Thursday, February 26, 2015

VIONGOZI WATAKIWA KUJIPIMA NINI WAMELIFANYA KATIKA TAIFA HILI


Na Nathan Mtega,

Songea.

IMEELEZWA kuwa viongozi wa ngazi mbalimbali nchini, wametakiwa kujipima katika utendaji wao wa kuwatumikia wananchi pamoja na wanaowaongoza kama wanatekeleza majukumu yao ipasavyo, kwa uadilifu na moyo wa uzalendo katika taifa hili kama walivyofanya wa asisi wetu akiwemo, Hayati Rashid Mfaume Kawawa.

Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko alisema hayo wakati alipokuwa akifungua tamasha la kumuenzi Hayati Rashid Kawawa linaloenda sambamba na kuwakumbuka mashujaa wa vita ya Maji maji, yanayofanyika mjini Songea mkoa humo ambayo yameanza kwa wajumbe wa kamati hiyo ya maandalizi inayofanya kazi chini ya Mwenyekiti wake, Fredrick Mwakalebela kwa kutembelea baadhi ya maeneo ambayo muasisi huyo aliishi na kufanya kazi mkoani hapa.

Alisema ni vyema wakati taifa linawakumbuka viongozi na waasisi wake pamoja na mashujaa wa vita hiyo, ambayo ndiyo ilikuwa chachu ya ukombozi wa bara la Afrika kila mmoja kwa nafasi yake katika jamii ajitafakari kama anatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, utawala bora pamoja na moyo wa uzalendo kama walivyokuwa waasisi wa taifa hili, ambao huenziwa kila mwaka.

Bendeyeko alisema ili tamasha hilo na maadhimisho ya kumbukumbu ya kuwaenzi mashujaa hao, yaweze kuwa na tija ni muhimu kwa kila mmoja kuhakikisha anaguswa na moyo wa uzalendo waliokuwa nao waasisi hao pamoja na mashujaa hao.


Alifafanua kuwa Hayati Rashid Kawawa, alikuwa na moyo wa kujitoa kama walivyojitoa mashujaa wa vita ya Majimaji ambayo ndiyo ilikuwa chachu ya ukombozi wa taifa letu na bara la Afrika huku kila mmoja anapaswa kujionja katika uongozi wa serikali na sekta binafsi, anajitoa kwa kiasi gani kwa ajili ya kutetea taifa na kujiepusha na ubinafsi usio na tija kwa jamii anayoiongoza.

Kama mashujaa wa vita hivyo pamoja na waasisi wake akiwemo Hayati Rashid Kawawa aliyejulikana pia kama simba wa vita, wasingekuwa na moyo wa kujitoa leo kiizazi kilichopo kisingeweza kufaidi matunda ya kujitoa kwao na taifa lingekuwa katika hali mbaya.

Awali naye mkurugenzi mkuu wa makumbusho hayo, Profesa Mabula alisema lengo lake ni kujenga makumbusho ya kuwaenzi viongozi wa kitaifa, katika sehemu moja ili kuendelea kudumisha historia yao kwa kizazi kilichopo na kijacho.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni; miaka mia moja na kumi ya vita vya maji maji na simba wa vita Rashid Mfaume Kawawa mzalendo wa kweli.

No comments: