Na Muhidin Amri,
Songea.
BAADHI ya Wakazi kumi wanaoishi
katika maeneo mbalimbali Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, wamepigwa faini ya
shilingi Milioni moja kwa ujumla wao baada ya kubainika wamekataa kulipa
shilingi 2,000 ambayo inatozwa kila mwezi kwa kila kaya, kwa ajili ya kuchangia
huduma za usafi wa mazingira katika Manispaa hiyo.
Mahakama ya Mwanzo Mfaranyaki iliyopo
mjini hapa, ndiyo iliyowahukumu adhabu hiyo na kwamba Wakazi hao ni wale wa kutoka
katika kata ya Majengo, Misufini, Bombambili na Matarawe.
Philipo Beno ambaye ni Mkuu wa
masuala ya usafi wa mazingira katika Mnispaa ya Songea akizungumza juzi na Waandishi
wa habari, alisema kuwa wameamua kuanza kuwapeleka Mahakamani Wananchi wote
wanaonekana kukaidi kulipa mchango huo, ili iweze kuwa fundisho kwa wengine
wenye tabia kama hiyo na hatimaye waweze kuchangia kwa urahisi bila usumbufu
wowote kwa kufuata taratibu na sheria ndogo zilizowekwa.