Sunday, February 22, 2015

WAKUU WA WILAYA WATEULE WATAKA USHIRIKIANO WASEMA WAPO TAYARI KUCHAPA KAZI

Rais Jakaya Kikwete.

Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

WAKUU wa wilaya wateule, ambao wanakwenda kuchukua nafasi ya mkuu wa wilaya ya  Mbozi, Ahamad Namohe na Mariam Jumaa aliyepangiwa kwenda wilaya ya  Lushoto, kwa nyakati tofauti wamewataka wananchi wa wilaya hizo kutoa ushirikiano wa kutosha kwao, ili waweze kusimamia kikamilifu shughuli za kimaendeleo wakati watakapokuwa katika maeneo hayo. 

Sambamba na maelezo hayo, pia wateule hao walisema watazingatia wanatekeleza majukumu yao ya kazi kwa kuhakikisha hawata muangusha, Rais Jakaya kikwete ambaye aliwateua katika kutekeleza na kusimamia maendeleo ya wananchi wake hususani kwenye nyanja ya elimu, afya na maji na mambo mengine mengi huko waendako.

Aidha katika mahojiano hayo, walitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais huyo kwa kuwaona na kuwaamini kuwa wanao uwezo, wa kuitumikia nchi yao.


“Nafasi niliyopewa ni adimu sana, binafsi nina amini kuwa kazi niliyopangiwa nitaifanya kwa uangalifu na uaminifu mkubwa, na kuhakikisha wilaya ninayokwenda inapiga hatua mbele kimaendeleo,” alisema Namohe.

Pamoja na mambo mengine, wakuu hao wa wilaya walionesha kujiamini katika maelezo yao wakisema kuwa kazi wanazoenda kufanya, hazina tofauti na kazi za uafisa tarafa walizokuwa wakizifanya, katika maeneo yao wilayani Tunduru.

“Hakuna kazi ngeni kwetu, kwani wakati tukiwa maafisa tarafa tulikuwa tunafanya vikao vya kujadili hali ya ulinzi katika kata zetu na kuhakikisha amani na maendeleo yanapatikana sehemu husika”, alisisitiza Mariam.

No comments: