Na Mwandishi wetu,
MSEMAJI wa Jeshi la Polisi hapa nchini, Kamishina Msaidizi wa
Polisi (ACP) Barnabas Mwakalukwa amewataka wananchi wanaofanyiwa vitendo vya
uhalifu mitandaoni wasiende Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), bali wanapaswa haraka
kutoa taarifa katika jeshi hilo ili wahalifu waweze kuchukuliwa hatua za
kisheria.
ACP Barnabas Mwakalukwa. |
Mwakalukwa alisema hayo leo alipokuwa akizungumza katika
mkutano wa pamoja na viongozi wa Mamlaka hiyo, kuhusu suala zima la uhalifu wa
makosa ya mitandao ambapo hivi sasa linaonekana kuendelea kushika kasi kubwa.
Alisema kuwa chochote kinachofanyika ambacho ni kosa la jinai
kwa watoa huduma wa mitandao ya simu mbalimbali wananchi wanapaswa kwenda
katika kituo cha Polisi kutoa taarifa ili waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye
vyombo vya kisheria kwa hatua zaidi.
Vilevile aliongeza kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia hivi
sasa vitu vingi vimekuwa vikifanyika 'online' hivyo mitandao ya kijamii
imeonekana ni muhimu kwa maendeleo, lakini pia imebadilisha mbinu ya kufanya
uhalifu katika mitandao ya kijamii kwa kutumiwa na baadhi ya watu kutapeli,
hata kutishia kuua, hivyo jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kwa ajili ya
kushughulikia makosa ambayo yanatokana na mtandao.
Hata hivyo kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa TCRA, Thadayo
Ringo naye alilishukuru jeshi la Polisi hapa nchini kwa kuweza kuwasaidia
katika kutatua changamoto mbalimbali hasa za kiusalama, huku akiwataka wananchi
watakaopata matatizo katika mtandao kwenda kutoa taarifa Polisi ili waweze
kuwasaidia kabla ya kufika kwao.
No comments:
Post a Comment