Wednesday, February 18, 2015

MEYA MANISPAA SONGEA AWAPA SOMO MADIWANI WENZAKE, WAPITISHA BAJETI YAO


Na Stephano Mango,
Songea.

MADIWANI katika Halmashauri ya Manispaa  ya Songea  mkoani Ruvuma, wamepitisha bajeti ya shilingi 41,886,830,984 kutoka kwenye vyanzo vyake mbalimbali vya mapato, ambayo itatumika, kipindi cha mwaka 2015/2016. 

Akisoma bajeti hiyo kwenye kikao cha baraza la madiwani, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo mchumi wa  Manispaa hiyo, Raphael Kimary alisema mchanganuo wake, unatokana na vyanzo vya mapato vya ndani katika halmashauri kiasi cha shilingi 3,259,613,000.

Kadhalika alieleza kuwa mishahara ni shilingi 24,710,969,400 matumizi mengine toka serikali kuu shilingi 2,296,844,000 ambapo ruzuku ya miradi mbalimbali ya maendeleo shilingi11,619,404,584  ikiwemo na vyanzo vya ndani vya halmashauri hiyo ni shilingi 3,259,613,000.


Kimary  alifafanua kuwa vipaumbele vyao ni kukamilisha miradi viporo ambayo haikukamilika ujenzi wake, yakiwemo majengo ya zahanati na vituo vya afya, ukarabati wa ofisi kuu, kata na mitaa, ujenzi wa vivuko vya madaraja, sekondari, shule za msingi, pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu. 

Mchumi huyo alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuboresha mitandao ya barabara kwa kiwango cha lami, kwenye kata mpya ambazo zimeongezwa  ili ziweze kupitika kwa urahisi hasa  kwa kata ambazo zipo mbali na makao makuu na Manispaa hiyo.

Kadhalika wataendelea kutekeleza mpango wa serikali wa tekeleza sasa kwa matokeo makubwa katika sekta ya kilimo, elimu, maji pamoja na mapato.

Awali Meya wa Manispaa hiyo, Charles Mhagama mara tu baada ya madiwani wote kuridhia kupitisha bajeti hiyo aliwataka kuonesha mfano mzuri, kuwa mstari wa mbele mwaka huu ambao unaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais katika kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu shughuli mbalimbali za maendeleo, ambazo zitaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa manispaa  hiyo kusonga mbele na madiwani wote kurudi kwenye baraza hilo kwa mara nyingine.

Mhagama  ambaye  pia ni diwani wa kata ya Matogoro, alisema hivi sasa ni vyema kila diwani akajitahidi kumalizia viporo vya miradi ya maendeleo kwa wananchi wake, ili aweze kujenga imani hasa kwa wapiga kura, ambao wataweza kumchagua tena katika chaguzi zijazo.

No comments: