Thursday, February 12, 2015

VYAMA VYA WAFANYAKAZI NCHINI FUNGUKENI KUSAIDIA WANACHAMA WENU



Na Mwandishi wetu,

NIMECHUKUA jukumu la kuvishauri vyama vya wafanyakazi pamoja na shirikisho la wafanyakazi hapa nchini, kutokana na hali halisi ya utatanishi kati ya waajiri na wafanyakazi katika mahusiano yao. Mahusiano hasi kati ya mwajiri na mwajiriwa yamekuwa nikawaida katika mazingira ya kazi hapa nchini.

Binafsi naamini vyama vya wafanyakazi ni kiungo kati ya waajiri na wafanyakazi hivyo kuwa daraja katika kushughulikia kero, changamoto au matatizo mbalimbali kati ya mwajiri na mfanyakazi, pia hushughulikia kutoa msaada wa kisheria kwa inapobidi.

Licha ya hapa kwetu Tanzania, kuwa na vyama vya wafanyakazi pamoja na juhudi mbalimbali za vyama hivyo bado kumekuwa na changamoto nyingi zinazowakabili wafanyakazi.

Hivyo upo umuhimu wa vyama hivyo kushirikiana na taasisi binafsi kutoa msaada wa kisheria pamoja na elimu kwa wafanyakazi, ili kuondoa hali ya manyanyaso, ukiritimba na urasimu unaofanywa na waajiri kazini.

Monday, February 9, 2015

DED TUNDURU ATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI WA KOROSHO

Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho akisisitiza jambo katika mikutano mbalimbali aliyokuwa akiifanya wilayani humo.


Na Steven Augustino,
Tunduru.

SERIKALI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imemtaka Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tinna Sekambo kuongeza nguvu katika usimamiaji wa zoezi la upandaji wa mikorosho mipya kwa wakulima wa zao hilo wilayani humo, ili waweze kuondokana na hali ya kipato duni walichonayo sasa, na hatimaye waweze kusonga mbele kimaendeleo.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho, alitoa agizo hilo wakati akimkabidhi miche ya mikorosho kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Chiza Marando ikiwa ni muda mfupi baada ya mkuu huyo wa wilaya, naye kukabidhiwa miche 30,000 yenye thamani ya shilingi milioni 85 kutoka kwa mwenyekiti wa mfuko wa kuendeleza zao la korosho Tanzania. (WAKUF) 

Aidha Nalicho alimweleza mkurugenzi huyo kuwa ili kufanikisha ugawaji wa miche hiyo kwenda kwa wakulima, maafisa ugani wanatakiwa kwenda katika vituo vyao vya kazi vijijini, na kuacha kukaa maofisini.

Mkuu huyo wa wilaya ya Tunduru, aliahidi kufanya ziara ya ufuatiliaji juu ya zoezi hilo, la upandaji wa mikorosho ambalo linaendelea wilayani humo kwa lengo la kujionea utekelezaji wake. 

WAFANYABIASHARA RUVUMA KUKAA NA WABUNGE WAO



Na Mwandishi wetu,
Songea.

WAFANYABIASHARA waliopo katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma  wamewataka wabunge wa mkoa huo, warudi kwenye majimbo yao ili waweze kujadili changamoto inayowakabili wafanyabiashara hao, juu ya ongezeko la kodi mara mbili na kiwango kilichokuwa kikitozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania. (TRA)

Akizungumza katika mkutano  uliyofanyika kwenye ukumbi wa Songea Club uliopo mjini hapa, Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Isaya Mbilinyi alisema kuwa  ongezeko hilo limefikia asilimia 100 jambo ambalo, linalowafanya wafanyabishara wengi kushindwa kumudu gharama ya ulipaji wa kodi.

Mbilinyi alisema kuwa kutokana na Bunge kupitisha kiwango hicho cha ulipaji kodi, ni vyema wabunge wa majimbo ya mkoa wa Ruvuma warudi  na kukaa pamoja na wafanyabiashara  hao ili waweze kujadili na kutambua changamoto hiyo ambayo inawakabili.

Saturday, February 7, 2015

WATU WANAODAIWA KUUNDA MTANDAO WA KIGAIDI MKOANI RUVUMA WAKAMATWA

Watuhumiwa wanaodaiwa kuunda kikundi cha ugaidi, wakipandishwa katika karandinga la Polisi mjini Songea, mkoani Ruvuma.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

WATU saba wanaodaiwa kuunda mtandao wa kigaidi katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma wamekamatwa mkoani humo, na watafikishwa Mahakamani wakati wowote, kujibu mashtaka yanayowakabili.

Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema kuwa watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa, wanatuhumiwa kuhusika na matukio matatu tofauti ya urushaji na utegaji wa mabomu ya kienyeji mkoani humo.

Msikhela alisema, tukio la kwanza lilitokea Septemba 16 mwaka jana, majira ya saa 1.30 jioni huko katika eneo la Misufini mjini Songea, ambapo kikundi hicho kinachojihusisha na ugaidi huo kiliwarushia askari polisi waliokuwa doria siku hiyo, bomu la kienyeji ambalo lilisababisha askari watatu kujeruhiwa vibaya.

TUME YA UCHAGUZI YAENDESHA MAFUNZO WILAYANI MBINGA JUU YA MFUMO WA MATUMIZI MASHINE ZA KISASA UANDIKISHAJI WAPIGA KURA

Afisa uchaguzi kutoka makao makuu ya Tume ya uchaguzi hapa nchini, Crecencia Mayalla upande wa kushoto, akitoa maelekezo kwa Waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, namna ya kutumia mashine za kisasa (BVR) ambazo zitatumika kwa ajili ya zoezi la uandikishaji wapiga kura, ambalo linatarajiwa kuanza hivi karibuni hapa nchini.


Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa makini na kufuatilia juu ya mfumo wa matumizi, mashine za kisasa (BVR) kwenye ukumbi wa Chuo cha maendeleo Mbinga mjini.

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

TUME ya Taifa ya uchaguzi hapa nchini, imeendesha mafunzo kwa Waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, juu ya mfumo wa matumizi, mashine za kisasa (BVR) ambazo zitatumika kwa ajili ya uandikishaji wapiga kura, katika daftari la kudumu mapema mwaka huu.

Mafunzo hayo ambayo yameendeshwa kwa siku mbili, katika ukumbi wa chuo cha maendeleo ya jamii wilayani humo, yanalenga uboreshaji wa daftari hilo kwa lengo la kudhibiti mianya ya udanganyifu kwa baadhi ya watu, ambao hujiandikisha zaidi ya mara moja.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Afisa uchaguzi kutoka makao makuu ya tume hiyo, Crecencia Mayalla alisema mfumo huo unarahisisha pia utendaji kazi wakati wa zoezi hilo la uandikishaji wapiga kura, ambalo linatarajiwa kuanza hivi karibuni.

“Mashine hizi zinatengeneza kadi ya mpiga kura, ambayo inamwezesha mtu kufungua akaunti benki, kumdhamini polisi, kupata paspoti ya kusafiria na hata cheti cha kuzaliwa”, alisema Mayalla.

Thursday, February 5, 2015

WANAFUNZI WANUSURIKA KUPOTEZA MAISHA BAADA YA KUVAMIWA NA NYUKI

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela.

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

BAADHI ya wanafunzi wanaosoma katika shule ya msingi Mahela, wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamenusurika kupoteza maisha yao kufuatia kundi la nyuki kuwavamia na kuwauma sehemu mbalimbali za miili yao, wakati wakiwa katika eneo la shule hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 4 mwaka huu, majira ya saa 5 asubuhi.

Msikhela alifafanua kuwa wanafunzi 71 ndio waliopatwa na mkasa huo, ambapo walikimbizwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi.

Wednesday, February 4, 2015

WADAU WA UTOAJI HAKI WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA, DC MBINGA APONGEZA MFUMO WA "MOBILE COURT"

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga akizungumza katika maadhimisho ya siku ya sheria nchini, katika ukumbi wa Mahakama ya wilaya hiyo ambapo aliitaka jamii kuzingatia haki na sheria za nchi zilizowekwa.
 
Wadau ambao walishiriki katika maadhimisho ya siku ya sheria nchini, wakiwa katika picha ya pamoja kwenye viwanja vya Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa Mahakama, serikali na wadau wa utoaji haki ikiwemo mashirika na taasisi zisizo za kiserikali na jamii kwa ujumla, ndio wenye wajibu na fursa ya kuwezesha jamii, juu ya kujua upatikanaji wa haki zao za msingi Mahakamani. 

Sambamba na hilo, mustakabali wa haki za wananchi unategemea uwajibikaji na usimamizi mzuri kwa kila mdau wa mahakama, katika kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuzingatia haki na sheria zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha mawakili binafsi wamenyoshewa kidole kuacha tabia ya kutumia vifungu vya kisheria ambavyo, vinapokonya haki ya mtu na kusababisha mlundikano wa kesi mahakamani, hasa mahabusu gerezani kwa mashauri ya jinai yasiyokuwa yalazima.

Rai hiyo ilitolewa na Hakimu mkazi mwandamizi, mfawidhi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Geofrey Mhini katika maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika wilayani humo, yakiwa na maudhui ya; fursa ya kupata haki ni wajibu wa mahakama, serikali na wadau mbalimbali.

Hakimu huyo alisema mfumo wowote imara duniani, ni lazima uzingatie haki na mfumo wa sheria ambao unajitosheleza katika kulinda haki za raia wake, pamoja na utoaji wa haki sawa kwa wakati na ukamilifu, ndio dira ya uwepo wa sheria na utawala bora.

Tuesday, February 3, 2015

UPEPO MKALI ULIOAMBATANA NA MVUA WAEZUA NYUMBA 53 TUNDURU


Na Steven Augustino,
Tunduru.

UPEPO mkali ambao uliambatana na mvu iliyokuwa inanyesha kwa masaa kadhaa, umesababisha nyumba 53 kuezuka na nyingine kubomoka katika kijiji cha Sisi kwa sisi, kilichopo kata ya Sisi kwa sisi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma na kuacha familia hazina makazi.

Aidha taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa, upepo huo umeezua nyuma 51 za bati na mbili zilizokuwa zimeezekwa kwa nyasi.

Kufuatia tukio hilo imebainishwa kuwa hasara iliyojitokeza ni ya zaidi ya shilingi milioni 53.925.

Taarifa za tukio hilo zinafanua kwamba, tukio hilo lilitokea January 27 mwaka huu, majira ya saa 10 jioni katika kijiji hicho na kuzuka taharuki kubwa kwa wakazi wa kijiji cha Sisi kwa sisi wilayani humo.

KATIKA HILI MADIWANI MBINGA TUNAPASWA KUBEBA LAWAMA, TULICHAGULIWA TUZINGATIE KANUNI NA TARATIBU ZILIZOWEKWA


Na Kassian Nyandindi,

DIWANI ni kiongozi ambaye hudumisha maendeleo ya wananchi wake katika serikali za mitaa, ikiwa ni wajibu wake muhimu kwa kiongozi waliyemchagua na wenye kujenga imani naye, katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo mbalimbali kwenye eneo husika ambalo amepewa ridhaa ya kulitawala.

Siku zote diwani akiwa kwenye baraza lililokuwa imara, hupinga vitendo vya rushwa na kuweka misingi imara ambayo hujenga uhusiano mzuri baina ya baraza na wafanyakazi wake, na haya yasipozingatiwa huleta mipasuko isiyokuwa ya lazima na hata mifarakano ambayo husababisha kuharibu wajibu wa kutathmini utendaji kazi wa idara katika halmashauri.

Wahenga wetu husema; Kibuyu kilichokuwa na shimo chini hakiwezi kujazwa na ukipanda nyasi huwezi kuvuna mchele. Maneno haya ni moja kati ya misamiati michache ambayo huelimisha namna tu tunavyotakiwa kuwa makini, katika utekelezaji na utoaji wa maamuzi katika mambo mbalimbali.

Kabla sijaenda mbali makala hii ya uchambuzi, mwandishi wetu anazungumzia juu ya mwenendo wa baraza la madiwani Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ambao wananchi wake hivi sasa wamefikia hatua ya kulalamikia kwamba wamekosa imani nao, limekosa mvuto na kupoteza mwelekeo katika baadhi ya maamuzi mbalimbali.

Mnamo Januari 23 mwaka huu, Madiwani wa wilaya hiyo walifanya baraza lao lengo ikiwa kujadili, kupitisha na kutoa maamuzi ya kimaendeleo ambayo yaliwasilishwa kwa manufaa ya wanambinga na taifa letu kwa ujumla.

Ninachotaka kuzungumzia hapa licha ya baraza hilo kutekeleza hayo, lakini agenda kuu na mwisho ilikuwa juu ya kutoa maamuzi ya kumwajibisha Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Mathias Mkali kuhusiana na tuhuma kadhaa walizokuwa wakimtuhumu ambazo zilitolewa na Mkurugenzi wake mtendaji, Hussein Ngaga.

JWTZ WATEGUA BOMU TUNDURU, WANANCHI WAKUMBWA NA TAHARUKI


Bomu lililookotwa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kisha kuteguliwa na JWTZ.

Na Steven Augustino,

Tunduru.

JESHI la Polisi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kwa kushirikiana na  Jeshi la wananchi JWTZ wametegua na kulipua bomu lenye ukubwa wa milimita 82 ikiwa ni lengo la kuzuia madhara yanayoweza kutokea baadae, kama vile usalama wananchi wa kijiji cha Wenje wilayani humo, ambako bomu hilo lilionekana.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo  Msikhela alisema kuwa bomu hilo lilionekana karibu na nyumba ya mkulima mmoja, aliyefahamika kwa jina la Ngaunje Sadick.

Alifafanua kuwa bomu hilo ni la kurushwa na bunduki yenye uwezo mkubwa, huenda lilitelekezwa katika maeneo hayo miaka ya 1960 wakati wa harakati za wapigania uhuru wa nchi jirani ya Msumbiji, na kuangukia upande wa Tanzania ambapo inaonesha halikulipuka kutokana na matatizo ya kutokuwa na nguvu.

Kamanda Msikhela alifafanua kuwa bomu liliteguliwa kwa kulipuliwa kwa kuunguzwa na moto mkubwa, uliowashwa kwa kutumia kuni nyingi huku akiongeza kuwa kutokana na kukosa nguvu na kushindwa kulipuka wakati liliporushwa, lilitoa mwanga mdogo ulioonesha kuwa tayari limekwisha haribika.

Kufuatia hali hiyo Wananchi wa mkoa wa Ruvuma, na maeneo mengine wameshauriwa pale wanapoona kitu cha ajabu mfano wa bomu, wasikiguse badala yake watoe taarifa haraka katika vyombo vya ulinzi na usalama, ambavyo vipo karibu nao.

DOKTA NCHIMBI: CCM HAINA TATIZO LA KIMUUNDO WALA MFUMO


Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya sherehe za maadhimisho ya miaka 38 ya kuzaliwa CCM, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea, Dokta Emmanuel Nchimbi akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe katika maadhimisho hayo, yaliyofanyika kitaifa juzi kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma, katikati ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho.

Na Kassian Nyandindi,

Songea.

MWENYEKITI wa maandalizi ya sherehe za miaka 38 ya Chama Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Mbunge wa Songea mjini, Dokta Emmanuel Nchimbi amesema, chama chake kina kila sababu ya kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, kwa kuwa kina mfumo na muundo imara.

Akizungumza muda mfupi baada ya maadhimisho hayo mjini Songea, Dokta Nchimbi alisema kuwa chama hicho, hakina tatizo la kimfumo wa muundo na kuongeza kuwa ushindi ni lazima.

“Chama hakina tatizo la muundo wala mfumo, tutakachofanya ni kubadilisha mikakati tu ili kujihakikishia ushindi katika uchaguzi ujao”, alisema.

Akizungumzia kuhusu kauli ya Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Jakaya Kikwete kuwataka viongozi wa chama kuwatembelea wanachama na kushawishi wanachama wapya, alisema  CCM ni chama kikubwa na ndani yake wapo viongozi waliolala ambao mwenyekiti wa taifa aliwakumbusha kuamka na kufanya kazi.

“Chama hakiwezi kuwa na maisha marefu kama viongozi katika ngazi zote hawajitumi, katika jeshi kubwa kama hili la CCM wapo watu ambao lazima wasukumwe na ndiyo hawa mwenyekiti wetu wa taifa, aliwasukuma kupitia hotuba yake.

 Alifafanua kuwa wanatakiwa kuamka na kufanya kazi kwa bidii ili kukiwezesha chama kushinda kwa kishindo, kama ambavyo kimekuwa kikishinda tangu kuanza kwa siasa za vyama vingi.

WAZIRI MKUU AFURAHISHWA NA MAENDELEO YA KILIMO BORA CHA KAHAWA SONGEA

Waziri MKuu, Mizengo Pinda.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema amevutiwa sana na kazi iliyofanywa katika muda mfupi kwenye shamba la kahawa la Aviv, lililopo kwenye kijiji cha Lipokela, wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi saba, eneo kubwa la shamba hilo limepandwa miche ya kahawa na mingine imezaa na imeshavunwa, ikilinganishwa na wakati alipofika shambani hapo Julai 2013 na kutembelea tu kitalu cha miche ya zao hilo. 

Hayo aliyasema jana, wakati alipokuwa akizungumza na wafanyakazi na menejimenti ya shamba la Aviv, baada ya kutembelea na kukagua miundombuinu ya umwagiliaji wa matone ya maji kwenye shamba hilo.

“Mkuu wa shamba hili, Bw. Medu amenieleza kwamba mpaka sasa wameshavuna kahawa mara moja na wanatarajia kuvuna tena hivi karibuni, lakini ili waweze kuanza kupata faida ni lazima wavune mara nne,

“Ndugu zangu kilimo kinataka uvumilivu na kinataka uwekezaji mkubwa.........hata kwa wakulima wadogo ni lazima kiwepo licha ya ugumu wake. Sasa ukisema kilimo ni kigumu na ukaacha kulima wakati una mke na watoto, je hao watakula wapi?”, alihoji. 

Aliwasifu wamiliki wa shamba hilo kwa kuchagua kulima zao la kahawa kwani lina walaji kila mahali ulimwenguni kote.

Sunday, February 1, 2015

PICHA ZA MATUKIO MBALIMBALI KATIKA MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA CCM SONGEA MKOANI RUVUMA

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Jakaya Kikwete, akilakiwa na maelfu ya wananchi wakati akiingia katika uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma, leo kuongoza kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM.
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akilakiwa na Katibu mkuu wa umoja wa vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda, na viongozi mbalimbali wa chama hicho wakati akiingia katika uwanja wa Majimaji mjini Songea, leo kuongoza kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM.

  Rais Jakaya Kikwete, akikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na UVCCM katika uwanja wa Majimaji mjini Songea leo, katika kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM.

  Rais, Jakaya Kikwete akiwa pamoja na viongozi wengine wa CCM wakipokea gwaride la heshima lililoandaliwa na UVCCM, katika uwanja wa Majimaji mjini Songea leo katika kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM.
Gwaride la lililoandaliwa na UVCCM likitoa heshima kwa viongozi katika uwanja wa Majimaji mjini Songea leo, wakati wa kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM.
Mwenyekiti wa Chama tawala CCM, Rais Jakaya Kikwete akihutubia maelfu ya wananchi kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea, leo katika kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM.
Msanii Diamond Platinum, akipongezwa na chipukizi wa UVCCM baada ya kutumbuiza katika uwanja wa Majimaji mjini Songea, leo katika kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM.
  Rais Jakaya Kikwete, akipokea wanachama wapya akiwa na Mbunge wa Songea mjini Dokta Emmanuel Nchimbi na Katibu mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, katika uwanja wa Majimaji mjini Songea leo, kwenye kilele cha sherehe za maadhimisho miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM. (Picha na Ikulu)

CCM RUVUMA YALIA NA UJENZI WA BARABARA YA NAMTUMBO TUNDURU

Leo bendi mbalimbali mjini Songea mkoani Ruvuma, nazo hazikuwa mbali kutumbuiza wakati wa maadhimisho ya miaka 38 kitaifa, kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Na Steven Chindiye,
Songea.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, kimemuomba Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Dokta Jakaya Kikwete kusimamia kikamilifu ujenzi wa barabara kiwango cha lami kutoka wilaya ya Namtumbo kwenda Tunduru mkoani humo, ili iweze kukamilika kwa wakati na kuufanya mkoa huo, ufunguke na kutoa fursa mbalimbali za kimaendeleo kwa wananchi wake na taifa kwa ujumla.

Hayo yalisemwa leo kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho na Mwenyekiti wa kamati ya  maandalizi ya sherehe za chama hicho Mbunge wa jimbo la Songea mjini Dokta Emmanuel Nchimbi, katika maadhimisho ya sherehe za kitaifa miaka 38 kuzaliwa kwa chama cha mapinduzi zilizofanyika kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Pamoja na mambo mengine walimpongeza Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Dokta Kikwete kwa kuupatia mkoa huo, heshima ya kuandaa maadhimisho hayo.

Maagizo mengine yaliyotakiwa kutolewa maelekezo kwa watendaji wake ni pamoja na ahadi iliyotolewa na Rais huyo, mwezi Julai mwaka jana alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo, juu ya ujenzi wa barabara kilometa 2.4 ambao hadi leo hii haujatekelezwa. 

NAPE: TUTAIBUKA NA USHINDI MNONO UCHAGUZI MKUU MWAKA HUU

Na Steven Chindiye,


Songea.

KATIKA uchaguzi mkuu ujao ambao unatarajiwa kufanyika hapa nchini, Chama Cha Mapinduzi (CCM)  kimeendelea kutamba kuibuka na ushindi mnono katika chaguzi hizo, ambazo zitahusisha Madiwani, Wabunge na Rais mwezi Oktoba mwaka huu.

Nape Nnauye ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi taifa wa chama hicho, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya kitaifa miaka 38  ya kuzaliwa kwa chama cha mapinduzi, yaliyofanyika uwanja wa Majimaji Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

NNauye ambaye alionesha kurusha vijembe hivyo kwa vyama vya upinzani akisema, kilichofanywa na CCM katika chaguzi za serikali za mitaa ilikuwa ni mvua za rasha rasha na kwamba katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, wapinzani hawata ambua kitu.

“Tayari ng’ombe amekwisha lala kibra hivyo lazima achinjwe”, alisema Katibu huyo.

HOTUBA YA RAIS KIKWETE KATIKA MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA CCM SONGEA MKOANI RUVUMA HII HAPA

Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (CCM), akiwasili katika uwanja wa Majimaji leo mjini Songea mkoani Ruvuma, katika sherehe za maadhimisho ya kitaifa miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM.
Hotuba ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Kikwete:

Mheshimiwa Makamu mwenyekikiti wa CCM, Philip Mangula Mwenyekiti wa NRM. Huyu ni rafiki yangu mkubwa, ni rubani pia. Alishawahi kunisafirisha na ndege akiwa kama rubani.

Nawashukuru wahusika wote na waheshimiwa mbalimbali mliopo hapa katika maadhimisho ya sherehe hizi.

Anammwagia sifa Mhe. Nchimbi kwa maandalizi mazuri na kuwashukuru viongozi mbalimbali wa CCM kwa kazi nzuri, akiwemo Katibu mkuu, AbdulRahman Kinana.

Nchi yetu imepiga hatua, kuna amani, utulivu na maendeleo yanayoonekana. CCM imeendelea kuaminiwa katika awamu zote. Hata mwaka huu itakuwa hivyo hivyo. Nalisema hili bila wasiwasi kabisa, roho baridiiiii.

Dalili ya mvua ni mawingu, ushindi tulioupata kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa Oktoba 2014 ni ushahidi tosha, ndugu zetu wapinzani hawana chao.

Tusikate tamaa, tunaweza kuwa na changamoto nyingi mwaka huu ila tunapaswa kuwa na ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi. Lazima tuhakikishe tuwe wamoja. Umoja ni ushindi.

Anaendelea.....

YALIYOJIRI KATIKA MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA CCM SONGEA MKOANI RUVUMA

Rais Kikwete akionesha alama ya Jembe na Nyundo, wakati anawasili uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma, katika maadhimisho ya shererhe za kitaifa miaka 38 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Kikosi maalum cha Halaiki-Makomandoo wenye umri mdogo, kikiwa kimebeba silaha za SMG kinapita mbele ya Mwenyekiti wa CCM, kumuonesha umahiri wao.
  
Dokta Emmanuel Nchimbi atoa hotuba:

Ndugu Mwenyekiti, uliagiza ujenzi wa barabara ya Manispaa bado haujatekelezwa, pia uliagiza wakulima wadogo wadogo wapewe kipaumbele kisha mawakala na ulitoa pesa takribani bilioni 7.7, tunakushukuru sana.

Mhe Rais, Wananchi wa Songea wanapenda sana mpira na wana timu yao ya majimaji, nimepata mdau kutoka marekani aliyetuchangia Milioni 150, hivyo kwako rais hatutaki chochote zaidi ya dua tu. (makofi).

Saturday, January 31, 2015

WAZIRI MKUU AWASILI MJINI SONGEA KUSHIRIKI SHEREHE ZA KITAIFA KUZALIWA KWA CHAMA CHA MAPINDUZI

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwasili katika uwanja wa ndege mjini Songea mkoani Ruvuma, na kulakiwa na Katibu wa Itikadi na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye, kushiriki maadhimisho ya miaka 38 ya kuzaliwa CCM yanayofanyika kitaifa leo mkoani humo na mgeni rasmi ni Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete. kulia ni Katibu mkuu wa chama hicho Abdulrahman Kinana.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akiwapungia mkono wananchi na wanaccm waliofika kumlaki uwanjani hapo.

Vikundi vya sanaa vikitumbuiza wakati wa mapokezi ya Pinda, Kinana na Philip Mangula.

Thursday, January 29, 2015

MGOMO WA WENYE MADUKA WAZIDI KUSAMBAA NCHINI

                                    Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.
Na Waandishi wetu, 
 
MGOMO wa Wafanyabiashara wa mduka umesambaa mikoa kadhaa hapa nchini, kupinga matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs).

Mgomo huo ulioanzia kwa wafanyabiashara wa maduka Kariakoo Jijini Dar es Salaam kuanzia juzi, kupinga Mwenyekiti wao Johnson Minja, kukamatwa na polisi, sasa umesambaa hadi miji ya Mwanza, Iringa, Songea na Dodoma.

APANDISHWA KIZIMBANI:

Minja (34) jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma kwa makosa mawili, likiwamo la kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa kutumia EFDs na kusomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Rebbeka Mbiru.

Wakili wa Serikali, Godfrey Wambari alidai kuwa Septemba 6 mwaka 2014 katika ukumbi wa Chuo Cha Mipango Dodoma alitenda kosa la kushawishi wafanyabiashara, kutenda kosa la jinai kwamba wasilipe kodi.

Katika shitaka la pili, siku na mahali pa tukio la kwanza mshtakiwa anadaiwa kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mashine za EFD. Upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi la dhamana.

Mshtakiwa alikana mashitaka yake;

Hakimu Mbiru alisema mshtakiwa huyo, atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili akiwemo mtumishi wa serikali mmoja, watakaosaini hati ya dhamana ya shilingi milioni nne.

Wakili wa utetezi, Godfrey Wasonga alidai kuwa mshtakiwa ni mfanyabiashara maarufu nchini na kwamba anaaminika hawezi kutoroka, hivyo mahakama ipunguze masharti ya dhamana.

Hata hivyo, mshtakiwa alitimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa Februari 11, mwaka huu.

BABA KANUMBA: NILIMTEMEA MATE KABROTHER AWEZE KUFANIKIWA KATIKA KAZI ZAKE

Msanii wa filamu nchini, Senga upande wa kulia akiwa na msanii mwenzake katika picha ya pamoja, Gidion Kabrother.
Na Kassian Nyandindi,

Ruvuma.

CHARLES Kanumba ambaye ni baba wa aliyekuwa nguli wa filamu hapa nchini, Marahemu Steven Kanumba amefunguka akisema kuwa alimtemea mate msanii Gidion Simon maarufu kwa jina la Kabrother, ili aweze kufanikiwa katika kazi zake za uigizaji wa filamu kama alivyokuwa mwanae Kanumba.

Alisema aliamua kufanya hivyo, ili ikiwezekana amrithi mwanae huyo ambaye alikuwa ni rafiki yake kipenzi akishirikiana na mwanae, katika kazi za uigizaji wa filamu kwa muda mrefu.

“Nilimtemea mate huyu mtoto, kwa sababu katika kazi zake alikuwa mtu wa karibu sana na mwanangu wakishinda hapa nyumbani, hivyo niliona nifanye hivi niweze kumpatia baraka na Mungu akimbariki aweze kuonyesha maajabu kama mwenzake”, alisema.

Alifafanua kuwa, Kabrother wakati anaanza kazi zake za uigizaji alikuwa akijifunza kupata ujuzi wa fani hiyo, kutoka kwa marehemu Kanumba.

Hayo yalisemwa na Baba Kanumba, wakati alipokuwa akizungumza na mtandao huu kwa njia ya simu ambapo aliongeza pia kwa kuwataka waigizaji wa filamu hapa nchini, kuwa na ushirikiano katika kazi zao ili waweze kusonga mbele katika tasnia yao ya sanaa na maigizo ya aina mbalimbali.

“Namsifu Kabrother kwa juhudi anazozifanya, ameanza kazi hii kwa muda mrefu mpaka hapa alipofikia katika kukuza kipaji chake”, alisema Baba Kanumba.