Na Dustan Ndunguru,
Songea.
KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mkoani
Ruvuma, Rajab Uhonde amewataka wanachama wa chama hicho wilayani humo kuvunja
makundi yote yaliyokuwepo wakati wa mchakato wa kuwapata viongozi wa chama
kuanzia ngazi ya shina, matawi na kata ili kuweza kuendelea kujenga ushindi katika
chaguzi zijazo za dola.
Uhonde alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati
alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake, kuhusiana na jinsi
ambavyo chama hicho kilivyoweza kufanikisha kukamilisha chaguzi mbalimbali kwa
ngazi hizo.
Alisema kuwa baada ya kukamilika kwa chaguzi hizo na kufanikiwa
kuwapata viongozi ndani ya chama kinachotakiwa sasa ni kwa wanachama kubaki
wamoja na pale ambapo patajitokeza kasoro vikao halali vitumike kumaliza kasoro
hizo na sio vinginevyo.
Alifafanua kuwa CCM hivi sasa inajipanga kufanya uchaguzi kwa
ngazi ya wilaya na kwamba aliwaasa viongozi wote waliokwisha chaguliwa wajipange
kikamilifu ikiwemo kufanya vikao vilivyo kwa mujibu wa katiba ya chama ili
kufanikisha masuala muhimu ambayo yataweza kuleta ufanisi.
Alisema lengo la chama chochote cha siasa ni kushika dola
hivyo ili hilo liweze kutimia ni muhimu kwa wanachama kuacha migongano miongoni
mwao na kwamba wanapaswa kushirikiana ambapo kwa kufanya hivyo ushindi utapatikana
bila shaka katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
Kuhusu wanachama wenye tabia ya kuhama chama baada ya
kushindwa kwenye uchaguzi ndani ya chama alisema huu ni uroho wa madaraka, badala
yake wanapaswa kufahamu kwamba katika uchaguzi wa aina yoyote ile kunakuwa na
matokeo mawili kushinda au kushindwa, hivyo pindi inapotokea kushindwa
wanapaswa kuvuta subira na kuwa wavumilivu hadi chaguzi zingine na sio
kukimbilia vyama vya upinzani.
No comments:
Post a Comment