Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI wenye matatizo ya aina mbalimbali katika jamii yanayohitaji
msaada wa kisheria na ushauri wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa
kuchangamkia fursa hiyo na kujitokeza kwa wingi ili waweze kupata msaada huo.
Aidha imeelezwa kuwa msaada utakaotolewa ni bure, hivyo watumie
fursa hiyo kwenda katika Ofisi za Kituo cha sheria na haki za binadamu zilizopo
mtaa wa Mbuyula, jengo la Mwalimu house karibu na hospitali ya wilaya hiyo iliyopo mjini hapa.
Mkurugenzi wa utetezi na maboresho kutoka Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam, Anna Henga akiwa ameambatana na Wataalamu
wenzake wa kisheria alisema hayo leo wakati alipokuwa akitoa utambulisho kwa Ofisi
ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga kwa Katibu tawala wa wilaya hiyo, Mhandisi Gilbert Simya.
Anna alifafanua kuwa kazi kubwa waliyokuja kuifanya wilayani
humo ni kutoa msaada wa kisheria bure kwa wananchi, wakishirikiana na Wasaidizi
wao wa kisheria (Paralegals) waliopo wilayani hapa kwa muda wa siku tano kuanzia Septemba 19
hadi 23 mwaka huu majira ya asubuhi hadi jioni.
Alisema kuwa masuala watakayohudumiwa wananchi wenye matatizo
ni pamoja na mashauri ya ndoa, ardhi, ajira, taratibu za kimahakama, uandaaji
wa nyaraka na mikataba ya madai mbalimbali, mirathi, sheria za mtoto, bima, ushauri
katika kesi za jinai na mengineyo yanayohusiana na masuala ya kisheria.
Vilevile aliongeza kuwa LHRC wamekuwa wakitembelea na kutoa
huduma katika wilaya ambazo kuna wasaidizi wao wa kisheria na haki za binadamu na
kwamba kuna wilaya 30 hapa nchini ambazo wananchi tayari wamekuwa wakipata
huduma hizo kutoka katika kituo hicho.
Kadhalika kwa muda wa siku hizo pia watakuwa wakitoa huduma
kwa wananchi wengine waliopo katika kata ya Litembo, Mapera, Matiri, Kigonsera,
Utiri, Mbinga mjini na Mpapa zilizopo wilayani humo.
“Kwa mwaka tunatembelea wilaya tatu mpaka nne na mpango wetu
wa baadaye ni kupanua huduma zetu kwa kuweza kuwafikia wananchi waliopo kwenye
wilaya zote zilizopo hapa Tanzania”, alisema Henga.
Pia alieleza kuwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu huu ni
mwaka wa 22 sasa hapa Tanzania tokea waanze shughuli hizo, ambapo kwa mwaka hutoa
msaada wa kisheria na ushauri kwa watu 12,000.
Naye kwa upande wake Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga, Simya alifurahishwa na ujio wa wageni hao wa kutoa huduma hizo za kisheria na
kueleza kuwa, watakuwa ni msaada mkubwa katika kutatua migogoro mbalimbali
ikiwemo ya ardhi ambayo imeshamiri wilayani hapa.
“Ninyi mtakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wetu, tunaomba mshirikiane na Ofisi hii ya Mkuu wa wilaya mtusaidie kuhamasisha watu wajitokeze kwa wingi ili tuweze kusuluhisha migogoro iliyopo ndani ya jamii”, alisema Simya.
“Ninyi mtakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wetu, tunaomba mshirikiane na Ofisi hii ya Mkuu wa wilaya mtusaidie kuhamasisha watu wajitokeze kwa wingi ili tuweze kusuluhisha migogoro iliyopo ndani ya jamii”, alisema Simya.
No comments:
Post a Comment