Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.
WANUFAIKA waliopo katika mpango wa kunusuru kaya maskini, ambao
unasimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma, wametakiwa kutumia vizuri fedha wanazozipata kutoka kwenye mfuko huo kwa
kuanzisha miradi midogomidogo ambayo itawakwamua kiuchumi.
Emmanuel Fikiri ambaye ni Afisa ufutiliaji wa TASAF wilayani
humo, alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na wanufaika wa kijiji cha
Mihango mara baada ya kutembelea na kukagua miradi yao ya ufugaji ambayo wameianzisha
kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Alisema kuwa malengo ya mpango huo wa kunusuru kaya maskini
ni kuweza kuwainua kiuchumi wananchi ambao hali zao kimaisha ni duni sio za
kuridhisha.
Fikiri alieleza kuwa miradi midogomidogo ya ufugaji kama
vile wa kuku wa kienyeji ni mzuri kwani ufuatiliaji wake ni rahisi, kutokana na
ukweli kwamba kuku hao hawashambuliwi kwa urahisi na magonjwa na mfugaji huweza
kupata mafanikio makubwa kwa muda mfupi.
“Nimewatembelea wanufaika ambao wamejikita na ufugaji wa kuku
na nguruwe kweli nafarijika na kazi wanazozifanya, niwaombe tu waendelee
kutumia vyema fedha wanazozipata na wajiepushe na matumizi mabaya ikiwemo
kuendekeza unywaji wa pombe”, alisema Fikiri.
Afisa ufuatiliaji huyo alisema ofisi yake itaendelea
kufuatilia kwa karibu matumizi ya fedha hizo zinazotolewa na mfuko huo, kwa
lengo la kuweza kunusuru kaya maskini wilayani humo na kwamba viongozi wa
vijiji na kata wanapaswa kupitia mikutano yao ya hadhara wahakikishe wanaendelea
kuhamasisha na kuwaelimisha wale ambao ni walengwa wa mpango huo juu ya
matumizi bora ya fedha hizo ili waweze kuendelea kuimarisha miradi yao midogo
wanayoianzisha hatimaye waondokane na umaskini.
Fikiri alisisitiza pia juu ya umuhimu wa wanufaika hao kujiunga
na mfuko wa bima ya afya ili hatimaye waweze kunufaika na matibabu bure kwa kipindi
cha mwaka mzima na kwamba fedha wanazozipata.
No comments:
Post a Comment