Kikundi cha akina mama ngoma za asili kijiji cha Luhagara kata ya Litumbandyosi wilayani Mbinga wakitumbuiza siku ya uzinduzi wa zoezi la upigaji chapa mifugo (Ngo'mbe) wilayani humo. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAFUGAJI waliopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
wametakiwa kupeleka watoto wao shule na kuacha tabia ya kuwafanya kuwa vibarua
wa kuchunga mifugo.
Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alisema hayo juzi wakati
alipokuwa mgeni rasmi akihutubia wananchi na wafugaji kwenye uzinduzi wa zoezi la upigaji
chapa mifugo (Ng’ombe) katika kijiji cha Luhagara kata ya Litumbandyosi
wilayani hapa.
“Hili sio ombi ni lazima, watoto wote wenye umri wa kwenda
shule sharti wapelekeni shuleni ili waweze kuandikishwa waweze kusoma na kupata
elimu itakayoweza kuwasaidia maishani mwao”, alisisitiza Nshenye.
Alisema kuwa ipo tabia watoto wa wafugaji wengi hawaendi
shule na jambo hili linasababishwa na wazazi wao muda mwingi kuwatumikisha
katika shughuli za kuchunga ngo’mbe badala ya kuwapeleka shule kwenda kusoma.
Vilevile katika hatua nyingine amewataka watendaji wa vijiji
na kata kusimamia sheria namba 12 ya mwaka 2010 inayowataka wafugaji wote
kusajili, kufanya utambuzi na ufuatiliaji wa mifugo yao ili kuweza kudhibiti tabia
ya uingizaji holela wa mifugo na kusababisha migogoro baina ya wafugaji, wakulima
na watu wa mipaka ya hifadhi na mazingira.
Hivyo katika utekelezaji wa zoezi hilo amezitaka halmashauri
ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga zilizopo wilayani hapa kutekeleza agizo hilo
la serikali kupiga chapa mifugo yote.
“Niwatake ndugu zangu wafugaji tuwe na mifugo michache lakini
yenye tija kubwa aidha tuache kuchungia mifugo yetu kwenye mashamba yenye mazao
au kuchungia kwenye misitu iliyohifadhiwa vyanzo vya maji atakayekiuka haya
hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa kwa wale wote watakaokaidi”,
alisema.
Nshenye akizungumzia pia kuhusu upatikanaji wa malisho kwa
ajili ya mifugo ya wafugaji wa wilaya hiyo alisema kuwa serikali inasisitiza
mpango wa matumizi bora ya ardhi ambapo serikali za vijiji zinapaswa kutenga
maeneo ya malisho ya mifugo kwa kuzingatia sheria ya ardhi namba 5 ya mwaka
1999 na sheria ya matumizi ya ardhi namba 6 ya mwaka 2007.
Awali akisoma taarifa ya idara ya mifugo na uvuvi, Mary
Ndunguru ambaye ni afisa mifugo na uvuvi alisema kuwa zoezi hilo la upigaji
chapa mwisho wake ni leo Septemba Mosi mwaka huu kwa halmashauri zote za mkoa
wa Ruvuma.
Ndunguru alieleza kuwa kwa wilaya ya Mbinga zoezi hili
lilianza Julai 24 mwaka huu kwa vijiji vyote 121 vilivyopo katika halmashauri
ya wilaya ya Mbinga.
No comments:
Post a Comment