Waziri wa mambo ya nje Tanzania, Dokta Augustine Mahiga. |
Na Waandishi wetu,
TANZANIA imesema kwamba, imeshitushwa baada ya kuorodheshwa
miongoni mwa nchi ambazo zimechunguzwa na Umoja wa Mataifa na kuhusishwa kuwa
na uhusiano wa kibiashara na Korea Kaskazini.
Akizungumza leo katika mkutano na waandishi wa habari Jijini
Dar es Salaam, Waziri wa mambo ya nje Dokta Augustine Mahiga alisema kuwa licha
ya uhusiano uliokuwepo awali tangu mnamo mwaka 2014, Tanzania imepunguza kabisa
uhusiano wa kibiashara na kidiplomasia na nchi hiyo.
“Hatuna ugomvi na Korea Kaskazini, lakini kitendo chao cha
kutengeneza masilaha ya kuangamiza sio mazuri kwa heshima na usalama duniani,
ndiyo maana tumeanza kuchukua hizo hatua za kupunguza mahusiano”, alisema Dokta
Mahiga.
Waziri huyo aliongeza kuwa uhusiano huo wa kibiashara ulikuwepo
kabla ya vikwazo vilivyowekwa hivi karibuni na Baraza la Umoja wa Mataifa.
Waziri Mahiga alifafanua kuwa anaelekea katika mkutano wa
kawaida wa umoja wa Mataifa ambapo atatumia fursa hiyo kujibu tuhuma hizo kwa
Baraza la usalama.
Tanzania na Uganda ni miongoni mwa baadhi ya nchi zinazochunguzwa
na Umoja wa Mataifa kwa tuhuma za kwenda kinyume na vikwazo vilivyowekwa na
Baraza la usalama la umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini.
Ripoti ya uchunguzi huo ilitolewa mnamo Septemba 9 mwaka huu
ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema kwamba, linachunguza
tuhuma hizo za Tanzania kuingia mikataba ya kijeshi na Korea Kaskazini inayogharimu
dola za Kimarekani milioni 12.5.
No comments:
Post a Comment