Uboreshaji wa Manispaa ya Songea ukiendelea kufanyika. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
IMEELEZWA kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma
imepokea jumla ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya uboreshaji wa bustani ya
Manispaa hiyo.
Mradi huo unafadhiliwa na Benki ya dunia chini ya Mpango wa Kuzijengea
Uwezo Serikali za Mitaa (ULGSP) na kwamba unatarajiwa kugharimu shilingi
milioni 399.95.
Hayo yalisemwa na Afisa habari wa Manispaa ya Songea, Albano
Midelo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu mjini hapa ambapo alifafanua
kuwa fedha ambazo zimekwisha lipwa hadi sasa ni shilingi milioni 97.83 na fedha
iliyobaki ni shilingi milioni 302.12.
Alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ujenzi wa miundombinu
mbalimbali katika kipindi cha miezi sita ambapo ulianza kujengwa Machi 15 mwaka
huu na unatarajiwa kumalizika ujenzi huo Septemba 30 mwaka huu.
Mradi huo ambao upo mkabala na Ofisi za halmashauri ya
Manispaa hiyo unajengwa eneo la mgahawa, choo cha kulipia, uzio na maeneo ya
kupaki magari (Parking bay).
Pia aliongeza kuwa bustani hiyo katika mji wa Songea ina eneo
la kupumzikia (Resting huts) na kwamba hatua ya ujenzi imefikia zaidi ya
asilimia 70.
Maeneo mengine ambayo yanaendelea katika bustani hiyo ni
ujenzi wa uzio kuzunguka bustani yote, utengenezaji wa bustani ambayo inawekwa
udongo na kupandwa nyasi na miti na ujenzi wa mnara na kazi ya kusambaza maji
katika eneo la ujenzi.
Manispaa ya Songea ni moja kati ya halmashauri za miji na
Manispaa 18 za Tanzania bara ambazo zipo katika mpango wa ULGSP ikiwa ni lengo la
kuendeleza miundombinu yake.
No comments:
Post a Comment