Monday, February 16, 2015

DED SONGEA NA MIKAKATI YA KUKAMILISHA UJENZI WA MAABARA



Na Stephano Mango,
Songea.

HALMASHAURI ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, imetoa shilingi milioni 259.5 kwa ajili ya utekelezaji ujenzi wa maabara, kwa shule za sekondari 23 ambazo zipo katika halmashauri hiyo, ili kuweza kukamilisha zoezi la ujenzi wa miundombinu yake.

Akizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika hivi karibuni mjini hapa Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Sigsiberth Valentine alisema halmashauri inaendelea kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete, ujenzi wa maabara tatu kwenye kila shule ya  Sekondari wilayani humo.

Valentine alisema, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana, halmashauri yake ilikwishatoa fedha na vifaa vya viwandani, vyenye thamani ya shilingi milioni 259,582,239 kwa ajili ya kazi hiyo.


Alisema kuwa fedha hizo zimetumika kuwalipa mafundi na ununuzi wa vifaa hivyo, na kwamba kilichobaki sasa asilimia kubwa ni ujenzi wa miundombinu ya vyumba vya maandalizi (Preparation rooms) katika maabara hizo, kufunga mitungi ya gesi na kupaka rangi majengo hayo.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa sekondari zingine zipo kwenye hatua ya mwisho wa ujenzi, na taratibu za kukamilika zinaendelea kwa kasi ili kuweza kufikia lengo husika.

Alizitaja shule ambazo zinajengwa maabara hizo katika wilaya ya Songea kuwa ni; Nguruma, Maposeni, Nalima, Magingo, Lipupuma na Gumbiro ikiwa zote ni za kata.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Rajabu Mtiula aliwataka wakuu wake wa idara kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati, wasimamie vyema rasilimali zote zinazotolewa na serikali, ili kuweza kukamilisha kazi hiyo ipasavyo na kwa viwango vinavyokubalika.

Mtiula alisema kila mkuu wa idara anapaswa kutumia nguvu zake zote kuhakikisha ujenzi huo unafanikiwa, kwani licha ya kuwa ni agizo la Rais lakini ni muhimu kwa faida ya kizazi hiki cha sasa, kijacho na taifa kwa ujumla.

No comments: