Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dokta Charles Msonde. |
Na Mwandishi wetu,
BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limetishia kuvifutia
usajili vituo vyote vya kufanyia mitihani ya darasa la saba inayotarajiwa kuanza
kufanyika kesho Septemba 6 hadi 7 mwaka huu hapa nchini.
Katibu Mtendaji wa NECTA Dokta Charles Msonde alisema hayo leo
wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya ofisi za
Baraza hilo la mitihani Mikocheni Jijini Dar es Salaam.
Msonde alisisitiza kuwa Baraza hilo linawataka wamiliki wa
shule zote hapa nchini kutambua kwamba, shule zao ni vituo maalum vya kufanyia mitihani
hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote ile kuingilia majukumu ya wasimamizi wa
mitihani hiyo.
“Baraza halitasita kukifuta kituo chochote cha mitihani
endapo litabaini na kuthibitisha pasina shaka kuwa kituo hicho kinajihusisha na
udanganyifu wa mitihani, tunatoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano kwa kipindi
hiki cha ufanyikaji wa mitihani ili wanafunzi wafanye kwa utulivu”, alisema.
Vilevile aliwaasa walimu, wamiliki wa shule, wasimamizi na
jamii kwa ujumla kutojihusisha na udanganyifu wa aina yoyote ile na kwamba kwa
wale watakaokiuka watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.
Awali alifafanua kuwa wanafunzi hao watafanya masomo matano
ambayo ni Kiswahili, Hisabati, Maarifa ya Jamii, Sayansi na somo la Kingereza ambapo
mitihani hiyo mpaka sasa imekwisha safirishwa na kupelekwa katika vituo husika.
Watahiniwa 917,072 kutoka shule za msingi 16, 583 ndiyo wanaotarajia
kufanya masomo hayo ambapo kati ya wanafunzi hao, wavulana ni 432,744 sawa na
asilimia 47.19, wakati wasichana ni 484,328 sawa na asilimia 52.81.
Watahiniwa 882,249 watafanya mtihani huo kwa lugha ya
Kiswahili na 34,823 watatumia lugha ya Kiingereza.
Jumla ya watahiniwa 94 wasioona wamesajiliwa kufanya mtihani
huo, wakiwemo wavulana 58 na wasichana 36.
Dokta Msonde alisema kuwa maandalizi yamekwisha kamilika
ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa vifaa vinavyohitajika katika halmashauri zote
nchini.
Pia amezitaka halmashauri kuhakikisha utaratibu wa uendeshaji
wa mitihani hiyo unazingatiwa kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
No comments:
Post a Comment