Tuesday, September 19, 2017

WASAIDIZI WA KISHERIA MBINGA WAVITAKA VYOMBO VYA DOLA KUELIMISHA WANANCHI

Upande wa kushoto anayezungumza ni Mkurugenzi wa utetezi na maboresho kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam, Anna Henga akiwa pamoja na Wafadhili wa kituo hicho kutoka Ubalozi wa ufalme wa Sweden na Norway katika kikao cha pamoja kilichofanyika leo na Wasaidizi wa kisheria (Paralegals) wa wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma katika Ofisi za wilaya hiyo zilizopo mtaa wa Mbuyula karibu na hospitali ya wilaya iliyopo mjini hapa.

Wasaidizi wa kisheria (Paralegals) kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakiwa katika kikao na viongozi wa LHRC kutoka jijini Dar es Salaam pamoja na Wafadhili wao wa Ubalozi wa ufalme wa Sweden na Norway, kikao ambacho kilifanyika katika Ofisi za kituo hicho zilizopo mtaa wa Mbuyula karibu na hospitali ya wilaya mjini hapa.
Wasaidizi wa kisheria (Paralegals) wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma leo wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kutoka jijini Dar es Salaam na Wafadhili wao wa kutoka Ubalozi wa ufalme wa Sweden na Norway katika Ofisi ya wilaya hiyo ya LHRC iliyopo mjini hapa.
Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

KUFUATIA kushamiri kwa matukio ya watu kuchukua sheria mkononi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Wasaidizi wa kisheria (Paralegals) Kituo cha Sheria na Haki za binadamu (LHRC) wilayani humo wamevitaka vyombo vya dola kuelimisha wananchi ili wasiendelee kufanya vitendo hivyo.

Wasaidizi hao walisema kuwa wananchi hao wamekuwa na tabia ya kuchukua sheria mkononi kwa kufanya vitendo vya kikatili ikiwemo mauaji, hasa pale wanapomkamata mhalifu ambaye anadaiwa kushiriki vitendo vya wizi kwa namna moja au nyingine.

Pia walieleza kwamba kufuatia uwepo wa jitihada za utoaji wa msaada wa kisheria na ushauri katika jamii wilayani humo, vitendo hivyo vimeanza kupungua na kwamba kinachotakiwa sasa ni Serikali kuendelea kuwaelimisha wananchi ili waachane na tabia hiyo.

Hayo yalisemwa leo na Wasaidizi hao wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wilaya ya Mbinga mkoani humo, wakati walipokuwa kwenye kikao chao wakizungumza mbele ya Wafadhili wao wa kutoka Ubalozi wa ufalme wa Sweden ambao ni Anette Windolm Bolme, Alexandra Hallqvist na Ludviq Bontell Meneja wa miradi Ubalozi wa ufalme wa Sweden na Victor Mlunde kutoka Ubalozi wa ufalme wa Norway walipotembelea katika Ofisi za kituo hicho zilizopo mtaa wa Mbuyula jengo la Mwalimu house karibu na hospitali ya wilaya hiyo mjini hapa.


“Vyombo vya dola bado ni tatizo hapa kwetu kwa kufikisha elimu kwa wananchi wasiweze kuchukua sheria mkononi, sasa kuna haja kwa vyombo hivi wafanye kazi ya ziada kuelimisha jamii wasipende kuchukua sheria mkononi kama vile haya mauaji ya kikatili”, walisema.

Akichangia hoja Daniel Chindengwike ambaye ni Mkuu wa LHRC wilayani hapa alisema kuwa kitendo cha kuanzisha Kituo cha sheria na haki za binadamu katika wilaya hiyo, imekuwa ni msaada mkubwa kwa wanambinga katika kupata haki zao za msingi ambapo watu wengi sasa wamekuwa wakikimbilia hapo kwa ajili ya kupata msaada wa kisheria.

“Hivi sasa tumekuwa tukielimisha wananchi hata Makanisani pale wanapokuwa wamemaliza ibada, wamekuwa wakipata elimu ya haki za binadamu na hili tunalifanya kwa sababu ya siku hizo za ibada mara wanapomaliza kusali kunakuwa na mkusanyiko wa watu wengi ambao ni rahisi kuwafikishia elimu hii”, alisema Chindengwike.

Naye Samweli Kayuni ambaye pia ni msaidizi wa kisheria aliongeza kuwa hata katika masuala ya kesi za mirathi, ndoa, ardhi na jinai wameweza kutoa ushauri wa kisheria kwa waathirika mbalimbali wenye matatizo hayo na kuweza kufanikiwa kupata suluhisho lenye tija katika masuala hayo ambayo yalikuwa yakiwasumbua kwa muda mrefu.

Kwa upande wake akihitimisha mazungumzo ya kikao hicho kwa niaba ya Wafadhili wenzake, Anette Bolme kutoka Ubalozi wa ufalme wa Sweden alipongeza jitihada zinazofanywa na Wasaidizi hao wa kisheria na haki za binadamu wilayani Mbinga na kueleza kwa kifupi kuwa amefurahishwa na utendaji wao wa kazi huku akiwataka waendeleze jitihada hizo.

No comments: