Wednesday, September 6, 2017

MBOWE AMPONGEZA SPIKA NDUGAI KWA KUUNDA KAMATI NZURI YA KUCHUNGUZA TANZANITE NA ALMASI

Na Mwandishi wetu,
Dodoma.

MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe ametoa pongezi kwa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kwa kuunda kamati nzuri ya wabunge bila ya kujali itikadi zao na kuweza kurudisha ripoti ambayo itaisaidia serikali.

Freeman Mbowe.
Mbowe alisema hayo leo alipokuwa akitoa hotuba yake fupi katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya bunge hilo ya kukabidhi ripoti ya kamati hiyo ambayo ilipewa kazi ya kuchunguza biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi.

Alisema kuwa bunge hilo likiamua kufanya kazi kwa mujibu wa Katiba ya nchi linayo nafasi kubwa ya kuisaidia serikali, kwa kuunda kamati ambayo inauwezo wa kufanya kazi nzuri ya kutetea maslahi ya Watanzania.

“Mheshimiwa Spika ameisaidia serikali nina imani timu yake wanatambua bunge limejaa watu wenye uwezo mkubwa tofauti ambao wakitumika kikamilifu wanaweza wakawa msaada mkubwa kwa taifa hili katika utekelezaji wa kazi za serikali”, alisema.


Vilevile Mbowe alisema kuwa kamati hizo zimeweza kutambua madhaifu mengi katika mikataba ya kuchunguza biashara hiyo ya madini huku akidai kuwa imekuwa kawaida ya kamati teule za bunge zinapotumwa kufanya majukumu yake huwa zinapeleka ripoti zilizojaa ukweli ambazo kwa bahati mbaya wakati mwingine hazitekelezwi.

“Natambua busara ya Mheshimiwa Spika iliyompeleka mpaka aone ripoti hizi kwa unyeti wake zisisomwe tu ndani ya bunge, lakini hata watu wengine ambao ni watendaji wakuu, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama navyo viweze kushiriki kupokea ripoti hizi,

“Kwa busara hizo hizo ili ripoti hizi ziweze kupata uzito wa kibunge, tuzijadili ndani ya bunge ili wabunge sasa watoke na maazimio rasmi ambayo yatakuwa ni maelekezo ya bunge kwa serikali”, alisema.

Aliongeza kuwa kwa sababu wengi wametajwa katika ripoti hizo haki itendeke kwa wote, vyombo vyote vya umma vitakavyofanya kazi ya kusimamia jambo hili au maazimio yatakayokuwa ya bunge au maelekezo yoyote ya kibunge au serikali, vikafanye kazi kwa haki kila mmoja apate haki inayomstahili bila kuonewa mtu kulingana na changamoto inayomuhusu.

Mbowe alisema kuwa Spika wa bunge, Ndugai wakati anaunda kamati teule ya kuchunguza jambo hilo aliweza kuchanganya wabunge kutoka vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi bungeni na kuweza kuona jinsi wabunge walivyofanya kazi kwa pamoja na sio kwa misingi ya kiitikadi.


Pamoja na mengine, Mbowe ameomba ushirikiano huo usiishie hapo kwenye kamati hiyo teule bali uendelee mpaka katika kulitumikia taifa hili kwa kuwa wote ni Watanzania na nyumba wanayoijenga ni moja.

No comments: