Dar es Salaam, Tanzania.
BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limelaani
shambulizi la hivi karibuni lililotekelezwa na watu wasiojulikana dhidi ya
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Tundu Lissu. |
Mbunge huyo aliyejeruhiwa Septemba 7 mwaka huu kwa kupigwa
risasi tano mjini Dodoma, hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya
Aga Khan, Jijini Nairobi nchini Kenya.
Baraza hilo pia limeungana na Watanzania kulaani kwa nguvu
zote matendo yote ya vurugu, mauaji na uvunjifu wa amani nchini.
Tamko la baraza hilo lililosainiwa na Makamu wa Rais wa TEC,
Askofu Beatus Kinyaiya limetolewa baada ya kikao cha kawaida cha baraza
kilichofanyika kwa siku mbili Septemba 9 na 10 Jijini Dar es Salaam.
“Katika Taifa letu sasa tunashuhudia matendo ya mauaji ya
watu wasio na hatia kama ilivyokuwa kule Mkuranga, Rufiji na Kibiti, utekwaji
wa watu na kuteswa, utekaji wa watoto, ulipuaji wa ofisi za watu na hivi
karibuni shambulio la mbunge Lissu,” limesema baraza katika tamko hilo.
Vilevile imeelezwa kuwa vurugu na mashambulizi ya aina yoyote
ile yanalifedhehesha Taifa kwa kuwa matendo hayo ni dhambi, uhalifu na si
utamaduni wa Mtanzania, hivyo vyombo vinavyohusika havina budi kuyakomesha mara
moja ili yasiweze kuendelea kutokea na kuleta madhara kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment