Haya ni mafuta Halisi ya Albino ambayo huuzwa kati ya shilingi 40,000 hadi 90,000. |
|
Na Mwandishi wetu,
Songea.
MFAMASIA wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,
Ndavitu Sanga ametahadharisha watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) waliopo katika
Manispaa hiyo, uwepo wa mafuta feki ya kupaka aina ya Sunblock Cream UV40 kwa
ajili ya Albino ambayo yanasaidia kujilinda dhidi ya Saratani ya ngozi.
Aidha Sanga ameeleza kuwa mafuta hayo feki yamekuwa yakiuzwa
kwa shilingi 3,500 hadi 6,000 na kwamba mafuta halisi ambayo sio feki yamekuwa
yakiuzwa kwa shilingi 40,000 hadi 90,000.
Sanga ambaye pia ni Mkaguzi wa vipodozi katika Manispaa ya
Songea alisema kuwa uchunguzi uliofanywa katika maduka ya vipodozi kwa
kushirikiana na uongozi wa Chama cha Albino mkoani humo, umebaini kuwa mafuta
hayo huuzwa katika maduka ya vipodozi yaliyopo mjini hapa jambo ambalo ni
kinyume cha sheria na taratibu husika zilizowekwa.
“Hairuhusiwi mafuta haya ya kupaka Albino aina ya Sunblock Cream
UV40 kuwepo kwenye maduka ya vipodozi, badala yake mafuta haya yanaruhusiwa
kuwepo kwenye maduka ya dawa ya binadamu (Pharmacy)”, alisema Sanga.
Vilevile alieleza kuwa katika kupambana na hali hiyo, kuanzia
mwaka wa fedha wa 2015/2016 halmashauri ya Manispaa ya Songea imekuwa ikitenga bajeti
ya shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya manunuzi ya mafuta hayo ambayo hugawiwa
bure kwa watu wenye matatizo ya ngozi (Albino) katika Kituo cha Afya Mjimwema.
Alifafanua kuwa bajeti hiyo bado ni ndogo kwa sababu inaweza
kununua mafuta kwa Albino 38 tu ukilinganisha na idadi ya waliopo wapo 60 katika
Manispaa hiyo.
Kadhalika katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Manispaa ya Songea
imetenga jumla ya shilingi milioni 1.68 kwa ajili ya mafuta hayo ambapo changamoto
iliyopo ni kwamba mafuta hayo hayapatikani katika Bohari ya Hifadhi ya Dawa
(MSD) badala yake yamekuwa yakiuzwa katika maduka ya dawa ya binadamu (Pharmacy).
Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonesha kwamba mkoa
wa Ruvuma una jumla ya watu wenye Albino 523 ambapo Tanzania ina zaidi ya Albino
16,000.
Albino wamekuwa wanakabiliwa na changamoto ya ugonjwa wa
kansa ya ngozi kutokana na kukosa mafuta hayo hali ambayo inasababisha maisha
yao kuwa hatarini.
No comments:
Post a Comment