RAIS Dokta John Pombe Magufuli amewataka viongozi mbalimbali wa Serikali
ambao wametajwa kwenye ripoti za Bunge ya madini ya Almasi na Tanzanite, waachie
ngazi mapema katika nafasi zao ili vyombo vya usalama viweze kufanya kazi yake
vizuri katika kuwachunguza na kuwachukulia hatua za kisheria.
Kauli ya Rais huyo aliitoa leo wakati alipokuwa akikabidhiwa
ripoti hizo Ikulu Jijini Dar es Salaam mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi
wengine walioalikwa katika tukio hilo la makabidhiano ya ripoti hizo.
“Wapo watu wametajwa tajwa na wengine mimi ndio nilihusika kuwateua
sasa ukishatajwa tajwa, naagiza vyombo vya ulinzi na usalama vifuatilie hili
tena kwa haraka na wale ambao wametajwa kwenye ripoti hii ambao ni wateule
wangu ili vyombo vya usalama viweze kufanya kazi yake vizuri ni matumaini yangu
watakaa pembeni”, alisema Rais Magufuli.
Pia alieleza kuwa atashangaa kuona endapo watu waliotajwa
kwenye sakata hilo la wizi wa madini hayo hawataanza kukamatwa na kwamba leo
hii anataka wakamatwe.
Katika ripoti hiyo ambayo iliwasilishwa jana mjini Dodoma na hivi
leo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumkabidhi Rais Magufuli iliweza kuwataja
baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za
mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene, Waziri wa zamani wa
Nishati na Madini na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja pamoja na aliyekuwa
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na viongozi wengine
mbalimbali ambao Rais ameagiza washughulikiwe haraka.
Pamoja na mambo mengine Rais Magufuli alisema kuwa Profesa Abdulkadir
Mruma ambaye pia alitajwa kwenye ripoti hizo alipandikizwa kwa maadui ili
kuibua taarifa ya namna nchi inavyoibiwa madini.
No comments:
Post a Comment