Na Mwandishi wetu,
Songea.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge amewataka
wakulima wanaozalisha zao la mahindi mkoani humo kuacha kukata tamaa kutokana
na ukosefu wa soko la uhakika la kuuza zao hilo.
Aidha Dokta Mahenge alisisitiza kuwa badala yake wanatakiwa kuendelea
na uzalishaji ili kuepuka uwezekano wa kutokea njaa ndani ya mkoa huo na jamii
kukosa chakula.
Vilevile Mkuu huyo wa mkoa amewaomba wafanyabiashara wa ndani
na nje ya mkoa huo kuunga mkono hatua ya serikali, kununua mahindi ya wakulima
ambayo bado yanapatikana kwa bei ndogo ili kuweza kuwanusuru wakulima wasiweze
kupata hasara.
Dokta Mahenge alitoa kauli hiyo jana wakati alipotembelea
kituo cha ununuzi wa mahindi kijiji cha Mgazini kata ya Mgazini halmashauri ya
wilaya ya Songea mkoani hapa.
Alisema kuwa serikali imepanga kununua tani 8,182 ndani ya
mkoa wa Ruvuma, kiasi ambacho kinatajwa kuwa ni kidogo ikilinganishwa na
uzalishaji mkubwa wa mahindi uliofanywa na wakulima wa mkoa huo.
Kadhalika alieleza kuwa serikali imepanga kununua kiasi hicho
cha mahindi kwa ajili ya kuweka akiba ya chakula hasa pale itakapotokea njaa,
hivyo wakulima nao ni lazima wachangamkie fursa ya kutafuta soko la ndani la
kuuza mahindi yao kwa kuwa serikali haitakuwa na uwezo wa kununua mahindi yote
yaliyozalishwa.
Kiwango hicho kinafuatia baada ya Wakala wa Hifadhi ya
Chakula ya Taifa (NFRA) msimu uliopita alishindwa kufikia lengo lake la kununua
mahindi licha ya kupangiwa kununua tani 20,000 ambapo alifanikiwa
kununua tani 10,000 tu ikilinganishwa na msimu wa mwaka 2015 ambapo alinunua
tani 75,000 za mahindi Kanda ya Songea mkoani hapa.
“Lengo la serikali kuanzisha NFRA ni kwa ajili ya kununua
mahindi kwa lengo la kuweka akiba, serikali haifanyi biashara kama baadhi ya
watu wanavyofikiria tunawaomba wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vitakavyosaidia
kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa na wakulima wetu”, alisema.
Pia Dokta Mahenge amemuagiza Meneja wa Wakala wa hifadhi ya
chakula Kanda ya Songea kupunguza mgawo wa mahindi katika vituo vyenye mwitikio
mdogo na kuelekeza nguvu kubwa katika maeneo ambayo kuna mwitiko mkubwa wa
wakulima kupeleka mahindi yao.
“Nakuagiza maeneo ambayo wakulima hawachangamkii fursa hii ya
kupeleka mahindi yao punguza mgawo na elekeza nguvu katika maeneo ambayo
wakulima wameonesha mahitaji ya kupata fedha mimi ndiyo Mkuu wa mkoa nakuagiza tekeleza
jambo hili”, alisisitiza Dokta Mahenge.
Naye kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Songea, Pololet Mgema
alifafanua kuwa wilaya hiyo katika kipindi cha mwaka huu imepata mgao mdogo wa
fedha ambao hauwezi kutosheleza mahitaji ya wakulima ambapo ameiomba serikali
kuangalia uwezekano wa kuongeza fedha za kununulia mahindi hayo ili kuepusha
wakulima wasiweze kupata hasara.
Meneja wa NFRA Kanda ya Songea, Amos Mtafya alisema kuwa
ununuzi wa mahindi katika kanda hiyo ulianza rasmi mwezi Agosti mwaka huu ambapo
kanda hiyo imepangiwa na serikali kununua tani 8,182 za mahindi.
Alisema kuwa katika mgawo huo halmashauri ya wilaya ya
Namtumbo imepangiwa kununua tani 1400, Manispaa ya Songea tani 582, Songea vijijini kata
ya Mgazini tani 2,000, Madaba tani 400, Mbinga mji tani 500, Mbinga vijijini tani
1,100 na Nyasa tani 200.
Mtafya alibainisha kwamba katika zoezi hilo changamoto kubwa
ni ukosefu wa fedha kwani wakulima wamezalisha mahindi mengi na Wakala huyo
hana uwezo wa kuyanunua yote na kwamba taarifa husika zimekwisha pelekwa NFRA
makao makuu juu ya uwepo wa tatizo hilo ili kuweza kuona namna linavyotatuliwa
na kuweza kuwaweka wakulima mahali pazuri.
No comments:
Post a Comment