Sunday, February 1, 2015

NAPE: TUTAIBUKA NA USHINDI MNONO UCHAGUZI MKUU MWAKA HUU

Na Steven Chindiye,


Songea.

KATIKA uchaguzi mkuu ujao ambao unatarajiwa kufanyika hapa nchini, Chama Cha Mapinduzi (CCM)  kimeendelea kutamba kuibuka na ushindi mnono katika chaguzi hizo, ambazo zitahusisha Madiwani, Wabunge na Rais mwezi Oktoba mwaka huu.

Nape Nnauye ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi taifa wa chama hicho, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya kitaifa miaka 38  ya kuzaliwa kwa chama cha mapinduzi, yaliyofanyika uwanja wa Majimaji Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

NNauye ambaye alionesha kurusha vijembe hivyo kwa vyama vya upinzani akisema, kilichofanywa na CCM katika chaguzi za serikali za mitaa ilikuwa ni mvua za rasha rasha na kwamba katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, wapinzani hawata ambua kitu.

“Tayari ng’ombe amekwisha lala kibra hivyo lazima achinjwe”, alisema Katibu huyo.


Awali wakitoa burudani kwa wananchi waliofurika mjini Songea kwenye uwanja wa Majimaji, wakiwemo wapenzi na wakereketwa wa chama cha mapinduzi, bendi ya TOT inayomilikiwa na chama hicho, walikuwa wakiimba wimbo wa kupongezwa kwa utekelezaji wa sera za chama huku watu wengi wakishangilia na kufurahi.

Katika wimbo huo pamoja na mambo mengine,  walitaja baadhi ya mafanikio yaliyotekelezwa na chama tawala kupitia serikali yake ya awamu ya nne kuwa kimejenga shule nyingi, hospitali, vituo vya afya na zahanati ikiwa ni juhudi ya kuhakikisha wananchi wake wanapatia huduma nzuri.

Mwenyekiti CCM Taifa naye azungumza:

Mwenyekiti wa Chama hicho Dokta Jakaya Kikwete, wakati akihutubia maelfu ya wanachama na wakereketwa wa CCM waliojitokeza kushiriki maadhimisho hayo, alisema, “dalili ya mvua ni mawingu kwani ushindi mkubwa kilioupata chama cha mapinduzi CCM  katika uchaguzi wa serikali za mitaa, ni kielelezo tosha cha ushindi mwaka huu”.

 Dokta Kiwete, amewataka wanaccm wasibweteke kwa ushindi huo, badala yake waunganishe nguvu zao kwa kufanya kazi pamoja, ili kujihakikishia ushindi huo unapatikana tena katika uchaguzi ujao.

Alifafanua kuwa huu ni mwaka ambao lazima kazi ya jumuiya za chama cha mapinduzi, zinazokiwezesha chama hicho kushinda, lazima zifanye kazi zinazo onekana na kuonesha dira katika ushindi wa chaguzi zijazo.

Kadhalika aliwataka viongozi wa CCM waliopo madarakani, kujipima kuwa wapo katika kundi gani katika utekelezaji wa yale waliyoahidi kwa wananchi huku akiongeza kuwa mwaka huu, ni mwaka wa uchaguzi ambao wapiga kura watawahukumu viongozi waliopo madarakani kwa mambo waliyoyatekeleza ambayo walitoa ahadi kwa wananchi wao, katika uchaguzi mkuu uliopita.

No comments: