Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MRADI wa Panda miti kibiashara ambao umeanzishwa katika
Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, umeweza kuzalisha miche bora ya
miti milioni 1.2 katika kitalu cha miti Kihaha kilichopo mjini hapa ambayo
watagawiwa wananchi bure na kuipanda ili waweze kuondokana na umaskini.
Aidha imeelezwa kuwa miche hiyo itapandwa katika hekta 500 msimu
wa mvua mwaka huu katika eneo la Lihumbe na Ukimo kata ya Mbangamao pamoja na Lipilipili
kata ya Mpepai.
Imeelezwa kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuwasaidia wananchi
maskini ambao wamejiunga kwenye vikundi katika maeneo hayo, ili waweze kuinua
kipato chao kwa njia ya panda miti kibiashara ambapo watagawiwa bure miti hiyo na
kuipanda kwa njia ya kitaalamu ili baadaye waweze kuvuna mbao bora.
Mwandishi wa habari hizi ambaye alitembelea katika eneo la
uzalishaji wa miche hiyo na kuzungumza na Afisa misitu wa halmashauri ya mji
huo, David Hyera alisema kuwa miche ya miti iliyozalishwa kwenye kitalu hicho
ni aina ya Milingoti (Eucalyptus) na Mikaratasi (Pines).
Hyera alisema kuwa upandaji wa miti hiyo ambao ni wa mbegu
bora ukishafanyika kitaalamu uvunaji wake unakuwa ni wa muda mfupi tokea
ipandwe ardhini tofauti na mtu ambaye hutumia mbegu za kienyeji.
Alifafanua kuwa miche aina ya Milingoti ikishapandwa uvunaji
wake unakuwa ni wa ndani ya miaka mitano ambapo mpandaji anaweza kupata faida
ya kuvuna nguzo, kama zile ambazo hutumiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
tofauti na yule anayetumia mbegu za kienyeji huchukua muda wa zaidi ya miaka 10
mpaka kuanza kuivuna.
Pia aliongeza kuwa kwa yule ambaye hupanda miti aina ya Mikaratasi
kwa kutumia mbegu bora uvunaji wake hutumia miaka 12 tu, tofauti na yule
atakayetumia mbegu za kienyeji huchukua muda wa zaidi ya miaka 20 mpaka
kuivuna.
“Kwa mwaka huu eneo la Lihumbe na Ukimo kata ya Mbangamao
pamoja na Lipilipili kata ya Mpepai, mradi unakwenda kwenye vikundi vya
wananchi na kupandwa miti hii bora katika hekta 500 zilizopo kwenye maeneo hayo”,
alisema Hyera.
Alibainisha kuwa eneo hilo la upandaji ni la serikali na
kwamba litabaki kuwa la serikali, lakini miti itakayopandwa itabaki kuwa mali
ya wananchi wenyewe walioipanda ambao wataingia mkataba wa maelewano sio chini
ya miaka 33 na halmashauri ya mji wa Mbinga.
Vilevile alieleza kuwa mkataba huo utawawezesha wananchi hao
kupanda miti hiyo mpaka kuivuna, watapata kipato ambapo halmashauri hiyo na
serikali kwa ujumla itaweza kupata ushuru wake kupitia mavuno yatakayofanyika
kwenye miti hiyo na hatimaye kuweza kuboresha huduma za kijamii.
Hyera alisema kuwa mradi wa uzalishaji miche katika kitalu
cha Kihaha unafanywa kwa ufadhili wa nchi ya Finland na kusimamiwa na Wakala wa
mbegu za miti Tanzania chini ya usimamizi wa Afisa misitu huyo wa halmashauri
ya mji wa Mbinga.
Kadhalika mradi huo tokea uanzishwe miaka minne iliyopita
umeweza kusaidia kutengeneza ajira kwa wakazi wanaoishi karibu na eneo la
kitalu hicho kufuatia malipo wanayolipwa kwa wale wanaofanya kazi za ugani, utunzaji
wa vitalu na upandaji miti vijijini.
No comments:
Post a Comment