Na Mwandishi wetu,
Songea.
MKUU wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Cosmas Nshenye amepongeza
juhudi zinazofanywa na kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa cha 842 Mlale JKT kwa
ubunifu wao wa miradi mbalimbali ya kiuchumi, inayolenga kupunguza baadhi ya
kero zinazokikabili kikosi hicho bila kutegemea msaada wa serikali na wahisani
wengine.
Cosmas Nshenye. |
Nshenye alitoa pongezi hizo juzi wakati alipokuwa akifunga
mafunzo ya awali ya kijeshi Operesheni Tanzania ya viwanda kwa vijana 1,710 kwa
mujibu wa sheria ambao wamemaliza mafunzo yao ya miezi mitatu.
Aidha amewaagiza makamanda na askari wa kikosi hicho
kuendelea na mipango thabiti itakayoweza kuharakisha maendeleo ya mkoa huo,
ikiwemo ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa kwa wingi
katika kikosi hicho na mkoa wote kwa ujumla.
Kadhalika aliwataka vijana waliomaliza mafunzo kutumia
mafunzo hayo kwa manufaa ya Watanzania na nchi kwa ujumla kwa kukubali kujitolea
wakati wote watakapohitajika hasa katika shughuli za ulinzi.
Alisema kuwa ni matumaini ya Watanzania kuona vijana
wanaopitia Jeshi la kujenga taifa wanakuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa mstari wa
mbele katika kupambana na vitendo vya rushwa, matishio ya kiusalama kwa nchi, madawa
ya kulevya na mmomonyoko wa madili badala yake huwa wa kwanza katika kukemea
maovu yanayofanywa na wachache wasiothamini amani tuliyonayo.
Alisema Jeshi la kujenga taifa linaowajibu mkubwa wa
kuwakutanisha vijana kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na kuwaweka pamoja na
kuwafundisha masomo ikiwemo mafunzo ya kijeshi, uraia na stadi za
kazi ambapo amewapongeza wakufunzi wa vijana waliomaliza mafunzo hayo kwa
kujitoa kwa moyo wa dhati kuwafundisha vijana hao kwa kuhakikisha
wanafikia kiwango kilichokusudiwa.
Nshenye aliongeza kuwa mfunzo hayo yanayo umuhimu mkubwa
katika nchi yetu katika kuweza kujenga kizazi bora kitakachoweza kuliweka taifa
letu katika misingi iliyokuwa imara kwa Nyanja zote za kiuchumi, kisiasa, kijamii
na kiutamaduni.
No comments:
Post a Comment