Na Kassian Nyandindi,
Songea.
OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
imeipatia Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, zaidi ya shilingi
milioni 151 kwa ajili ya kazi ya ujenzi na ukarabati wa shule ya msingi ya watoto
walemavu wasioona iliyopo Luhira katika Manispaa hiyo.
Aidha mradi huo imeelezwa kuwa unahusisha ujenzi wa mabweni
matatu, vyoo vya ndani ya mabweni ya shule hiyo vyenye matundu 18, shimo la
choo la nje na ukarabati wa darasa moja ikiwemo uezekaji wa majengo mawili ya madarasa.
Mradi huo ambao mkandarasi wake ni Wakala wa Majengo Tanzania
(TBA) ulianza Aprili 20 mwaka huu na unatarajia kukamilika ifikapo Oktoba 20
mwaka huu na kwamba shule ya msingi Luhira ina wanafunzi mchanganyiko ambao ni
wale wanaoona na wasioona.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo,
Gisbert Ndunguru alisema jumla ya wanafunzi wanaoona wapo 1,411 ambapo kati yao
wasichana 672 na wanaume 739.
Ndunguru alieleza kuwa shule hiyo ina kitengo pia kwa ajili
ya watoto wasioona nchini ambacho kilianzishwa mwaka 1982 hata hivyo shule ya
msingi Luhira ni miongoni mwa shule kongwe nchini, ilianzishwa mwaka 1929 na
kwamba Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanzania Hayati Rashid Kawawa alisoma na kupata
elimu yake ya msingi katika shule hiyo.
Naye Mkuu wa kitengo cha wanafunzi wasioona katika shule hiyo
ambaye pia ni mlemavu wa macho, Salum Hapendeki alisema kitengo hicho kina
wanafunzi 44 wasioona kati yao wavulana ni 19 na wasichana 25 na kwamba uwezo
wa kitengo hicho ni kuchukua wanafunzi wasioona 60.
Afisa elimu maalum katika Manispaa ya Songea, Rehema Nyagawa
alisema shule hiyo kwa muda mrefu imekuwa inakabiliwa na upungufu wa matundu ya
vyoo hali ambayo ilikuwa ikisababisha watoto wa kiume kujisaidia choo kimoja na
walimu.
Pia Nyagawa aliongeza kuwa shule ina majengo chakavu ambayo
ni mabweni, jiko na bwalo la chakula na uchakavu wa magodoro na vitanda vya
kulalia wanafunzi.
Kadhalika aliipongeza serikali kwa mradi wa ukarabati ujenzi
wa mabweni na matundu ya vyoo ambao utapunguza changamoto hizo zilizokuwa kero
kubwa na kuathiri mazingira ya watoto hao.
No comments:
Post a Comment