Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.
WANANCHI wa kata ya Kihungu, Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoa
wa Ruvuma wameipongeza serikali ya awamu ya tano hapa nchini kupitia Wizara ya
elimu, sayansi, teknolojia na ufundi kwa kuipatia shule ya msingi Kihungu iliyopo
katika kata hiyo, shilingi milioni 66.6 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya
madarasa na vyoo vya shule hiyo.
Naibu wa Wizara ya elimu, Injinia Stella Manyanya. |
Aidha imeelezwa kuwa hali hiyo itawawezesha wanafunzi wa
shule hiyo kuweza kusoma katika mazingira mazuri na kuinua kiwango chao cha
ufaulu wa masomo hasa pale wanapokuwa darasani.
Katika kikao kilichofanyika jana shuleni hapo na kuhudhuriwa
na wazazi, walimu na wanafunzi hao walisema kuwa shule yao ambayo ilijengwa
miaka ya tisini iliyopita na wananchi wenyewe ina vyumba vya madarasa na vyoo
vilivyokuwa chakavu ambavyo sio rafiki kwa matumizi ya watoto hao.
Mashaka Lupogo ambaye ni mkazi wa kijiji hicho licha ya
kuipongeza serikali alisema kuwa fundi ambaye amepewa jukumu la kujenga vyumba
hivyo vya madarasa na vyoo hivyo anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa umakini
mkubwa ili ujenzi wa viwango vinavyotakiwa uweze kufikiwa kulingana na thamani
halisi ya fedha iliyotolewa na serikali.
Vilevile naye Aderick Komba na Romwald Komba walisema kwa
nyakati tofauti kuwa wale viongozi wenye jukumu la kusimamia ujenzi huo pia
wanapaswa kuhakikisha kwamba, malengo husika yanafikiwa ili kuwepo na matumizi
mazuri ya fedha hizo na kwamba wao kama wananchi hawatasita kutoa taarifa sehemu
husika pale watakapobaini uwepo wa dalili za matumizi mabaya ya fedha hizo.
Mtaalamu wa majengo wa halmashauri ya mji wa Mbinga ambaye ni
msimamizi mkuu wa ujenzi wa miundombinu hiyo ya shule ya msingi Kihungu, Jordan
Kapinga alisema kuwa atahakikisha anatekeleza majukumu yake ipasavyo ili
hatimaye yaweze kupatikana majengo yenye ubora unaotakiwa.
Naye fundi aliyepewa jukumu la ujenzi wa shule hiyo, Valence
Urio alithibitisha kuwa atatekeleza jukumu hilo alilopewa na serikali kwa ufanisi
mzuri ili hatimaye vyumba hivyo vya madarasa na vyoo viweze kukamilika ujenzi
wake kwa wakati na viwango vinavyotakiwa na hatimaye miundombinu yake iweze
kudumu kwa miaka mingi kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
No comments:
Post a Comment