Monday, February 16, 2015

HATIMAYE WATUHUMIWA MATUKIO YA KIGAIDI SONGEA WAPANDISHWA KIZIMBANI

Watuhumiwa wa kurusha mabomu katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wakisubiri kusomewa mashtaka yao katika Mahakama ya mkoa huo.


Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

KIKOSI cha kutuliza ghasia (FFU) mkoani Ruvuma, hivi karibuni kimeweka ulinzi mkali katika Mahakama ya mkoa huo, wakati watuhumiwa sita waliojihusisha na vitendo vya ugaidi, kutegesha na kulipua mabomu Manispaa ya Songea mkoani humo, ambayo waliyatengeneza kienyeji, katika matukio matatu tofauti na kujeruhi baadhi ya askari.

FFU walikuwa wamezingira Mahakama hiyo, kwa kushirikiana na askari polisi huku watu wakizuiwa kuzunguka au kupita, kwenye eneo hilo la mahakama.

Mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya mkoa wa Ruvuma, Simon Kobelo, na mwendesha mashtaka ambaye ni wakili mfawidhi wa serikali kutoka ofisi ya Mwanasheria mkuu kanda ya Songea, Silvanus Mkude ambapo kesi hiyo ilikuwa ikinguruma, huku wakitajwa washtakiwa waliohusika katika tukio hilo la ulipuaji wa mabomu katika mji huo.


Watuhumiwa hao ni;  Juma Kibwana maarufu kwa jina la Msabila, Mwalimu Yusuph, Hamza Singano, Yassin Mussa maarufu kwa jina la Kafupi, Hassan Mponda na Said Steven Mhando wote wakazi wa manispaa hiyo.

Wakili Mkude alidai Mahakamani hapo kuwa, washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka ya matatu tofauti ya kujaribu kuwaua askari Polisi, ambao walikuwa doria wa kikosi cha barabarani waliokuwepo kwenye eneo la kazi, huko eneo la Mshangano Songea.

Kosa la kwanza linalowakabili ni la kujaribu kuua, mnamo Desemba 25 mwaka jana katika eneo la mtaa wa kotazi Majengo, watuhumiwa hao mmoja kati yao alijaribu kuwarushia bomu lililotengenezwa kienyeji askari Polisi waliokuwa wanafanya doria na kabla hajafanikiwa kurusha bomu hilo, lilimlipukia yeye mwenyewe na kumsababishia kifo papo hapo na askari Polisi wawili kujeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.

Shtaka la pili, mnamo Octoba 27 mwaka jana majira ya jioni, lilichimbiwa ardhini bomu la kienyeji eneo la Mshangano kando kando ya barabara ya Kutoka Songea kwenda Njombe, ambalo eneo hilo hutumiwa ukaguzi wa magari yanayotoka na kuingia Songea mjini kwa lengo la kuwalipua askari na kabla hawajatimiza adhma hiyo, askari waligundua na kulitegeua haraka ili lisiweze kuleta madhara.

Alilitaja shtaka la tatu, ambalo linawakabili watuhumiwa hao kwamba wanadaiwa kuwa Septemba 16 mwaka jana, majira ya saa 12:00 jioni huko katika kata ya Misufini Matarawe mjini Songea, waliwarushia bomu la kutengenezwa kienyeji askari waliokuwa kazini na kusababisha askari watatu kujeruhiwa.

Hata hivyo kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za kigaidi, washtakiwa hawakuweza kujibu mashataka hayo yanayowakabili na kwamba kesi hiyo itatajwa tena Februari 19 mwaka huu, na wote wamerudishwa rumande.

No comments: