Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa Tanzania ni nchi ambayo imekuwa ikiongoza kwa
uzalishaji wa mazao ya misitu Afrika Mashariki na kati, kupitia mikoa ya Nyanda
za juu kusini hivyo wananchi wanaoishi katika mikoa hiyo wanapaswa kuendelea
kupanda miti ili iweze kuwasaidia kuinua kipato chao.
Hayo yalisemwa juzi na Mshauri wa maliasili mkoa wa Ruvuma,
Afrikanus Chale wakati alipokuwa kwenye kikao cha makubaliano ya kutiliana
saini juu ya usimamizi shirikishi wa upandaji miti aina ya Milingoti
(Eucalyptus) na Mikaratasi (Pines) katika msitu wa Lihumbe uliopo kijiji cha
Lipilipili kata ya Mpepai halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani humo.
Kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya mji
huo ambapo kilifuatia baada ya wananchi wanaoishi katika kijiji hicho kuikubali
programu hiyo ambayo ni ya upandaji miti kibiashara kupitia vikundi vya
wakulima wa miti chini ya uangalizi wa halmashauri hiyo.
Akizungumzia hilo Mshauri huyo wa maliasili alisema kuwa
mradi huo wa panda miti kibiashara ni mradi ambao unatekelezwa na Serikali na
kufadhiliwa kwa pamoja kati ya Wizara ya maliasili na utalii hapa nchini na Serikali
ya Finland ambao utekelezaji wake ulianzia mwaka 2014 katika mkoa wa Njombe.
Chale alifafanua kuwa mradi huo umekuwa ukiendelea mkoani
Ruvuma katika wilaya zake hususan kwa hapa Mbinga, ambapo lengo ni kuweza
kusaidia vikundi vya wakulima ambavyo vimejikita katika shughuli za upandaji wa
miti kwa namna ambayo ni bora zaidi ili waweze kupata tija hasa katika
uzalishaji wa mazao yatokanayo na miti.
“Miti hii baadaye wananchi itawasaidia kuinua kipato chao,
tunategemea itakapokomaa halmashauri na Serikali kwa ujumla itaweza kupata
kipato wananchi wa Mbinga na maeneo jirani pia wataweza kunufaika kupitia mradi
huu”, alisema.
Alifafanua kuwa msitu wa hifadhi ya Lihumbe una jumla ya hekta
797.94 ambazo ni sawa na ekari 1,994.85 ndizo zinazotarajiwa kupandwa miti na
wananchi waliojiunga kwenye vikundi hivyo na kwamba kwa pamoja wamesaini mikataba
ya makubaliano hayo kati ya wananchi hao na halmashauri hiyo kwa kipindi cha
miaka 33.
Awali akizungumza katika kikao hicho cha makubaliano hayo Mwenyekiti
wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Kipwele Ndunguru alisema kuwa makubaliano hayo
yanalenga kuwanufaisha wanavikundi wenyewe ambapo mradi utawapatia bure miche
bora ya miti na kuipanda katika msitu huo.
Kipwele alisema kuwa miti hiyo ambayo watakwenda kuipanda
inachukua muda mfupi kuivuna hivyo wanavikundi watanufaika pale itakapofikia
hatua ya kukomaa na kuanza kuivuna kwa mfumo wa kupasua mbao au kuuza nguzo za
umeme.
Hata hivyo alieleza kuwa shughuli za upandaji miti hiyo wanatarajia
kuanza rasmi msimu wa mvua zitakapoanza mwaka huu mwezi Novemba hadi Disemba
ambapo aliwataka wanavikundi kutunza mazingira kwa kuzuia vitendo vya uchomaji
moto katika eneo ambalo miti hiyo itapandwa.
No comments:
Post a Comment