Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKUU wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Pololet Mgema
amewashushia lawama na kuwashitaki kwa Rais Dokta John Pombe Magufuli wafanyakazi
wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani humo kwamba wanafanya kazi kwa
mazoea, badala ya kwenda na kasi ya awamu ya tano inayolenga kuongeza ufanisi katika
utekelezaji wa mpango wa kuharakisha maendeleo hapa nchini.
Mkuu wa wilaya ya Songea, Pololet Mgema. |
Mgema alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumza na
wananchi na baadhi ya wafanyakazi wa Shirika hilo katika kijiji cha Litapaswi kata ya
Mpitimbi wilayani humo.
Kwa mujibu wa Mgema alisema kuwa wafanyakazi hao wameshindwa
kubadilika na kuendana na kasi ya Rais Dokta Magufuli kwa kile alichoeleza kuwa
wamekuwa wakitumia muda mwingi kukaa ofisini na kusubiri wateja badala ya
kuwafuata walipo jambo ambalo linasababisha baadhi ya watu kutofikishiwa huduma
ya umeme kwa wakati.
“Bado watumishi wa TANESCO wanafanya kazi kwa mazoea kwa
kuwasubiri wateja ofisini badala ya kuwafuata pale walipo, kuna wateja wakubwa
wanahitaji huduma ya umeme kwa ajili ya shughuli zao lakini watumishi hawa ni
kikwazo kikubwa, wanatumia muda mwingi kukaa ofisini badala ya kwenda kwa mteja”,
alisema Mgema.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya aliishukuru serikali ya awamu ya
tano kwa kuhakikisha mkoa wa Ruvuma unaunganishwa na gridi ya taifa chini ya mradi
wa Makambako Songea ambao unatarajia kukamilika mwakani.
Alisema kuwa serikali ya mkoa huo itahakikisha inakuwa karibu
na kufuatilia ujenzi wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati na
kuwawezesha wananchi kuharakisha kukua kiuchumi kupitia nishati ya umeme.
Mkoa wa Ruvuma una vijiji 507 hata hivyo vijiji vitakavyo
bahatika kuunganishiwa umeme ni 209 ambapo ameiomba serikali chini ya Wizara ya
nishati kuhakikisha kwamba vijiji vilivyobakia vinaingizwa katika mpango huo wa
kupata umeme.
Hata hivyo Mgema aliongeza kuwa umeme huo utaweza kuchochea kukua
kwa uchumi wao kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na vikubwa, hasa ikizingatiwa
kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wake wanategemea kilimo hivyo umeme
utasaidia kuanzisha viwanda kwa ajili ya kuongeza thamani mazao mbalimbali
wanayozalisha.
No comments:
Post a Comment