Monday, September 18, 2017

MADIWANI NA MAOFISA WATENDAJI MBINGA WATAKIWA KUSIMAMIA UBORA WA KAHAWA

Wakulima wa kahawa wakianika kahawa kwenye vichanja kabla haijapelekwa sokoni kwa mauzo.
Na Dustan Ndunguru,     
Mbinga.

MADIWANI na Maofisa watendaji wa vijiji na kata katika maeneo yao wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamesisitizwa kusimamia vyema ubora wa zao la kahawa kwa kuwahimiza wakulima kuzingatia ipasavyo kanuni bora za maandalizi ya zao hilo ikiwemo kuanika kahawa kwenye vichanja, na sio kama baadhi yao wanavyotandika mikeka chini na kuianika pale wanapoichuma kutoka shambani.

Onyo hilo limetolewa juzi na Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu kuhusiana na ubora wa zao hilo unavyopaswa kuzingatiwa kanuni zake za kilimo, hasa kipindi hiki cha msimu wa mavuno ya zao la kahawa unaondelea kufanyika wilayani humo.

Nshenye alisema kuwa kahawa ni zao ambalo limekuwa ni tegemeo kubwa kwa uchumi wa wananchi wa wilaya ya Mbinga, hivyo wakulima wanapaswa wakati wote kuzingatia maelekezo wanayopewa na wataalamu wa ugani juu ya utunzaji na uzalishaji wake wa zao hilo.


Alisema wanunuzi wa zao hilo ambao hivi sasa wamepewa kibali halali cha kununua kahawa kwa wakulima, wahakikishe wananunua kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na maeneo ya kununulia yaainishwe na sio kuingia katika mfumo wa utoroshaji kahawa ambapo kwa atakayekamatwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kufikishwa Mahakamani.

Alifafanua kuwa baadhi ya makampuni yenye kibali cha kununua kahawa yamekuwa na tabia ya kutorosha kahawa wakiwa na lengo la kukwepa kulipa ushuru ambapo kufanya hivyo huikosesha serikali mapato yake.


“Kwa wale ambao watabainika kuhusika na utoroshaji huu kamwe hawatavumiliwa hatua kali zitachukuliwa papo hapo na msimu ujao hawatapata tena leseni ya kununua zao la kahawa”, alisisitiza Nshenye.

No comments: