Dokta Khamis Kigwangala. |
Na Waandishi wetu,
WAKUU wa mikoa na wilaya hapa nchini, wametakiwa kusimamia
kikamilifu upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kuanzia kwenye zahanati, vituo vya
afya na hospitali ili wananchi waweze kupata huduma bora.
Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dokta Khamis Kigwangala alipokuwa
akifungua majengo ya kutoa huduma ya afya ya uzazi katika zahanati 26 mkoani
Kigoma, shughuli iliyofanyika kijiji cha Mwakizega, wilaya ya Uvinza mkoa wa
Kigoma.
Dokta Kigwangala alisema kuwa serikali imetenga shilingi
bilioni 269 kwa ajili ya kununua dawa katika kipindi cha mwaka huu ambapo mwaka
jana 2015 kiasi kilichotengwa kununua dawa hizo kilikuwa ni shilingi bilioni
31.
Shirika la Engender Health limejenga majengo 26 ya kutoa
huduma ya afya ya uzazi yenye uwezo wa kutoa huduma ya uzazi na upasuaji wa
dharura pindi inapohitajika, kwa vile baadhi ya wilaya hazina hospitali za
wilaya ambazo ni ngazi ya rufaa kwa wagonjwa wanaotoka kwenye vituo vya afya na
zahanati.
“Vifo vya akina mama na watoto lazima vipungue kuanzia ngazi
ya familia, jamii, vituo vya kutoa huduma ya afya kwa sababu kama kila mmoja
atakuwa makini kufuata maelekezo ya wataalamu ni wazi vifo vitapungua, maana
asilimia 19 ya vifo vinavyotokana na uzazi chanzo ni kuharibika mimba”, alisema
Dokta Kigwangala.
Alisema kuwa mkoa wa Kigoma kuna vifo 248 katika kila vizazi
hai 100,000 ambapo chanzo chake ni kuvuja damu nyingi wakati wa kujifungua na
ukosefu wa damu.
Naibu mwakilishi mkazi wa EngenderHealth Tanzania, Lulu
Ng’wanakilala alisema mradi huo ulihusisha ujenzi wa zahanati mpya 24 na
ukarabati wa nyingine mbili zilizogharimu shilingi bilioni 2.749 huku vifaa
tiba vikigharimu shilingi milioni 612.5.
Ng’wanakilala alieleza kuwa watoa huduma 417 walipata mafunzo
ya kuhudumia akinamama wajawazito ambapo wengine 156 walifundishwa jinsi ya
kuhudumia na kutoa elimu vijana 10,700 mkoani Kigoma.
Mwakilishi wa Bloomberg Philanthropies hapa nchini, Dokta
Godson Maro alisema wataendelea kutoa ufadhili kwenye miradi ya afya mkoani humo
ambapo lengo ni kufikia asilimia 75 ya akinamama wanaojifungua katika vituo vya
huduma ya afya ifikapo mwaka 2019.
Vifo zaidi ya 100 vinavyotokana na uzazi vimezuiliwa na
magonjwa ya kuambukiza yamepunguzwa kutokana na kuboreshwa kwa huduma ya afya
katika ngazi ya zahanati hadi hospitali za juu.
“Hadi sasa akinamama 5,000 walijifungua katika vituo vya
huduma na mimba 289,217 zisizopangwa zilizuiliwa, lakini pia mimba zaidi ya
89,000 hazikuharibika kama ilivyokuwa awali huduma ilipokuwa haijaboreshwa”, alisema
Dokta Maro.
Kaimu Mganga mkuu mkoa wa Kigoma, Dokta Fadhil Kibaya alisema
hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu asilimia 76 ya dawa zilizopatikana ambapo
lengo la kitaifa lilikuwa ni asilimia 80.
No comments:
Post a Comment