Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

IDARA ya afya kupitia kitengo chake cha huduma ya afya, uzazi na mtoto katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kimeweza kuvuka lengo la kitaifa kwa kutoa chanjo watoto 14,436 sawa na asilimia 98.7 ya waliochanjwa chanjo za kuzuia magonjwa ya aina mbalimbali wilayani humo.

Watoto waliochanjwa ni wale wenye umri wa mwaka mmoja na kwamba kuna jumla ya chanjo kumi ambazo mtoto huchanjwa kwa awamu tatu tofauti na kuweza kufikia idadi ya chanjo hizo.

Sunday, December 25, 2016

WANANCHI SONGEA WATAKIWA KUPUNGUZA TATIZO LA UTAPIA MLO KWA WATOTO WADOGO

Baadhi ya Wakazi mji mdogo wa Peramiho mkoani Ruvuma, wakisikiliza kwa makini uzinduzi wa kampeni ya kupunguza na kuzuia udumavu kwa watoto.
Na Mwandishi wetu,    
Songea.

WANANCHI wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wametakiwa kuwa na mikakati na mipango thabiti, yenye kulenga kupunguza tatizo la utapia mlo wilayani humo ambao umekuwa ukiwaathiri watoto wadogo katika makuzi yao, kwa kuwafanya waonekane kuwa wamedumaa.

Mwito huo umetolewa juzi na Katibu tawala wa wilaya hiyo, Pendo Daniel alipokuwa akizungumza na wananchi wa mji mdogo wa Peramiho wilayani hapa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupunguza na kuzuia udumavu kwa watoto hao.

Alisema kuwa serikali tayari imekwisha agiza, kutenga na kuongeza bajeti ya lishe katika ngazi zote ikiwemo shilingi 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano kwa mwaka na kwamba, maagizo hayo tayari yametolewa kwenye ngazi husika katika halmashauri zote za mkoa huo.

Saturday, December 24, 2016

VIFO VYA WATOTO WADOGO MBINGA VYAPUNGUA

Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa vifo vitokanavyo na watoto waliochini ya umri wa miaka mitano katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, vimepungua kwa kiasi kikubwa ambapo katika kipindi cha mwezi Oktoba mwaka jana hadi Septemba mwaka huu ni watoto wa nne tu, ndio waliofariki dunia sawa na watoto wawili kwa kila walipokuwa watoto 100,000.

Mary Ngonyani ambaye ni Mratibu wa kitengo cha huduma ya afya, uzazi na mtoto wilayani humo alisema pia kwa ujumla vifo vya watoto hao husababishwa hasa na wale wanaozaliwa kabla ya kutimiza umri wa kuzaliwa (njiti) na magonjwa mengine ya akina mama pale anapokuwa mjamzito.

Alifafanua kuwa upungufu wa vifo hivyo unatokana na jitihada zinazofanywa na wataalamu wa kitengo hicho kuendelea kupambana na kudhibiti tatizo hilo ili lisiweze kuendelea kuwepo au kujitokeza, kwa kufikisha elimu husika katika jamii hususan kwa akina mama wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya.

WATU WENYE UKIMWI MBINGA WATAKIWA KUZINGATIA DAWA

Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

MRATIBU wa kudhibiti na kuenea kwa ugonjwa wa Ukimwi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Francis Kapinga amewataka watu ambao wamepima afya zao na kubainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo wilayani humo kuzingatia ratiba ya kunywa dawa kwa wakati na sio kuzembea, hali ambayo amesema kuwa endapo wasipozingatia hilo wanaweza kuhatarisha usalama wa afya zao.

Aidha Kapinga amefafanua kuwa wengi wao hivi sasa wanaoishi na virusi vya ugonjwa huo wamekuwa watoro wa kuzingatia ratiba ya kunywa dawa kwa wakati na kwamba, jitihada zinaendelea kufanyika kuwatafuta pale walipo ili waweze kuendelea kunywa dawa hizo.

Kadhalika alibainisha kuwa upimaji na ushauri uliotolewa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu, jumla ya watu 51,639 wakiwemo wanawake 26,421 na wanaume 25,218 walijitokeza kupima afya zao.

JAFFO: DOKTA MAGUFULI AMEVUNJA REKODI ULIPAJI MADENI NDANI YA NCHI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.
Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa tokea nchi hii ipate Uhuru, Rais wa awanu ya tano Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amekuwa wa kwanza kuvunja rekodi katika ulipaji wa madeni mbalimbali ndani ya nchi, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 970 ameweza kulipa kwa wakandarasi  na wadeni wengine ambao walikuwa wakiidai serikali.

Suleiman Jaffo ambaye ni Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) alisema hayo jana alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma huku akiongeza kuwa, nchi hii ilifikia mahali pabaya kwa sababu ya madeni hayo na watu wachache kuwa wabinafsi wakitaka kujilimbikizia mali nyingi.

Alifafanua kuwa ufanisi huo wa ulipaji wa madeni umetokana na serikali kuwa imara katika ukusanyaji wa mapato yake, ambapo imekuwa ikikusanya shilingi bilioni 800 kila mwezi.

Hivyo aliwataka watendaji wa serikali ambao walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea muda wao umepita na wanapaswa kubadilika ili waweze kuendana na kasi ya awamu ya tano, ambayo ina malengo ya kusimamia na kutekeleza ipasavyo maendeleo ya wananchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

WAGANGA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA KIKAANGONI WAZIRI ASHANGAZWA KUPATA TAARIFA HOSPITALI HAZINA DAWA

Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

NAIBU Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jaffo amesema kuwa ameshangazwa kupata taarifa kwamba baadhi ya hospitali za serikali hapa nchini hazina dawa, wakati serikali imekuwa ikituma fedha kila mwezi kwa ajili ya kununua vifaa tiba na madawa ya kutibu wagonjwa.

Suleiman Jaffo.
Aidha kufuatia hali hiyo ametoa onyo kali kwa Waganga wakuu wa mikoa na wilaya kwamba endapo atasikia au kupata taarifa kuwa hospitali hizo hazina madawa, wajiandae kuwajibishwa na kutolea maelezo fedha hizo za kununulia dawa baada ya kuzipokea wamezitumia kwa shughuli gani.

“Sitegemei kusikia hata dawa aina ya Panadol hakuna, serikali imekuwa ikileta fedha kwenye mahospitali yetu kupitia mfuko wa Busket fund lakini taarifa nilizonazo kumekuwa na mchezo mchafu wa kutumia fedha za mfuko huu, watu kulipana posho wakati wananchi wanateseka”, alisema Jaffo.

WAHASIBU HALMASHAURI ZA WILAYA WATAKIWA KUACHA KUWA MIUNGU WATU

Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

AGIZO limetolewa kwa Watunza fedha wote waliopo katika Halmashauri za wilaya hapa nchini, kutimiza wajibu wao wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kazi za serikali na kuacha kuwa miungu watu.

Vilevile wametakiwa kuvunja madaraja na minyororo ya ubinafsi, badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia taratibu husika na maadili ya utumishi wa umma.

Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jaffo alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, katika ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.

Waziri huyo alisema kuwa katika halmashauri kumekuwa na tabia kwa baadhi ya Wahasibu kutoa taarifa za uongo kwamba, mfumo wa ulipaji malipo (Epicor) pale malipo husika yanapotakiwa kufanyika umekuwa ukisumbua jambo ambalo sio la kweli hivyo wanapaswa kubadilika.

Wednesday, December 21, 2016

MANISPAA SONGEA YABAINI KAYA HEWA 2,692 AMBAZO HAZIKUWA NA SIFA YA KUENDELEA KUPEWA RUZUKU YA TASAF

Baadhi ya Wanufaika wa ruzuku ya kaya maskini wakiwa katika ofisi za serikali ya kijiji mtaa wa Oysterbay kata ya Msamala Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wakisubiri kupewa ruzuku na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). 
Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao unahudumia kaya maskini katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, umeengua kaya hewa 2,692 ambazo zimebainika kwamba hazikuwa na sifa ya kuendelea kupewa ruzuku ya kuhudumia kaya maskini.

Kaya zilizoenguliwa ni kati ya 7,695 zilizokuwa zinanufaika na ruzuku hiyo ambapo hivi sasa baada ya uhakiki kufanyika, kaya zenye sifa ya kupata fedha kutoka kwenye mfuko huo zimebakia 5,003.

Albano Midelo ambaye ni Ofisa habari wa Manispaa hiyo alibainisha hayo jana alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu na kueleza kuwa tayari shilingi milioni 277 zimetolewa kwa kaya maskini 5,003 zilizopo katika mitaa 53 ya Manispaa ya Songea ambayo ipo kwenye mpango wa kupewa ruzuku.

WATU 133 WAFARIKI DUNIA KWA UGONJWA WA MALARIA SONGEA

Na Kassian Nyandindi,      
Songea.

IMEELEZWA kuwa jumla ya watu 133 waliokuwa wakiishi katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamefariki dunia katika kipindi cha mwaka 2015 baada ya kuugua ugonjwa hatari wa malaria.

Aidha katika mwaka huo Manispaa hiyo ilikuwa na wagonjwa 28,624 waliougua ugonjwa huo na kutibiwa katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za afya, ambao ni sawa na asilimia 16.9 ya wagonjwa wote 169,266.

Ofisa habari wa Manispaa ya Songea, Albano Midelo alisema hayo jana alipokuwa akihojiwa na mwandishi wa habari hizi na kuongeza kuwa wagonjwa waliougua na kulazwa katika kipindi hicho walikuwa 8,084 sawa na asilimia 28.8 ya wagonjwa wote 30,129 waliolazwa na kuruhusiwa kurudi makwao.

RADI YAKATISHA MAISHA YA MTOTO CREDO WAWILI WANUSURIKA

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

MTOTO Credo Adrian Ndomba (4) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Miembeni katika kitongoji cha Majembe kata ya Kitanda Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, amefariki dunia papo hapo baada ya kupigwa na radi na kumuunguza mwili wake akiwa amelala.

Zubery Mwombeji.
Aidha katika tukio hilo ambalo lilitokea nyakati za usiku mtoto mwenzake, Esther Ndomba pamoja na mama yao mzazi, Yustina Ndunguru (30) nao walinusurika kupoteza maisha baada ya radi hiyo iliyoambatana na mvua kuunguza nyumba waliyokuwa wamelala.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alimweleza mwandishi wetu kuwa tukio hilo lilitokea Disemba 18 mwaka huu majira ya usiku ambapo Esther na Yustina, walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitali ya halmashauri ya mji wa Mbinga iliyopo mjini hapa kwa ajili ya matibabu zaidi.  

Tuesday, December 20, 2016

HALMASHAURI MANISPAA YA SONGEA KUTUMIA MILIONI 488 UJENZI MRADI WA MAJI RUHUWIKO KANISANI



Na Kassian Nyandindi,            
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, inatarajia kutumia shilingi milioni 488 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji katika mtaa wa Ruhuwiko Kanisani, kwa lengo la kuwaondolea kero upatikanaji wa maji wakazi wanaoishi katika mtaa huo.

Aidha tayari Manispaa hiyo imeingia mkataba na kampuni ya Giraf Investment na kwamba hadi sasa mradi huo, ambao umefadhiliwa na benki ya dunia ujenzi wake umefikia asilimia 95. 

Albano Midelo ambaye ni Ofisa habari wa Manispaa hiyo alisema hayo alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari mjini hapa, huku akiongeza kuwa ni asilimia ndogo imebakia katika kukamilisha ujenzi wake ili wananchi hao waweze kukabidhiwa mradi na kuanza kuutumia.

MWANAFUNZI CHUO KIKUU SONGEA AKUTWA AKIWA AMEFARIKI DUNIA BAADA YA KUJINYONGA MSITUNI

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Yakobo (AJUCO) tawi la Songea mkoani Ruvuma, Henry Mwelang’ombe (24) ambaye ni wa mwaka kwanza amekutwa akiwa amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba aina ya manila, kwenye msitu uliopo nyuma ya shule ya sekondari ya wasichana Songea iliyopo mjini hapa.

Habari zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa mwili wa mwanafunzi huyo ulikutwa na mwalimu mmoja anayefundisha katika sekondari hiyo ya wasichana ambaye hakutaka kumtaja jina lake.

Mwombeji alisema kuwa mwalimu huyo alikuwa akielekea shambani kwake majira ya asubuhi ambapo ghafla aliukuta mwili wa marahemu huyo ukiwa unaning’inia kwenye mti katika msitu huo Disemba 18 mwaka huu majira hayo ya asubuhi.

Kamanda huyo wa Polisi hapa mkoani Ruvuma alifafanua kuwa mwalimu huyo baada ya kuona tukio hilo ambalo lilimshitua, alichukua jukumu la kutoa taarifa kwa majirani wanaozunguka eneo hilo ambapo baadaye walilazimika kwenda kutoa taarifa kituo kikuu cha Polisi Songea mjini na askari walikwenda huko, kwenye eneo la tukio wakiwa wameongozana na daktari ambaye alithibitisha kuwa Henry amefariki dunia kutokana na kujinyonga huko.

Sunday, December 18, 2016

MWEKA HAZINA NA WENZAKE SONGEA WASIMAMISHWA KAZI KWA TUHUMA YA KUBADILI MATUMIZI YA FEDHA BILA KUPEWA IDHINI NA KAMATI HUSIKA



Julius Konala,     
Songea.

BARAZA maalum la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, limewasimamisha kazi kwa muda usiojulikana watumishi wake watatu wa halmashauri hiyo kwa ajili ya kupisha uchunguzi, dhidi ya tuhuma zinazowakabili za kubadili matumizi ya fedha bila kupewa idhini na kamati ya fedha, uchumi na mipango.

Watumishi hao wamesimamishwa juzi katika kikao maalum cha baraza hilo kilichoketi kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo mjini hapa, chini ya Mwenyekiti wake Rajab Mtiula na kuhudhuriwa na sekretarieti ya mkoa huo pamoja na wakuu mbalimbali wa idara wa wilaya hiyo.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Rajab Mtiula aliwataja watumishi waliosimamishwa kazi kuwa ni Wenisalia Swai ambaye ni Ofisa maendeleo ya jamii, Mwajuma Sekelela mweka hazina na Amina Njogela Ofisa ugavi na manunuzi wote wa halmashauri ya wilaya ya Songea.

WASHAURIWA KUTUMIA NISHATI YA MAKAA YA MAWE

Na Kassian Nyandindi,            
Mbinga.

JAMII hapa nchini imeshauriwa kuacha kukata miti hovyo na kuitumia kwa ajili ya shughuli za kibinadamu, badala yake wanapaswa kutumia nishati ya makaa ya mawe kwa ajili ya shughuli zao za kila siku, hatua ambayo itasaidia kutunza mazingira na kuepukana na athari kubwa ya uharibifu wa mazingira kunakosababishwa na matumizi ya kuni.

Kufuatia hali hiyo serikali kupitia wataalamu wake imeombwa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi, juu ya madhara ya ukataji miti na matumizi ya kuni kwa ajili ya kupikia au shughuli nyingine za kibinadamu.
Makaa ya mawe.

Ushauri huo ulitolewa juzi na Leah Kayombo ambaye ni Meneja wa shirika lisilokuwa la kiserikali, Mbalawala Women Group Organisation lililopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  waliotembelea kuona namna shirika hilo, lilivyofanikiwa katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi na uchimbaji wa makaa ya mawe kijijini humo.

NOVATUS LUAMBANO ANATAFUTWA NA JESHI LA POLISI



Na Gideon Mwakanosya,         
Songea.

Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linamsaka Novatus Luambano (32) mkazi wa kijiji cha Mahanje Madaba wilayani songea, ambaye ni dereva  wa basi dogo ambalo liliacha njia kisha kupinduka na kusababisha kifo cha abiria mmoja na wengine  27 kujeruhiwa vibaya.

Zubery Mwombeji Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji amewaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea Disemba 15 mwaka huu, majira ya mchana huko katika kijiji cha Hanga Ngadinda wilaya ya Songea vijijini ambapo gari lenye namba za usajili T 435 BHT aina ya Toyota Coster, lililokuwa likiendeshwa na Novatus lilipinduka kutokana na kuwa katika mwendo kasi kisha dereva huyo kutokomea kusikojulikana.

Alimtaja aliyefariki dunia papo hapo katika ajali hiyo kuwa ni Witness Tembe (11) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Matarawe iliyopo katika Manispaa ya Songea mkoani hapa.

MAMA ASHIKILIWA NA POLISI KWA KUMUUA MWANAYE



Na Gideon Mwakanosya,         
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia, Eva Kapinga (20) ambaye ni mkazi wa wa kata ya Mateka Manispaa ya Songea mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mtoto wake Catherine Kapinga mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu, kisha mwanamke huyo kuamua kujichoma na kisu tumboni kwa lengo la kutaka kujiua. 

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Disemba Mosi mwaka huu majira ya jioni katika eneo la mtaa wa Mateka C ambapo Eva baada ya kujichoma kisi hicho amejisababishia jeraha kubwa ambalo limepelekea kulazwa hospitalini.

Mwombeji alifafanua kuwa siku ya tukio hilo Catherine aliuwawa na mama huyo ambaye pia ni mjamzito, na kwamba chanzo cha mauaji hayo bado hakijulikani licha ya kwamba taarifa za awali zinaeleza kuwa Eva alikuwa na malumbano kati yake na mama yake mzazi Sofia Mayunga ambaye alikuwa akimuuliza kwa nini ameamua kushika mimba wakati anajua kuwa ana mtoto mdogo wa umri wa mwaka mmoja, jambo ambalo limfanya kupandwa hasira na kuamua kufanya kitendo hicho.

Friday, December 16, 2016

AGIZO LA WAZIRI KUWASIMAMISHA KAZI WATENDAJI TASAF MBINGA LATEKELEZWA

Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amesema kwamba amesikitishwa na kitendo cha maofisa Washauri na Wafuatiliaji Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani humo ambao walipewa dhamana ya kusimamia zoezi la ugawaji wa fedha kwa kaya maskini, kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na kusababisha fedha hizo kulipwa watu ambao hawakuwa na sifa.  

Cosmas Nshenye.
Aidha alifafanua kuwa kufuatia hali hiyo serikali wilayani hapa imechukua hatua ya kumsimamisha kazi Mratibu wa mfuko huo, Ahsante Luambano ambaye alisema kuwa ameshindwa kuwajibika kwa kusimamia ipasavyo zoezi la uibuaji wa kaya hizo na kusababisha wengi wao walioingizwa katika mpango wa kulipwa fedha hizo kuwa ni viongozi wa serikali ngazi ya vijiji na vitongoji.

Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, Nshenye alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, huku akiongeza kuwa barua ya Waziri mwenye dhamana ya Desemba 5 mwaka huu ambayo waliipata imetoa maagizo ya kuwasimamisha kazi waliohusika katika kuvuruga utekelezaji wa mpango huo kwa muda usiojulikana hadi uchunguzi utakapokamilika na wahusika kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Wednesday, December 14, 2016

WANANCHI MBINGA KUENDELEA KUNUFAIKA NA MPANGO WA UPIMAJI ARDHI


Mkurugenzi mtendaji Halmashauri wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Gombo Samandito akizungumza na wakazi wa tarafa ya Mbuji juzi kuhusiana na mpango wa halmashauri hiyo kuanza mchakato wa kuanzishwa kwa miji midogo sambamba na  uendelezaji wa miji hiyo, ambapo baadhi ya maeneo yatachukuliwa na serikali kwa ajili ya kupisha huduma mbalimbali za kijamii kama vile ujenzi wa shule, zahanati, miundo mbinu ya maji na barabara.

Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imejiwekea mkakati wa kupanga na kupima maeneo yote ya bonde la Hagati na tarafa ya Mbuji yaliyopo wilayani humo, kutokana na wakazi wanaoishi katika maeneo hayo kuendeleza maeneo yao kwa kujenga makazi holela.

Aidha imeelezwa kuwa sababu nyingine inayoifanya halmashauri hiyo kutaka kutekeleza mpango huo ni ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaoishi katika maeneo hayo, huku ardhi iliyopo haitoshelezi kwa matumizi ya binadamu na asilimia kubwa wananchi wake wamekuwa wakitumia maeneo yao kwa shughuli za kilimo cha zao la kahawa.

Vilevile imefafanuliwa kuwa maeneo ya bonde hilo la Hagati na tarafa ya Mbuji hayana mgawanyiko rasmi wa matumizi ya ardhi hivyo halmashauri hiyo ya wilaya ya Mbinga, inakusudia kupanga na kupima maeneo ya wananchi bila kuathiri hali halisi ya mazingira yaliyopo sasa kwa kuzingatia kanuni na taratibu za sheria ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999 pamoja na sheria ya mipango miji namba 7 ya mwaka 2007.

Wednesday, December 7, 2016

SERIKALI YATUMIA MILIONI 55 KUENDELEZA MIRADI YA MAJI SAFI NA USAFI WA MAZINGIRA SONGEA

Na Mwandishi wetu,        
Songea.

KATIKA kuendeleza miradi ya maji safi na usafi wa mazingira, serikali hapa nchini imetoa zaidi ya shilingi milioni 55 kwa halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kwa ajili ya kuendeleza miradi hiyo kwa manufaa ya wananchi wake.

Aidha imefafanuliwa kuwa fedha hizo zitatumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji na usafi wa mazingira kwa lengo la kuzijengea uwezo Jumuiya za Watumiaji Maji (COWSO) na usimamizi wa maji.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa fedha hizo tayari zimetumika katika suala la uchangiaji huduma ya matumizi ya maji katika mitaa ya Mahilo, Muhombezi, Ruhuwiko Kanisani na Chandarua.

NAMTUMBO WAANZA MCHAKATO WA KUANZISHA KITUO CHA KURUSHA MATANGAZO

Na Kassian Nyandindi,         
Namtumbo.

HALMASHAURI ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imeanza mchakato wake wa kuanzisha kituo cha kurusha matangazo (Redio ya jamii) ambayo itakuwa ikiyarusha ndani ya wilaya hiyo, kwa lengo la kuhamasisha maendeleo mbalimbali ya wananchi.

Yeremias Ngerangera ambaye ni Ofisa habari wa wilaya hiyo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa mchakato wa kuanzisha Redio hiyo ya jamii, unaendelea vizuri ambapo tayari kamati ya kusimamia suala hilo imeundwa na kuanza kazi yake.

Alitaja idara zilizopo kwenye kamati hiyo ni idara ya mipango, utawala, maendeleo ya jamii, afya, mazingira pamoja na kitengo cha sheria na usalama ambazo zinatoka katika halmashauri ya wilaya ya Namtumbo.

DOKTA KALEMANI AZITAKA TAASISI ZA KIFEDHA KUSHIRIKIANA NA WAWEKEZAJI BINAFSI WANAOZALISHA UMEME

Na Kassian Nyandindi,                
Mbinga.

NAIBU Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani amezitaka taasisi za kifedha hapa nchini kushirikiana na wawekezaji binafsi ambao wanazalisha umeme wa nguvu ya maji, katika kuwapatia mikopo yenye riba nafuu ili waweze kuendesha shughuli ya uzalishaji wa nishati hiyo kwa ufanisi zaidi.

Dkt. Medard Kalemani.
Aidha ameeleza kuwa serikali kwa kushirikiana pia na Wakala wa umeme vijijini (REA) wameweka mikakati ya kuhakikisha kwamba umeme utapelekwa katika maeneo yote ya vijijini na kwenye taasisi za serikali, kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma hiyo katika maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme.

Hayo yalisemwa na Dkt. Kalemani juzi alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakati alipotembelea kituo cha kuzalisha umeme wa nguvu ya maji unaoendeshwa na kampuni ya Andoya Hydro Electric Power(AHEPO) katika kata ya Mbangamao wilayani humo.

Thursday, December 1, 2016

MADIWANI SONGEA WAPITISHA OMBI LA KUKIPANDISHA HADHI KITUO CHA AFYA MJIMWEMA KUWA HOSPITALI

Ni moja kati ya sehemu ya jengo la kituo cha afya Mjimwema Songea.
Na Gideon Mwakanosya,       
Songea.

BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea  mkoani Ruvuma limeridhia na kupitisha ombi la kukipandisha hadhi kituo cha afya Mjimwema na kuwa hospitali ya halmashauri ya Manispaa hiyo.

Ombi hilo liliwasilishwa katika baraza hilo ili hatua nyingine ngazi za juu ziweze kuendelea na kuthibitishwa kuwa hospitali kamili.

Aidha kupandishwa huko na kuwa hospitali ni agizo lililotolewa Januari 11 mwaka huu na Waziri wa afya, ustawi wa jamii, jinsia, watoto na wazee Ummy Mwalimu alipotembelea kituo hicho.

Waziri Mwalimu aliagiza hayo kwa kuutaka uongozi husika wa Manispaa hiyo kuwasilisha katika Wizara yake ombi hilo ili liweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu husika na hatimaye kufikia maamuzi ya mwisho ya kituo cha afya Mjimwema kuwa hospitali ya wilaya katika Manispaa hiyo.

MANISPAA YA SONGEA YATEKETEZA BIDHAA FEKI ZENYE VIAMBATA VYA SUMU YENYE MADHARA KWA BINADAMU

Na Kassian Nyandindi,         
Songea.

KATIKA kuhakikisha kwamba udhibiti wa vyakula na dawa unakuwa endelevu katika Manispaa ya Songea mkoa wa Ruvuma, idara ya afya halmashauri ya Manispaa hiyo imefanya ukaguzi wa kushitukiza na kuweza kukamata vyakula vibovu na vipodozi ambavyo vina sumu vyenye thamani ya shilingi 500,000.

Aidha ukaguzi huo wa vyakula ambavyo vimekamatwa na muda wake wa matumizi umepita, viliweza kupatikana vya shilingi 300,000 huku chumvi isiyokuwa na madini joto ikiwa ni ya shilingi 80,000 na vipodozi vyenye viambata vya sumu vikiwa vyenye thamani ya shilingi 120,000.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowafikia waandishi wa habari na kuthibitishwa na Ofisa habari wa Manispaa ya Songea, Albano Midelo ilieleza kuwa watuhumiwa waliokamatwa wakihusika kuuza bidhaa hizo wamechukuliwa hatua ya kulipishwa faini ya shilingi 122,500 kila mmoja ikiwemo na gharama ya uteketezaji.

Monday, November 28, 2016

CHAWATA MBINGA YATOA MSAADA WA BAISKELI MAALUM KWA MWANAFUNZI WA SEKONDARI RUANDA

Damian Kapinga akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kata ya Ruanda mara baada ya kukabidhiwa baiskeli maalum ya kutembelea.
Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

CHAMA Cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma, kimetoa msaada wa baiskeli maalum ya kutembelea mlemavu Damian Kapinga (22) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili, shule ya sekondari Ruanda wilayani humo yenye thamani ya shilingi milioni moja.

Akikabidhi msaada huo shuleni hapo mbele ya Mkuu wa shule Stephano Ndomba na Diwani wa viti maalum tarafa ya Namswea Immaculatha Mapunda, Mwenyekiti wa chama hicho wilayani hapa Martin Mbawala alisema kuwa baiskeli hiyo ya kutembelea mtoto huyo imepatikana kutokana na jitihada zilizofanywa na chama, kutoka kwa wasamaria wema.

Mbawala alisema kuwa chama kimefanya jitihada ya kutafuta baiskeli hiyo kutokana na taabu alizokuwa akizipata mtoto huyo kutambaa kwa mikono na magoti wakati wa kwenda shule kuhudhuria masomo yake, hivyo kiliona kuna kila sababu ya kumtafutia chombo hicho ili kumrahisishia asiendelee kupata adha hiyo.

“Nakukabidhi baiskeli hii iweze kukusaidia na kukurahisishia uweze kutembea na kuhudhuria masomo yako vizuri, nawaomba viongozi wa kata hii ya Ruanda muendelee kumtunza mtoto huyu kama walivyo wenzake ambao hawana matatizo ya ulemavu”, alisisitiza Mbawala.

SERIKALI YAOMBWA KUINUSURU HOSPITALI YA MISHENI MBESA TUNDURU

Na Kassian Nyandindi,        
Tunduru.

HOSPITALI kongwe ya Misheni Mbesa ambayo inamilikiwa na Kanisa la Bibilia Tanzania wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, ipo katika hali mbaya yenye kuhatarisha kufungwa wakati wowote kuanzia sasa kutokana na Madaktari kutoka nje ya nchi ambao walikuwa ni tegemeo kubwa katika kuendesha hospitali hiyo kuanza kufunga virago kurejea makwao, baada ya mikataba yao ya kufanya kazi kwisha.

Hospitali ya Misheni Mbesa.
Katibu tawala wa hospitali hiyo, Dkt. John Mwaya alisema hayo wakati alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya hospitali yake kwa Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera ambaye alifanya ziara ya kutembelea hospitali hiyo kwa lengo la kujionea maendeleo mbalimbali.

Dkt. Mwaya alibainisha kuwa changamoto kubwa inayotishia kufa kwa hospitali yake ni kuwepo kwa upungufu wa Madaktari wenye taaluma na wauguzi walio somea fani hiyo ili kuweza kutosheleza ikama husika.

Sunday, November 27, 2016

MBUNGE WA TUNDURU KUSINI AMWAGA NEEMA KWA WANANCHI WAKE


Na Julius Konala,     
Tunduru.

MBUNGE wa Jimbo la Tunduru kusini mkoani Ruvuma, Daimu Mpakate ametoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani zaidi ya shilingi milioni 100 ili viweze kutumiwa na wananchi wake jimboni humo, kwa ajili ya kuwaletea maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Daimu Mpakate.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo alisema kuwa miongoni mwa misaada iliyotolewa ni mashine nane za kusaga nafaka zenye thamani ya shilingi milioni 16, vitabu vya kiada na ziada kwa shule za sekondari vyenye thamani ya shilingi milioni 32, mashine za kushonea nguo (vyerehani) nane vyenye thamani ya shilingi milioni 2, pamoja na fedha taslimu shilingi milioni 2 kwa ajili ya kugharimia kushona sare za shule kwa wanafunzi 120 watakaochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwakani.

Mpakate alitoa msaada huo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya serikali ya kijiji cha Mbesa wilayani humo ambapo vifaa hivyo vilitolewa kwa matumizi ya jamii kupitia shule nane za sekondari ambazo ni Nalasi, Mbesa, Mchoteka, Malumba, Ligoma, Lukumbule, Namasakata na Semeni.

HALMASHAURI MANISPAA SONGEA YAVUKA LENGO LA UTOAJI CHANJO


Na Gideon Mwakanosya,          
Songea.

HALMASHAURI Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imevuka lengo la utoaji chanjo kwa kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano na kufikia asilimia 217.5 katika kipindi cha kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu.

Albano Midelo ambaye ni Ofisa habari wa Manispaa hiyo alimweleza mwandishi wetu kuwa katika kutekeleza zoezi hilo la chanjo ya kitaifa kwa kuhakikisha kila mtoto anafikiwa, limeweza kuleta ufanisi mkubwa kwa kukidhi vigezo vya utoaji chanjo ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na yale yanayozuiliwa kwa chanjo.

“Manispaa yetu imevuka lengo hili kutokana na watoto na akina mama wajawazito kutoka nje ya halmashauri, kupata huduma katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya”, alisema.

Monday, November 21, 2016

NFRA SONGEA YAONGEZA BEI YA KUNUNUA MAHINDI YA MKULIMA

Na Kassian Nyandindi,          
Songea.

SERIKALI kupitia Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea mkoani Ruvuma, imelazimika kuongeza bei ya kununua mahindi ya wakulima kufuatia kuwepo kwa ushindani mkubwa kutokana na wanunuzi binafsi wengi wao mkoani humo, kununua mahindi kwa bei kubwa kutoka kwa wakulima wanaozalisha zao hilo.

Aidha kufuatia kuwepo kwa ushindani huo, NFRA imeongeza bei ambapo awali walikuwa wakinunua kwa shilingi 350 kwa kilo na kwamba kuanzia Novemba 7 mwaka huu wananunua mahindi kwa shilingi 580 kwa kilo maeneo ya vijijini na shilingi 600 kwa wale wanaoleta katika kituo kikuu cha Ruhuwiko kilichopo mjini hapa.

Kaimu Meneja wa Wakala huyo Kanda ya Songea, Majuto Chabruma alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya maendeleo ya zoezi la ununuzi wa mahindi linavyoendelea katika vituo mbalimbali vilivyotengwa katika wilaya zote za mkoa wa Ruvuma.

HALMASHAURI YATENGA MAMILIONI YA FEDHA KUBORESHA ZAO LA KOROSHO NAMTUMBO

Na Muhidin Amri,            
Namtumbo.

KATIKA kuhakikisha kwamba zao la korosho linaboreshwa na kuwa endelevu, halmashauri wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imetenga zaidi ya shilingi milioni 10 kwa ajili ya kufufua na kuendeleza zao hilo katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Kati ya fedha hizo shilingi milioni 5 zitatumika kununua miche ya zao hilo na shilingi milioni 5 zinazobakia zitatumika kwa ajili ya kununua mbegu za korosho kutoka chuo cha utafiti wa kilimo cha Naliendele kilichopo mkoani Mtwara.

Zao la korosho.
Afisa kilimo umwagiliaji na ushirika wilayani Namtumbo, Ally Lugendo aliyataja maeneo yatakayonufaika na mpango huo ni pamoja na kata ya Magazini, Lusewa, Msisima, Ligera, Lisimonji, Limamu, Likuyu, Mchomoro na Rwinga ambapo mbegu na miche hiyo itasambazwa katika maeneo hayo ambayo yana hali nzuri ya hewa inayostawi vizuri korosho.

Alisema kuwa halmashauri imefikia uamuzi wa kufufua zao la korosho baada ya kuwepo kwa soko la uhakika katika kipindi cha msimu wa mwaka huu ambapo bei imepanda kutoka shilingi 1,500 kwa kilo hadi kufikia shilingi 4,000 jambo ambalo halmashauri inaamini kwamba kama wakulima wataamua kuwekeza katika kilimo hicho wataweza kuondokana na umaskini katika familia zao.

Sunday, November 20, 2016

WAJASIRIAMALI SONGEA WANUFAIKA NA MIKOPO WASISITIZWA KUITUMIA KWA MALENGO YALIYOKUSUDIWA

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

WAJASIRIAMALI waliopo katika vikundi vya wanawake na vijana halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamepewa shilingi milioni 20 na halmashauri hiyo ili waweze kuendeleza vikundi vyao kwa kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo na hatimaye waweze kuondokana na umaskini.

Fedha hizo walizopewa ni mkopo ambao unalenga kusaidia vikundi 42 vya wajasiariamali hao na sehemu ya mkopo huo watapaswa kurejesha baada ya miezi 12 ambapo kila kikundi kimepewa kuanzia shilingi 800,000 huku vingine vikipewa shilingi 600,000.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Ofisa habari wa Manispaa hiyo Albano Midelo alisema kwamba vikundi vilivyopewa fedha hizo vimetoka katika kata 21 zilizopo katika Manispaa ya Songea.

Tuesday, November 15, 2016

WALIOKAMATWA WAKITOROSHA KAHAWA MBINGA KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Na Kassian Nyandindi,                   
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amesema kwamba katika tuhuma ambazo zimefikishwa Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, juu ya suala la utoroshaji wa zao la kahawa ni lazima shauri hilo lifikishwe Mahakamani ili hatua za kisheria ziweze kuchukua mkondo wake.

Cosmas Nshenye.
Aidha alisema kuwa ameonesha kuchukizwa kwake na tabia kwa baadhi ya Watendaji wa serikali kushindwa kusimamia kikamilifu sheria zilizopo juu ya namna ya kudhibiti hali hiyo, hatua ambayo huchangia kwa namna moja au nyingine wafanyabiashara wajanja kutumia mwanya huo kuvunja sheria zilizowekwa na serikali wakiwa na lengo la kukwepa kulipa kodi au ushuru halali kwa mujibu wa sheria.

Nshenye alisema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kufuatia kukamatwa kwa mfanyabiashara, Khatwib Rajabu mkazi wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera akidaiwa kushirikiana na wenzake kufanya tukio la utoroshwaji wa kahawa wilayani hapa, bila kufuata taratibu na sheria husika zilizowekwa na serikali.

“Hapa kesi lazima iwepo na kama sio kwa mfanyabiashara aliyehusika kutorosha kahawa basi itabaki kwa watumishi wa serikali waliohusika kutoa kibali hiki, huku wakijiua kwamba wanafanya makosa”, alisisitiza Nshenye.

Saturday, November 12, 2016

HATIMAYE MWILI WA SPIKA MSTAAFU SAMUEL SITTA WAZIKWA URAMBO TABORA

HATIMAYE Novemba 12 mwaka huu yamefanyika mazishi ya Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel John Sitta ambaye alifariki dunia Novemba 7 mwaka huu 2016 katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani.


Mazishi hayo yamefanyika Urambo Tabora, kwenye eneo la makaburi ya ukoo wa Sitta ambayo yapo takribani kilometa mbili kutoka nyumbani kwake marehemu Sitta. (Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi….Amen)

CHADEMA WAFUKUZANA UANACHAMA SONGEA FUIME ADAIWA KUKALIA KUTI KAVU

Joseph Fuime akiwa katika majukwaa ya mikutano ya siasa mjini Songea iliyofanyika hivi karibuni.
Na Gideon Mwakanosya,           
Songea.

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kimemvua uanachama Joseph Fuime akidaiwa kufanya makosa mbalimbali ikiwemo kukihujumu chama hicho wakati alipokuwa mgombea ubunge kupitia tiketi ya CHADEMA jimbo la Songea mjini, katika uchaguzi mkuu uliopita Oktoba 25 mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Ofisini kwake, Katibu wa CHADEMA wilaya ya Songea, Olais Ng`ohison alisema kuwa Fuime amefutwa kwenye orodha ya kuwa mwanachama wa chama hicho, tangu Octoba 23 mwaka huu na kwamba  hivi sasa sio mwanachama tena wa chama hicho.

Alisema kuwa chama hicho kimelazimika kutoa taarifa kupitia vyombo vya habari kuwajuza wananchi, wadau, wakereketwa pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali baada ya kubaini kwamba watu wengi walikuwa hawafahamu kuondolewa na kufutwa uanachama kwa Fuime.

Friday, November 11, 2016

WAZIRI MKUU AONGOZA BUNGENI KUUAGA MWILI WA MAREHEMU SAMUEL SITTA

Na Waandishi wetu, 
Dodoma.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa leo ameongoza mamia ya wabunge, viongozi wa kitaifa na watumishi wa Ofisi ya Bunge kuuaga mwili wa Spika Mstaafu, Samwel Sitta.

Sitta alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 7 mwaka huu katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani.

Akizungumza wakati wa kuuaga mwili huo Bungeni mjini Dodoma leo Novemba 11 mwaka huu, Waziri Mkuu Majaliwa ametoa pole kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, mke wa marehemu Sitta, Margareth Sitta, mama wa marehemu Hajat Zuena Fundikila na familia ya marehemu na wabunge wote.

“Nitumie fursa hii pia kukupa pole Mheshimiwa Spika kwa pigo ambalo Bunge lako tukufu imelipata kwa kumpoteza mmoja wa viongozi mahiri wa Bunge hili katika historia ya nchi yetu,

“Msiba uliotupata wa Spika huyu mstaafu wa Bunge la tisa (2005-2010) na Mbunge mstaafu wa Jimbo la Urambo mkoani Tabora ni mzito”, alisema Majaliwa.

Alisema kuwa Sitta alikuwa ni mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.

“Serikali imepokea taarifa za msiba huu kwa mshtuko mkubwa, historia ya mzee Sitta ni pana sana, tunatambua utumishi wake uliotukuka katika nyadhifa mbalimbali alizozitumikia tutamkumbuka kwa utumishi wake,” alisema.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa Watanzania tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu kila mtu kwa imani yake ili tuweze kufikia japo mema machache aliyoyatenda katika enzi za uhai wake.

Enzi za uhai wake, Marehemu Sitta alibahatika kufanya kazi na marais wa awamu ya nne zilizopita tangu ya kwanza ya Hayati Baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akiwa mbunge kwa miaka 30.

Nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni pamoja na Mkuu wa Mikoa ya Iringa na Kilimanjaro, Waziri wa Ujenzi, Waziri anayesimamia Ustawishaji Makao Makuu, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa (wapili kulia) akimfariji mjane wa Spika Mstaafu Mama Margareth Sitta baada ya mwili wa Spika Mstaafu, Marehemu Samuel Sitta kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma Novemba 11, 2016.