Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.
WANANCHI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wametakiwa kuepuka
kusikiliza kauli za watu wanaopita kwenye maeneo yao wanayoishi, ambao hutoa
lugha za upotoshaji kuhusiana na matumizi ya dawa zinazotolewa na serikali
katika jamii kwa ajili ya kuzuia na kutibu magonjwa yaliyokuwa hayapewi
kipaumbele.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mratibu wa magonjwa yaliyokuwa
hayapewi kipaumbele wa wilaya hiyo, Sebastian Mhagama wakati alipokuwa akizungumza
na mwandishi wa habari hizi juu ya magonjwa hayo jinsi ambavyo yanavyoathiri
jamii.
Mhagama alisema kuwa jitihada kubwa inaendelea kufanyika kila
mwaka wilayani humo kutibu wale wote ambao huathirika sambamba na utoaji wa
elimu kwa wananchi, ili kuwafahamisha namna ya kuepukana nayo lakini kikwazo
kikubwa kimekuwa kutoka kwa baadhi ya watu ambao wamekuwa na tabia ya
kuwakatisha tamaa wenzao wanaotumia dawa hizo.
Aliyataja magonjwa hayo kuwa ni usubi, kichocho, matende na
mabusha ambayo licha ya kutopewa kipaumbele lakini hivi sasa yanapewa kipaumbele
kikubwa na yamekuwa yanatibika na kuzuilika, hivyo serikali kupitia Wizara ya
afya na ustawi wa jamii kwa kuhusisha halmashauri za wilaya dawa za magonjwa
hayo zimekuwa zikitolewa kwa wananchi wote bila ubaguzi.
Alisema kuwa pamoja na magonjwa hayo kutopewa kipaumbele kwa siku
za nyuma lakini bado yalikuwa na athari kubwa katika jamii na kwamba maeneo yaliyoathirika
zaidi wilayani hapa ni ukanda wa bonde la ziwa Nyasa ambalo limeathirika kwa
kichocho, usubi, minyoo ya tumbo, mabusha na matende kutokana na madimbwi ya
maji ambayo huzalisha mbu kwa wingi.
Mhagama alifafanua kuwa jamii imeelimishwa kuhusiana na madhara
ya magonjwa hayo na kuwapa dawa za kutibu na kuzuia ambapo hupewa mara moja kwa
mwaka na pia dawa hizo hutolewa bure.
Kadhalika alieleza kuwa magonjwa hayo licha ya kutopewa
kipaumbele bado ni vyema jamii ikatambua wazi kwamba madhara yake ni makubwa hasa
pale binadamu yanapompata, hivyo jamii inashauriwa mara kwa mara kusikiliza
ushauri unaotolewa na wataalamu ili kuweza kuepukana nayo au kuyatokomeza
kabisa.
No comments:
Post a Comment