Wednesday, February 18, 2015

JENISTA: HAMASISHENI WANANCHI WAJIANDIKISHE KATIKA DAFTARI LA WAPIGA KURA

Jenista Mhagama.


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WAZIRI wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama amewataka viongozi wa Jumuiya ya wazazi, vijana na umoja wa wanawake Tanzania (UWT) kuhakikisha wanafanya kazi ya kuhamasisha wananchi, kwenda kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kuipigia kura katiba pendekezwa, ili kutoa fursa ya upigaji kura kwa wananchi  wengi hasa katika kipindi cha uchaguzi mkuu ujao.

Jenista ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alitoa wito huo, wakati alipokuwa kwenye hafla fupi ya kupongezwa kwake kuwa katika nafasi hiyo ya uwaziri, iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa parokia ya  Bombambili, Manispaa ya Songea  mkoani Ruvuma.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wote wa jumuiya za CCM, ambapo alisema pamoja na mambo yote ya maendeleo ambayo yanafanywa na serikali, kazi iliyobaki katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ni kuhakikisha wananchi wanajiandikisha kwenye daftari la kupigia kura, pamoja na kuipigia kura katiba pendekezwa.


“Kama viongozi wa jumuiya za chama hiki tutasimama kidete kuhamasisha wananchi kwenda kujiandikisha kwenye  daftari hili, tutakuwa tumetoa fursa kubwa kwa wapiga kura kushiriki kikamilifu katika zoezi hili, ambalo lipo mbele yetu na hatimaye kukifanya chama chetu kiendelee kushika dola”, alisema Jenista.

Aidha Waziri  huyo licha ya kutoa wito huo, aligawa baiskeli 19 zenye thamani ya shilingi milioni 2.2 kwa jumuiya ya wazazi ikiwa ni mwendelezo wa  ahadi zake ndani ya chama, ambapo katika kipindi cha nyuma tayari alishagawa baiskeli hizo kwa jumuiya nyingine za  vijana na UWT kwa kila kata, kwenye jimbo lake.

Kwa upande wake katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Songea, Rajabu Uhonde alipozungumza kwenye hafla hiyo alisema kuwa chama chake kimejipanga vizuri kuhakikisha maagizo yote yaliyotolewa  toka ngazi ya taifa yanafanyiwa kazi, kwa utekelezaji na aliwaonya wale wote ambao wameonesha  nia ya kutaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi  mkuu ujao, wasubiri mpaka muda utakapofika vinginevyo wakionekana wanajipigia debe kabla ya wakati, watachukuliwa  hatua za kinidhamu ndani ya chama.

No comments: