Betramu Sanga ambaye ni afisa kilimo (katikati) akiwapa maelekezo juu ya kilimo bora cha zao la mpunga wakulima wa kijiji cha Mabuni kata ya Litumbandyosi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAKULIMA wanaozalisha zao la mpunga katika mradi wa
umwagiliaji Sanga mabuni uliopo kijiji cha Mabuni kata ya Litumbandyosi wilaya
ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba Halmashauri ya wilaya hiyo kufanya jitihada
ya kukamilisha ujenzi wa mfereji wa kuleta maji shambani ili waweze kuzalisha
zao hilo kwa wingi.
Aidha wameeleza kuwa mfereji huo unaoleta maji shambani ambao
una urefu wa mita 5,850 kutoka kwenye banio kuu la umwagiliaji, ambapo
zilizojengwa mpaka sasa ni mita 3,175 na kwamba zilizobakia ni mita 2,625
ambazo bado ujenzi wake haujakamilika na kuweza kuleta maji kwenye mashamba
yaliyopandwa zao hilo.
Silvester Ngonyani ambaye ni Mwenyekiti wa mradi huo, alisema
hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea kwa lengo
la kujionea mafanikio wanayoyapata na changamoto mbalimbali ambazo hukabiliana
nazo wakulima hao.