Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Abdul Mshaweji akiwa katika zoezi la ugawaji wa vyandarua katika mitaa mbalimbali ya Manispaa hiyo mjini hapa. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imegawa
vyandarua 35,874 kwa wanafunzi wa shule za msingi 81 zilizopo katika Manispaa
hiyo ili kuweza kukabiliana na ugonjwa wa Malaria.
Katika Manispaa hiyo pia imegawa vyandarua 450 kwa wazee wasiokuwa
na uwezo katika mitaa mbalimbali iliyopo mjini hapa ambapo zoezi hilo pia malengo
yake ni kufikia hatua ya kuwagawia vyandarua 1,000.
Albano Midelo ambaye ni Afisa habari wa Manispaa hiyo,
alisema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu huku akiongeza
kuwa hizo ni jitihada za kuutokomeza ugonjwa wa Malaria.
Midelo alifafanua kuwa halmashauri hiyo pia imepokea lita 1,000
za dawa ya kuua Mbu wanaoeneza ugonjwa huo na kwamba muongozo wa namna ya kutumia
dawa hiyo, umekwisha tolewa na serikali mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu huku
zoezi la upuliziaji kwenye maeneo mbalimbali linatarajiwa kuanza wakati wowote
kuanzia sasa.
Kiwango cha maambukizi ya Malaria katika halmashauri ya
Manispaa ya Songea ni asilimia 2.5.
Alibainisha kuwa hatua ambazo zinachukuliwa na Manispaa hiyo
katika kupambana na ugonjwa huo ni pamoja na kuhakikisha kwamba upatikanaji wa
dawa na vitenganishi kwa ajili ya matibabu vinakuwa vya kutosha ikiwemo na utekelezaji
mradi mdogo wa kitaifa wa usambazaji vyandarua kwa wanafunzi shule za msingi.
Mikakati mingine ya kupambana nao ni kuendelea kuhamasisha na
kuelimisha jamii juu ya matumizi sahihi ya vyandarua, kufanya zoezi la utambuzi
wa mazalia ya mbu kwenye kata zote ambazo zina maambukizi makubwa ya malaria hayo
ikiwemo na ufuatiliaji wa tiba sahihi ya ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment