Na Mwandishi wetu,
Songea.
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umewataka na kuwahimiza
wanamichezo hapa nchini, kuchangamkia fursa ya kujiunga na mpango wa matibabu
kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na wa NHIF ili waweze kupata huduma bora
za matibabu hasa pale wanapougua au kupata majeraha wanapokuwa michezoni.
Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Meneja NHIF mkoani
Ruvuma, Abdiel Mkaro wakati wa Bonanza maalum la kuhamasisha jamii hasa wana
michezo wajiunge na mifuko hiyo ili waweze kuwa na afya bora pale wanapougua.
Pia aliwataka Watanzania wakiwemo waandishi wa habari, kuona
umuhimu wa kijunga na mpango huo kwa lengo la kuwa na uhakika wa kupata
matibabu pale inapotokea wanapata ajali na magonjwa mbalimbali.
Bonanza hilo liliandaliwa na NHIF kwa kushirikisha michezo ya
aina mbalimbali kama vile kukimbia, mazoezi ya viungo, kukimbiza kuku pamoja na
mpira wa miguu ambapo timu ya soka ya Mkambi FC ilifanikiwa kuibuka mshindi baada
ya kuifunga timu ya NHIF magoli 4 kwa 2 kwa njia ya Penati baada ya matokeo ya
awali kufungana 1 kwa 1 katika kipindi cha dakika 90 za mchezo huo.
Pamoja na mambo mengine bonanza hilo lililoonekana kuvutia
watu wengi kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Songea, huku baadhi ya
washiriki wakiomba Mfuko huo wa Taifa Bima ya Afya kuendelea kuandaa bonanza
kama hilo kila mwisho wa mwezi ili kutoa fursa kwa wananchi wengi kushiriki na
kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuepusha uwezekano wa kupata magonjwa.
No comments:
Post a Comment