Saturday, February 14, 2015

WASIOPELEKA WATOTO KIDATO CHA KWANZA KUKIONA CHA MOTO



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKUU wa wilaya ya ya Tunduru mkoani hapa, Chande Nalicho ametoa wiki mbili kwa wazazi wilayani humo, wahakikishe kwamba wanawapeleka watoto wao ambao wamechaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari kidato cha kwanza mwaka huu, na kwa asiye tekeleza hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Nalicho alitoa kauli hiyo, wakati alipokuwa akitoa salamu za serikali kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo, kilichofanyika ukumbi wa Klasta ya walimu mlingoti mjini hapa. 

Akifafanua taarifa yake, Mkuu huyo wa wilaya alisema maagizo hayo ameyatoa kufuatia kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi ambao hawajaripoti katika shule walizochaguliwa kwenda kusoma, huku takwimu zikionesha ni asilimia tano tu ndio waliokwenda kuripoti na kuanza masomo kati ya asilimia 54.1 ya watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.


Kutoripoti kwa watoto hao, kunaondoa sifa kwa wilaya hiyo kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba.

Alisema katika matokeo hayo wilaya yake imefaulisha watoto 2,573 ambapo kati yake, wavulan ni 1,403 na wasichana 1,173 ikiwa ni tofauti na mwaka 2014 ni zaidi ya mara mbili, ambapo wilaya ilifaulisha watoto 1,364 na kushika nafasi ya mwisho kiwilaya. 
  
Sambamba na agizo hilo la Nalicho, kadhalika aliwataka madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru kuongeza nguvu katika kuendelea na uhamasishaji wa ujenzi wa maabara, katika shule za sekondari wilayani humo na kuhakikisha ujenzi wake unakamilika kwa wakati.

No comments: