Na Mwandishi wetu,
Madaba.
MKUU wa wilaya ya Songea Pololet Mgema amepiga marufuku
maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za ufugaji kutumika kwa kazi ya kilimo, badala
yake wakulima watumie maeneo yao yaliyoainishwa na serikali zao za vijiji au
kata kwa kazi hiyo.
Alisema serikali imekwisha maliza kazi ya kuainisha
maeneo yote kwa ajili ya ufugaji na kilimo katika halmashauri mbalimbali za
wilaya hivyo wanachopaswa kutekeleza ni kufuata sheria, kanuni na taratibu
zilizowekwa ili kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
“Katika wilaya hii sitaki kusikia kuna migogoro kati ya
wakulima na wafugaji kugombea masuala ya ardhi, serikali imekwisha maliza kuainisha
maeneo yote kwa ajili ya shughuli za maendeleo naagiza kila mmoja wetu
kuzingatia maelekezo haya”, alisema.
Mgema alisema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa zoezi la usajili,
utambuzi na ufuatiliaji wa mifugo katika kijiji cha Hanga kata ya Gumbiro halmashauri
ya wilaya ya Madaba mkoani hapa.
Aliwataka pia wananchi kuheshimu mipaka iliyowekwa na sio
kuingilia maeneo yaliyohifadhiwa na kuleta migogoro isiyokuwa na tija katika
jamii ambayo inarudisha nyuma maendeleo yao na kuleta madhara makubwa.
Katika hatua nyingine Mgema, ameiagiza halmashauri ya wilaya
ya Madaba kuhakikisha kwamba inatenga fedha za kutosha kwa ajili ya huduma za
mifugo kama vile chanjo na ujenzi wa miundombinu husika katika maeneo ya
ufugaji ili wafugaji waweze kufuga kisasa hatua ambayo itaweza kusaidia serikali
kupata mapato yake.
Awali naye Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo, Shafi Mpenda
akizungumza katika uzinduzi wa zoezi hilo alisema kuwa huo ni utekelezaji wa
sheria ya Bunge namba 12 ya mwaka 2010 ambapo Serikali imeagiza Sekretarieti za
mikoa kufanya utekelezaji huo kupitia halmashauri zake za wilaya.
Mpenda alieleza kuwa uzinduzi wa kupiga chapa mifugo kimkoa
ulifanyika Julai 18 mwaka huu katika kijiji cha Matepwende halmashauri ya
wilaya ya Namtumbo, ambapo mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge aliagiza
halmashauri zote nane za mkoa huo kukamilisha kazi hiyo kabla ya Septemba Mosi 2017.
Alisema kuwa kwa halmashauri ya Madaba imejitahidi
kuhamasisha na kuelimisha wafugaji wake juu ya umuhimu wa zoezi hilo na wengi
wameitikia wito huo kwa maendeleo ya ufugaji wenye tija.
Alibainisha kuwa kufuatia hali hiyo anayo imani kubwa kwamba,
wataweza kuwa na daftari la kudumu lenye takwimu za mifugo ambalo litakuwa
linaboreshwa kila baada ya miezi sita.
No comments:
Post a Comment