Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifanya mazungumzo ya kikazi na Balozi wa Iran, Mousa Farhang leo ofisini kwake Magogoni Jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) |
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tanzania ipo salama na
imara na kwamba mtu yeyote atakayejaribu kutaka kuvuruga amani atachukuliwa
hatua kali za kisheria.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Septemba 13, 2017)
alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Bw. Mousa
Farhang jijini Dar es Salaam.
“Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote kutoka popote atakayejaribu
kuvuruga amani yetu. Nawaomba wananchi muwe makini na muendelee kuidumisha
amani yetu.”
Amesema kwa sasa Serikali ipo katika mapambano dhidi ya
vitendo vya ufisadi, rushwa, biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na
wahujumu uchumi.
Waziri Mkuu amesema licha ya Tanzania kuwa ni nchi ya amani
na yenye utulivu wa kisiasa, wameendelea kuwahamasisha wananchi wake kudumisha
mshikamano.
Amesema mbali ya kuimarisha amani nchini, pia Serikali
imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji jambo ambalo litawawezesha watakaokuja
kuwekeza nchini kupata tija.
Hivyo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka
nchini Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo vya kuchakata
mazao ya kilimo.
Pia amewakaribisha raia wa Iran kutembelea vivutio mbalimbali
vya utalii vilivyoko nchini Tanzania kama mlima wa Kilimanjaro, fukwe, mali
kale na mbuga za wanyama.
Kwa upande wake, Balozi Farhang ameipongeza Serikali kwa kuwa
na dhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi na kupambana na dawa za kulevya na
ufisadi.
Balozi huyo amesema Serikali ya Irani ipo tayari kushirikiana
na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi pamoja na
vitendo vingine vya kihalifu.
Balozi Farhang ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya
Tanzania ifungue Ofisi ya Ubalozi nchini Iran ili kuimarisha uhusiano huo,
ambapo Waziri Mkuu amekubali.
Pia Bw. Farhang amesema aliwahi kutembelea mbuga za wanyama
za Serengeti na Ngorongoro na kusema kwamba ni maeneo mazuri ambayo hajawahi
kuyaona tangu azaliwe.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, SEPTEMBA 13, 2017.
No comments:
Post a Comment