Thursday, February 12, 2015

FISI ALETA MAAJABU TUNDURU, WANANCHI WAINGIWA HOFU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mnyama mkali ambaye ni Fisi wa ajabu, amevamia kijiji cha Malombe wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, na kuanzisha tabia ya kuwapigia hodi wakazi wa kijiji hicho nyakati za usiku, na inapotokea wanafungua mlango huwadhuru kwa kuwajeruhi.

Sambamba na hilo mnyama huyo amekuwa na tabia mpya ya kwenda kufukua makaburi ya watu ambao wamekuwa wakizikwa, katika makaburi yaliyopo kijijini hapo.

Kwa mujibu wa taarifa za matukio hayo, imeelezwa kuwa fisi huyo alianza kuonekana mwanzoni mwa mwezi huu, hali ambayo imekuwa ikiwafanya wananchi wa kijiji hicho kuishi katika hofu kubwa.


Akizungumzia tukio hilo Diwani wa kata ya Mlingoti Magharibi, Mchemela Abdallah alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo, alizipeleka katika ofisi ya idara ya ardhi na wanayamapori wilayani humo, ili wawasaidie kumuondoa fisi huyo kabla hajasababisha madhara makubwa kwa wananchi.

Mchemela alilitaja tukio la kusisimua la fisi huyo kufukua kaburi la marehemu, Said Daimu Mjase ambaye aliyefariki na kuzikwa katika makaburi yaliyopo kijijini hapo, kuwa lilitokea Februari 3 mwaka huu.

Alisema sambamba na mnyama huyo kufanya matukio hayo, pia amekuwa akishika mbuzi, mbwa ambapo hadi sasa amekwisha kamata mifugo ya watu wa    nne ambao ni wakazi wa kijiji cha Malombe.

Alipotakiwa kuzungumzia matukio hayo Kaimu afisa wanyamapori, hamashauri ya wilaya ya Tunduru, Peter Matani pamoja na mambo mengine alikiri kuwepo kwa matukio hayo na akaongeza kuwa tayari amekwisha peleka askari wa idara hiyo, ili kumsaka na kumuua fisi huyo kabla hajaleta madhara makubwa kwa wananchi.


No comments: