Sunday, February 22, 2015

WATUMIAJI WA ARV WATAKIWA KUFUATA MAELEKEZO YA WATAALAMU



Na Amon Mtega,
Songea.

WATU wanaotumia dawa za kurefusha maisha (ARV) mkoani Ruvuma, wametakiwa kufuata maelekezo ya watalaamu wao, namna ya kutumia dawa hizo na kuachana na maelekezo yanayotolewa na watu wengine mitaani, ili waweze kuepukana na madhara yanayoweza kutokea baadaye.   

Wito huo ulitolewa na Mratibu wa magonjwa ya kifua kikuu na UKIMWI, wilaya ya Songea mkoani humo, Adam Ngunga kwenye mafunzo elekezi kwa wanachama zaidi ya 80 kutoka sehemu mbalimbali mkoani Ruvuma, wa shirika lisilokuwa la kiserikali (DMI) yaliyofanyika mjini hapa.

Wanachama hao walielekezwa namna ya kuepukana na maambukizi ya ugonjwa huo, pamoja na matumizi ya dawa za ARV kwa mgonjwa ambaye tayari anastahili kutumia dawa hizo, mara baada ya kushuka kwa  kinga zake mwilini.


Mafunzo hayo yalieandana na wanachama kupima afya zao na kuwataka huko waendako wakaelimishe jamii, juu ya matumizi sahihi ya dawa za UKIMWI ili kuondokana na malalamiko yasiyokuwa na msingi ambayo hujitokeza miongoni mwa jamii, hasa pale mgonjwa anapozembea kutumia dawa hizo.

Ngunga alisema, hali hiyo imekuwa ikiwasumbua wengi wao ambao hupuuza maelekezo ya watalaamu, na kuwafanya kuwepo kwa mabadiliko ndani ya miili yao na kuchukia dawa ambazo huzitumia, huku wengine wakipoteza maisha.

Alifafanua kuwa pamoja na kuwepo kwa baadhi ya watu kupuuzia maagizo yanayotolewa na daktari, pia amewataka wajenge utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara, ili waweze kujitambua na kufanya maamuzi yaliyo sahihi katika maisha yao ya kila siku.

No comments: