Na Mwandishi wetu,
WAHITIMU wa mafunzo ya awali ya kijeshi Operesheni Tanzania
ya viwanda kwa mujibu wa sheria 2017 waliohitimu mafunzo yao katika kikosi cha
842 Mlale JKT wilayani Songea mkoa wa Ruvuma, wameishukuru serikali kwa kurejesha
mafunzo ya vijana kwa mujibu wa sheria hatua ambayo itawezesha Taifa kuwa na
viongozi wenye maadili, utiifu na watakaoitumikia nchi katika misingi inayofaa.
Katika risala yao iliyosomwa na Yusuph George na Magreth
Masuki vijana hao walisema wakiwa katika mafunzo hayo wamejifunza mambo muhimu
ambayo ni pamoja na kuwasaidia katika uzalishaji mali
pamoja na ukakamavu, nidhamu, uwajibikaji, umoja na ushirikiano, utunzaji muda,
kazi za mikono na malezi.
Aidha wameahidi kuendelea kushirikiana hata baada ya kumaliza
mafunzo yao ili waweze kuwa na maendeleo endelevu miongoni mwao na Taifa kwa
ujumla na kuwataka vijana wenzao wanapomaliza elimu ya kidato cha sita na
kupata nafasi ya kujiunga na JKT kujifunza mambo yanayohusu uzalendo, tamaduni
za Mtanzania, nidhamu na ukakamvu lakini sio kujiunga kwa lengo la kupata cheti
bali uzalendo wa kweli katika nchi yao.
Kwa upande wake Mkuu wa mafunzo hayo Kapteni Hassan Bakari
alisema kuwa mafunzo hayo yalifunguliwa mwezi Juni mwaka huu yakiwa na vijana 1,735
hata hivyo vijana waliofanikiwa kumaliza mafunzo walikuwa 1,710 kufuatia vijana
25 kushindwa kumaliza mafunzo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro.
Alisema kuwa mafunzo hayo yalichukua muda wa miezi mitatu ambapo
wakati wote wa mafunzo vijana hao wamejifunza kwa nadharia na vitendo katika
masomo mbalimbali ya mafunzo ya kijeshi kama mbinu za kivita, ujanja wa porini,
usalama, utambuzi, elimu ya uraia na huduma ya kwanza.
Pia alisema katika mafunzo ya uraia wamejifunza namna ya
kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi kwa kutii sheria bila shuruti, kufanya
kazi kwa bidii, kutetea na kulinda katiba ya nchi na kuhakikisha wanakuwa
mstari wa mbele katika kudumisha amani ya nchi na maendeleo yaliyokusudiwa na
Serikali.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa JKT ambaye pia ni afisa
ustawi wa Jeshi hilo la taifa Kanali Anchilla Kagombola alisema kuwa Jeshi la
kujenga taifa limepewa jukumu la kuwaanda vijana katika kuipenda na kuitetea na
kuilinda nchi yao pamoja na kuwajengea uwezo katika shughuli mbalimbali za
uzalishaji mali.
Alisema serikali itaendelea kuongeza mpango mkakati katika
makambi yake ili JKT iweze kutekeleza adhima yake ya kuwajenga vijana waweze kuwa
sehemu ya jamii itakayowezesha taifa letu kupiga hatua mbele katika uzalishaji
mali na mkakati wa kukuza uchumi wa kufikia nchi ya viwanda.
Alisema kuwa serikali itaendelea kutoa mchango wake wa hali
na mali katika kuboresha mafunzo kwa vijana wote watakaopata nafasi ya kujiunga
na mafunzo kwa mujibu wa sheria na wale wa kujitolea huku akiwataka vijana
waliomaliza mafunzo hayo kwenda kuonesha mfano bora katika jamii badala ya kushiriki
na kujiunga katika makundi ya hovyo yanayoweza kuharibu sifa nzuri ya JKT.
No comments:
Post a Comment