DAWA za kulainisha nywele (Relaxer) ambazo zimekuwa
zinapendwa na wanawake wengi wa Afrika kwa kuwa zina uwezo wa kulainisha nywele
na kumfanya apendeze na awe wa kuvutia imeelezwa kuwa ni hatari kwa afya zao.
Wataalamu wa afya wanadai kuwa dawa hizo zinasababisha uvimbe
kwenye kizazi kutokana na kemikali za dawa hizo huingia mwilini kupitia
majeraha au ngozi wakati wa kupaka.
Daktari wa Manispaa ya Ilala, Laurent Chipata amefanya
utafiti na kubaini kuwa dawa za nywele na vipodozi zina kemikali ambazo
husababisha uzalishwaji wa vichocheo kwa kiasi kikubwa na kusababisha uvimbe
kwenye kizazi uitwao Fibroids au Leimyoma.
“Kemikali hizi hupenya kwenye ngozi na wakati mwingine hata
kwa harufu tu, husababisha kuzalishwa kwa wingi wa vichocheo aina ya Estrogen
ambavyo huchangia kuota kwa uvimbe wa Fibroids,” alisema Dokta Chipata.
Dokta Chipata alisema kuwa kukua kwa uvimbe kwenye kizazi
hutokea katika kipindi ambacho mama yupo kwenye uzazi yaani kabla hajakoma
hedhi.
Utafiti wa Dokta Chipata ulifanywa nchini na kujumuisha
wanawake wa kada tofauti tofauti wanaotumia dawa za nywele na wale wasiotumia
na ukubwa wa tatizo hili ulibainika.
“Zipo kemikali tofauti tofauti zinazosababisha uvimbe kwenye
kizazi, zipo za kwenye dawa za kilimo kama DDT na zile kwenye mafuta ya ngozi
kama vile Mercury na Hydroquionone,” alisema.
Alisema kuwa madhara yanayopatikana katika kemikali za
vipodozi ni makubwa siyo tu kwenye kizazi bali nyingine husababisha Saratani au
kufeli kwa figo. Anatoa mfano wa kemikali ya Zebaki (Mercury).
“Dawa za nywele zina madhara si lazima zipenye kwenye ngozi
baada ya mtu kupata jeraha la kuungua bali zinaweza kupenya zenyewe kwenye
ngozi kutokana na mfumo wa ngozi,” alisema Dokta Chipata.
Pia alishauri kuwa ni vyema watu wakasoma kwanza kipodozi
kimetengenezwa kwa nini kabla ya kukitumia na kuongeza kuwa ni salama zaidi
kubaki na ngozi au nywele halisi badala ya kujibadilisha.
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekataza vipodozi vyenye
kemikali kama biothionol, hexachlorophene, mercury, vinylchloride, zirconium na
bidhaa zenye aerosol, chloroquionone, steroids, methylene na chloroform.
Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2012 na Dokta Lauren Wise
na wenzake nchini Marekani na kuchapishwa kwenye Jarida la afya la nchini
Marekani ulibaini kuwa vipodozi vingi vina kemikali zenye vichocheo vya
estrogen ambavyo kwa kawaida huchochea kasi ya kuota kwa uvimbe kwenye kizazi
cha mwanamke na wakati mwingine kwenye mji wa mimba. Kitaalamu uvimbe au
vivimbe hivi hujulikana kama Fibroids au Myoma.
Dokta Wise alisema kuwa aliwafanyia uchunguzi wanawake
wanaotumia dawa za kulainisha nywele na kuangalia umri walioanza kutumia dawa
hizo, mara ngapi, waliungua kiasi gani na walikaa na dawa hizo kichwani kwa
kipindi gani.
Aliwafuatilia wanawake 23,580 wanaotumia dawa za kulainisha
nywele na baada ya kipindi fulani walipimwa. Kati yao, 7146 waligundulika kuwa
na uvimbe kwenye kizazi baada ya kupimwa kwa mionzi na wengine kufanyiwa
upasuaji.
Kwa nini Relaxer ni hatari kwa wanawake?
Dokta Wise alifafanua kuwa mchanganyiko uliokwenye dawa za
nywele hasa zilizoandikwa “Lye Relaxer” ni sodium hydroxide wakati makopo ya
dawa yaliyoandikwa “No Lye Relaxer” yana calcium hydroxide na guanidine
carbonate.
Bidhaa za kulainisha nywele zilizoandikwa ‘No lye relaxer’
zinadaiwa kusababisha majeraha kwa kiasi kidogo ukilinganisha na zile
zilizoandikwa “Lye Relaxer”.
No comments:
Post a Comment