Na Muhidin Amri,
Songea.
BAADHI ya wakulima wa mahindi wilayani Songea mkoa wa Ruvuma wameipongeza
serikali kwa kuweka utaratibu mzuri juu ya suala la ununuzi wa
mahindi na bei nzuri ambao umesaidia wakulima wengi kuuza mahindi yao kwa bei
ya uhakika inayolingana na gharama ya uzalishaji.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith
Mahenge ambaye alitembelea vituo vya ununuzi wa zao hilo katika maeneo
mbalimbali wilayani Songea walisema kuwa, utaratibu uliotumika kwa Wakala wa
Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kukunua mahindi kupitia vikundi umewezesha
kazi hiyo kutoingiliwa na wajanja wachache ambao kila mwaka wamekuwa wakinunua
mahindi ya wakulima kwa bei ndogo na wao kwenda kuuza NFRA kwa bei kubwa.
Walisema kuwa licha ya serikali kuweka mgawo mdogo wa mahindi
kiasi cha tani 2,000 kwa halmashauri ya wilaya hiyo inayounda jimbo la
Peramiho, utaratibu huo umewezesha kupunguza usumbufu kwa wakulima kukaa muda
mrefu vituoni kusubiri kupimiwa mahindi yao tofauti na hivi sasa ambapo kila
mkulima anatumia kikundi chake kwa kuuza tena kwa muda mfupi.
Batholomeo Nkwera ambaye ni mwanachama wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ameipongeza serikali ya awamu ya tano
kwa umakini wake katika kushughulikia mahitaji na matatizo
mbalimbali ya wakulima na kusisitiza kuwa, hatua hiyo itaendelea kuhamasisha
wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao.
Mkulima mwingine Athanas Komba aliongeza kuwa serikali
imewatendea haki kwani licha ya kuweka mgao mdogo, hata hivyo umeepusha
malalamiko na kuwapongeza wafanyakazi wa NFRA waliopo katika vituo vya ununuzi
kwa kuwa wazi na utaratibu ambao kila mkulima ameridhika nao licha ya wengine
kukosa nafasi ya kuuza mahindi yao.
No comments:
Post a Comment